Mazingatio Ya Kuachiwa Huru ‘Mdude Chadema’

بسم الله الرحمن الرحيم

Tunampongeza Said Nyagali (Mdude) kwa kushinda kesi na kuachiwa huru bila ya hatia. Mdude, kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, aliyetekwa mara mbili, kuteswa kukaribia kufa, akabambikiziwa kesi ya kusafirisha madawa ya kulevya ya heroin gramu 23.4 na kushikiliwa gerezani kwa mwaka na kidogo.
Hatimae leo Juni 28 Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya imemuachia huru ambapo Hakimu Mfawidhi, Zawadi Laizer amesema wazi upekuzi ulofanyika nyumbani kwa mshtakiwa ulikuwa batili na haukufuata sheria na kanuni za upekuzi. Yumkin katika upekuzi huo batil ndio alitegeshewa hayo madawa ya kulevya.
Hata hivyo, tukio hili litukumbushe mambo mawili makubwa:
Awali, dhihirisho la ziada la kuwepo kesi za dhulma na uonevu za kumbakizwa kama alivyowahi kusema Raisi Mama Samia Suluhu Hassan kwamba Takukuru walikuwa na kesi 147 za aina hiyo. Wahanga hubambikiziwa kesi kama hizo kwa misingi ya chuki za kisiasa, kidini au kutishiwa wasalimishe mali zao ili kununua uhuru wao nk.
Pili, lazima pia tukumbuke kwamba kando na Mwanachadema Mdude ambae kaachiwa huru leo, bado kuna mahabusu wengi mikoa mbalimbali, kwa mamia kama sio maelfu wenye hali mbaya zaidi magerezani kwa mgongo wa sheria ya kibaguzi, uonevu ya ugaidi.
Baadhi ya watuhumiwa hao waliwahi kutekwa awali, kuteswa, na baadhi wanaendelea kuteswa mpaka leo, wote wanaendelea kusota magerezani kwa miaka mingi kuliko hata Mdude, kiasi cha baadhi kufika miaka 4 na wengine zaidi. Na baya na kubwa zaidi kesi za watuhumiwa hao hazisikilizwi kwa kisingizio cha kutokamilika ushahidi kwa miaka mingi. Kinyume na kesi ya huyu Mdude ambae walau kesi yake imesikilizwa.
Kwa msingi huo, tunawaomba Waislamu na wapenda haki kwa jumla wasisite kupaza sauti kuwatetea na kuwapigania mahabusu wengine wengi katika mikoa mbali mbali kuanzia hapa Dar es Salaam, Arusha, Mtwara, Pwani, Tanga, Mwanza nk. ambao wanakabiliwa na hali mbaya sana ya uonevu na dhulma kuliko Mdude.
Lakini pia tunavitanabahisha vyombo vya kusimamia haki vijitakase mbele ya Umma, kwa kuwa kuachiwa huru Uamsho, kuachiwa huru Mdude nk. ni dalili ya wazi ya kuwepo utamaduni uliokita wa kupinda haki kwa dhamira ya uonevu na dhulma. Hivyo, ni wakati sasa kwa vyombo hivyo kuwaachia huru mahabusu wote au kuanza mara moja kusikiliza kesi zao na kujitenga na kisingizio cha uonevu cha kutokamilika ushahidi kwa miaka mingi.
Risala ya Wiki No. 104
17 Dhu al-Qi’dah 1442 Hijri / 28 June 2019 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.