Maangamizi Ya Gaza Ni Maangamizi Yetu Sote Umma Wa Kiislamu

بسم الله الرحمن الرحيم

Huu ni takriban mwaka wa pili tangu kijidola bandia cha Israel kilipoanza

mashambulizi ya kikatili yanayoambatana na mauaji ya halaiki ndani ya Gaza kufuatia

tukio la tarehe 7 Oktoba 2023.

 

Uvamizi wa kijidola cha mayahudi kwa agizo na nyenzo za kijeshi, kisiasa na kidiplomasia za Marekani na kuungwa mkono na nchi kadhaa za magharibi umeambatana na maangamizi yasiyo na mfano. Kuanzia mauaji makubwa ya halaiki kiasi cha kupotea roho za Waislamu 65,000 na majeruhi kwa maelfu, wengi wao wakiwa wanawake na watoto (kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Ukanda wa Gaza na vyombo vya habari vikubwa vya kimataifa). Ambapo vyanzo vingine vinaelezea hadi sasa zaidi ya watu laki mbili wameshauawa!

 

Aidha, uvamizi huo ambao umeshaangamiza takriban Gaza yote isipokuwa kijisehemu kidogo unachokimalizia kwa sasa, kando na kuvunjavunja takriban robo tatu ya majumba ya makaazi ya watu, umeleta uharibifu mkubwa sana kwa rasilmali watu na miundo mbinu mbalimbali. Kwa mfano, kuuwawa wanahabari zaidi ya 270, mpaka mwezi wa Agosti 2025 (Tv ya Al-Jazira), kuuwawa mamia ya walimu wakiwemo wa vyuo vikuu, kuuwawa wahudumu wa afya takriban 1400 (Relief web), kuvunjwa misikiti 79% (zaidi ya elfu moja), makanisa matatu ya Ukanda wa Gaza, kuuwawa wanavyuoni wa Kiislamu zaidi ya 255 na wengine wengi kuwekwa kizuizini nk. (Wizara ya Waqfu- Gaza), Hospitali takriban 36 za Ukanda wa Gaza, zinazofanya kazi ni chache sana, nyingi zimevunjwa kwa mabomu nk. Bila ya kusahau uvamizi endelevu wa Israel kwa Ukanda wa Magharibi ukiambatana na mauaji, kuvunja majumba, kuharibu mashamba, kuwatoa watu katika majumba yao, kamatakamata kiholela nk.

 

Ukatili wote huo wa kijidola cha Israel na mauaji ya halaiki unajiri ilhali Marekani kwa mara ya sita inapiga kura ya turufu (veto) kuzuiya usitishaji wa uvamizi huo na mauaji hayo ya halaiki. Bila ya kutaja vitisho vya Marekani kwa Mahkama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), kuitetea Israel licha ya Tume Huru ya Haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa na baadhi ya taasisi za haki za binadamu za ndani ya Israil kutamka wazi hadharani kwamba dola ya Israil inatenda  mauaji ya halaiki ndani ya Gaza.

 

Enyi Majeshi katika Ulimwengu wa Nchi kubwa za Kiislamu hususan jirani na Israel,

Munajua kwamba mna dhima mbele ya Mola wenu kuinusuru Gaza kwa kuwa mna nguvu mikononi mwenu? Jee mnajua kuwa nguvu mlizonazo ni amana kutoka kwa Mola wenu kwa ajili ya kunusuru Umma wenu na sio watawala vibaraka?  Bado mna shaka juu ya uovu na ukatili wa kijidola bandia cha Israel? Mnasubiri nini kuikomboa Gaza? Bado munasitasita na muna imani na kijidola hicho pamoja na yote kinchoendelea kuyatenda ikiwemo Waziri wao mkuu kutangaza wazi lengo lao la kuzipora ardhi zetu kukamilisha mradi wao kufanya ‘Israel kubwa’ (Great Israel Project)

Au bado mna tamaa kwamba kijidola bandia cha Israel kitaleta amani, ilhali mnaona mbele ya macho yenu kila siku kinafanya mashambulizi Syria, Yemen, Lebaon, na hivi karibuni Qatar nk. Kijidola hicho hakiheshimu mamlaka ya nchi yoyote kwa mujibu wa sheria zao za kimataifa wala mikataba. Patilizeni fursa ya dhahabu kuimaliza Israel na kumuonesha Allah ujanadume wenu, ambao sisi hatuna shaka nao, na nyinyi ndio tumaini la Umma wetu.

