Mgeni Mtukufu Ramadhani Yuko Mbali na Dhihaka za Wanademokrasia
Ramadhani tayari imeingia, kama kawaida wanademokrasia wameanza dhihaka na dharau zao kwa mgeni huyu adhimu na Uislamu kwa jumla. Viongozi wa kidemokrasia katika madola makubwa kama Uingereza, Marekani, Ufaransa, Canada nk na wakala wao kama kawaida yao hujifanya kupaza sauti zao ati kutuma salamu za kuwatakia Waislamu kheri ya kuingia Ramadhani. Aidha, hata hapa petu tunawasikia wengi kutoa salamu za Ramadhani Kariim. Si hayo tu bali pia tutaona maandalizi ya futari kutoka kwa viongozi hao wa kidemokrasia ati kwa ajili ya Waislamu.
Tunasema hii ni dhihaka, dharau na shere kubwa kwa Umma wa Kiislamu na mfumo wake, kwa kuwa madola kama Marekani na washirika wake na hata wafuasi wao katika nchi changa kila dakika wako mbioni kuuangamiza Ummah wa Kiislamu na mfumo wao. Iweje kuwatakia Waislamu kheri katika ibada ya Ramadhani ilhali kile kinachoilinda na kudhamini ladha ya Ramadhani ambacho ni dola ya Khilafah wanaipinga kurejea kwake kwa nguvu na gharama zote? Waislamu pia kupewa salamu kutoka mabunge ya kidemokrasia ni jambo la kushangaza sana, kwa kuwa imani ya kisekula ya mabunge ya kidemokrasia inapingana moja kwa moja na aqida ya Kiislamu, hasa ukitilia maanani kuwa Ramadhani ni mwezi ulioshushwa muongozo kwa watu wote. (huda li-nasi)
Mfumo wa kibepari na nidhamu yake ya kidemokrasia kamwe hauthamini, haujali wala hauheshimu na hautoheshimu mwezi wa Ramadhani. Wao na mfumo wao ndio huruhusu na kudhamini kila aina ya uchafu na ufuska katika ulimwengu hata ndani ya kipindi cha mwezi mtukufu ”mgeni mwema”. Tunashuhudia dhulma zao za kiuchumi, uvamizi wa biladi za Waislamu kama Syria, Iraq, Somalia, Afghanistan nk. na kuunga mkono kwao vibaraka wanaoangamiza Waislamu kama ndani ya Yemen, Turkistan ya Mashariki, Myanmar, Palestina nk. Mfano hai wa kuhuzunisha wa karibuni, wakati Waislamu sehemu nyengine wanaanza Ramadhani, ndani ya Syria na Gazza Waislamu wanakula mabomu na makombora. Haya yote ni katika vipingamizi katika kuifanikisha ibada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa Waislamu.
Aidha, upinzani wa nchi za magharibi dhidi ya ujumbe wa Uislamu uko wazi wazi, wakijizatiti kwa kila aina ya vita kijeshi, kifikra, kithaqafa na kisheria ili kufikia lengo lao la kuizima kabisa nuru yake. Bila ya kusahau kuwa wao ndio wanaozuiya ulinganizi wa Uislamu kwa propaganda, kuuwa, kutesa, kupoteza na kuwasweka majela walinganizi mukhlisina kwa kisingizio cha sheria ya ubaguzi ya ‘kupambana na ugaidi’, na badala yake kuwatumia wakala wao waovu kwa ambao huusaliti Uislamu kwa thamani duni ya maisha ya dunia.
Ibada ya Ramadhaani ni ibada tukufu yenye hadhi kubwa ndani ya Uislamu, haimaliziki tu katika upande wa utawa na kualikwa vyakula vitamu na wanademokrasia. Jambo hilo ni kinyume na ibada yenyewe, na pia ni kinyume na taarikh yetu tangu zama za Mtume SAAW, masahaba ra na wema waliofuatia. Wao waliuchukulia mwezi huu kuwa ni kipindi adhimu cha kukithirisha amali zote za kheri kuanzia swaum, sala za sunnah, usomaji wa Quran, kutoa sadaka, kufanya ulinganizi wa Uislamu, kupigana jihad dhidi ya makafiri na hata kufungua miji.
Ramadhani ndio mwezi wenye fungamano na jambo kubwa la msingi wa ukombozi wa mwanadamu kwa kuanza ndani yake kushuka wahyi kwa Mtume SAAW. Kumbwa zaidi pia Ramadhani ikateuliwa na Allah SW kuwa ndio mwezi wa kushushwa muongozo wa Quran kutoka Bait-ul izzah mpaka kufikia wingu wa dunia. Kisha kushushwa kidogo kidogo kufuatia matukio na minasaba mbalimbali kwa muda wa miaka 23 kupitia Mtume SAAW ili kwa muongozo huo awaongoze wanadamu.
Waislamu tuna wajibu wa kuchukua hadhari kubwa na mbinu na hadaa za maadui wa Uislamu ambazo ni hatari kwa Uislamu wetu na fikra zake. Aidha, tudharau dhihaka za mfumo wa kibepari na wafuasi wake. Bali tuzidishe shauku yetu kwa mgeni huyu mtukufu (Ramadhani) na kuyakumbatia kwa mikono miwili yaliokuja nayo kuanzia thamani ya kinafsia na ya kisiasa. Na mwisho tukumbuke tuna jukumu kubwa la kulingania kwa jitihada kubwa ili kuleta mageuzi kwa msingi wa Uislamu, ili mwaka ujao mgeni huyu Insha Allah apokewe na mwenyeji wa kheri, yaani dola ya Kiislamu ya Khilafah ambaye ndie mlinzi wa matukufu yote ya Kiislamu na Waislamu.
Abdullah Juma
03 Ramadhan 1440 Hijri / 7 Mei 2019 Miladi
#RamadhanNaMuongozoWaQuran
Maoni hayajaruhusiwa.