 

Enyi Wanazuoni vipenzi wa Kiislamu,

Nani atawahesabu, kuwakosoa na kuwanyoosha watawala vibaraka katika ulimwengu wa Kiislamu ambao idhilali yao katika kuunga mkono Israeil imeruka mipaka ya aibu. Ndio watawala hawa vibaraka ambao hutumia bandari zao, anga zao, rasilmali za Umma wa Kiislamu kukiwezesha kijidola cha Israel kuendelea kuiangamiza Gaza, halafu wakati huo huo eti wanaitaka Hamas iwaachie mateka na kusalimisha silaha zao. Ndio vibaraka hawa wanoaunga mkono sera ya hatari ya ‘dola mbili’ ambao ni mtego wa hatari wa kuipa Israil nguvu dhidi ya Umma wa Kiislamu. Mtego ambao baadhi ya nchi za magharibi kama Uingereza na Ufaransa wanajifanya kuunga mkono kama huruma kwa Waislamu wa Palestina, kumbe wanajificha nyuma yake, kwa kuwa tangu mwanzo wako bega kwa bega na Israil katika ukatili wake.

 

Pazeni sauti zenu Enyi Wanazuoni, tumieni mimbar zenu na majukwaa mengine kuwakosoa kwa ukali watawala vibaraka ambao wamefikia daraja duni hata kuliko watumwa. Jee hamuoni namna Qatar ilivyojipendekeza kwa Marekani kwa kumpatia Trump fedha na zawadi nyengine nono kisha Marekani inampa Israel silaha na ruhusa kuipiga nchi yake. Kuna aibu na fedheha kuliko hiyo? Trump na kijidola bandia cha Israil wanawachukulia watawala hawa ni vitimbakwiri duni kuliko hata paka.  Enyi Wanazuoni hata muda ukirefuka vipi msiwaache mkono wala msiwachoke Waislamu wa Gaza, kwa kuwa wao ni Umma wetu. Basi changamsheni majeshi na changamsheni Umma usimame imara wasimime wajibu wao, na msiwasahau Waislamu wa Gaza kwa uchache walau dua katika misikiti yenu.

Enyi Umma mtukufu wa Kiislamu,

Mnajua kuwa ukimya wenu ni hatari kwa qadhia kama hii na mfano wake. Lau mtasimama kidete kwa sauti zenu mtawalazimisha wanavyuoni na wanajeshi nao kusimamia qadhia za Umma wenu. Basi msiingie katika mtego wa shetani wa kunyamaza kimya.

Jee mnashindwa na makafiri wanapaza sauti zao kutetea Gaza kwa kusukumwa na ubinadamu tu, ilhali nyinyi mna imani na udugu wa Kiislamu. Sauti zenu ni wajibu ili kuwahimiza  wanavyuoni na wanajeshi wa nchi kubwa za Kiislamu kuchukua hatua.

 

Kwa kumalizia, yanayoendelea Gaza na madhila mengine katika ulimwengu wa Kiislamu ni matokeo ya Umma wetu kukosa dola ya Khilafah kulinda na kusimamia mambo ya Umma wetu ikiwemo kuhifadhi mali, heshima na damu zetu. Ni wajibu kujifunga na ufaradhi wa ulinganizi wa kurejesha tena dola yetu ambayo ndio kinga ya kweli ya kila chetu.

 

26 Septemba 2025 M / 03 Rabi’ al-thani 1447 H 

Maoni hayajaruhusiwa.