Maadhimisho ya “Siku ya Wazawa” ni Unafiki kwa Ubepari
Kila Agosti 9 ni Siku ya Kimataifa kuwaenzi wazawa duniani. Imechaguliwa kuwa ni siku ya kulinda , kuhifadhi na kukuza uwepo wa jamii hizo na kutambua mchango wao katika ustawi wa wanadamu. Siku hiyo ilichaguliwa rasmi na Baraza la Umoja wa Mataifa mnamo Disemba 1994.
Kwa hakika jambo hili ni unafiki wa hali ya juu kwa madola ya magharibi, kwani ukifuatilia kwa kina madola makubwa ya kibepari ambayo ndio hujipambanua kuweka wasimamizi na watetezi wa maadhimisho hayo katu hawathamini wazawa wala wanadamu kwa ujumla.
Na kwa udhati hoja ya ‘uzawa’ imekuwa inatumika kwa ajili ya kutetea maslahi fulani ya mabepari , na kama maslahi yakihatarishwa kwa mabepari basi fikra hii huwekwa pembeni.
Madola makubwa ya wamagharibi yamekuwa ndio wauaji, watesaji na wakandamizaji wakubwa wa wanadamu wakiwemo wazawa katika maeneo mbalimbali duniani.
Kuna mifano mingi kudhihirisha kwamba wamagharibi na mfumo wao wa kibepari hauwajali wazawa wa sehemu husika na wala hawana ubinadamu bali wao kipimo chao ni maslahi tu.
1. Marekani ya Kusini
Uvamizi huu ulifanywa na wareno na wahispania ndani ya karne ya 18. Wavamizi hao walitumia nguvu kuingia katika bara hilo na walilazimisha kupora ardhi kutoka kwa wazawa. Matokeo yake walitenda dhulma na mauaji ya mamilioni ya wazawa wa pale.
2. Marekani ya Kaskazini
Kama haitoshi Wahispania hao hao waliingia Amerika kaskazini baada ya Christopher Columbus kupelekwa pale na mabaharia wa kiyahudi, kupora ardhi na kuangamiza wazawa. Baada ya kipindi cha miaka 156 ya utawala wao waliuwa wazawa mamilioni ambao Columbus aliwaita “Wahindi wekundu”na jina hilo kubakia mpaka leo. Jamii hii ya Wahindi wekundu wamebakia wachache leo kwa sababu waliuwawa kwa wingi huko nyuma. Halikadhalika Ufaransa Iliingia Bara la hilo la Amerika kupitia California na wakatenda dhulma na ukatili kama Wahispania kwa kuangamiza wazawa. Inasadikiwa waliuwa wazawa milioni 20.
3. Afrika ya Kusini
Uvamizi wa Afrika ya Kusini ulitendwa na wajerumani na waholanzi kwenye karne ya 18, uvamizi huo ulileta majanga makubwa. Wavamizi hao walipofika pale walijibadilisha jina na kuamua kujiita makaburu/boers ambayo maana yake ni wakulima, ila wakulima hawa walipora ardhi kutoka kwa wazawa wa hapo na walichoma mashamba yao na kuuwa wazawa kwa mamilioni. Hatimae wavamizi hao waliasisi sera thaqili za ubaguzi wa rangi ambapo waliwagawa watu kwa misingi ya ubaguzi wa rangi. Na kwa upande wa Namibia wajerumani walitesa, kuuwa na kunyanyasa wazawa kiasi cha kudiriki kuingiza sumu kwenye visima vya maji na kuuwa watu wengi ambao ndio wazawa wa eneo lile.
4. Afrika ya Mashariki
Dunia haitosahau ukatili mkubwa uliofanywa na wajerumani pindi walipokwapua ardhi ya wazawa wa Afrika Mashariki hususan kwenye maeneo yaliyofahamika kama Tanganyika (Tanzania ya leo). Wajerumani waliuwa watu wasio na hatia zaidi ya elfu 20 kipindi walipokuwa wazawa walipopambana kutetea utu wao na rasilimali zao katika Vita ya Maji Maji. Wajerumani walipata upinzani mkubwa kutoka kwa Mujahidina waliokuwa maeneo ya Pwani na matokeo yake wakaua kwa hasira na kisasi raia wasiokuwa na hatia. Inaaminika pia Wajerumani waliingiza mbwa hadi misikitini kwa chuki, na yasemekana hii ndio sababu iliyomfanya Abushir bin Salim, mfanyabishara wa Bagamoyo kutangaza vita tukufu vya jihad dhidi ya utawala wa Wajerumani. Aidha, Wajerumani walidiriki kuweka sumu kwenye miti ya matunda kama mbinu mojawapo waliotumia kudhuru wazawa.
5. Biashara ya Utumwa kiujumla
Biashara ya utumwa ya pembe tatu (Triangular Slave Trade) ni jeraha jengine lilowadhuru wazawa kutokana na mikono ya nchi za kibepari za magharibi. Mabepari wa magharibi kwa msaada wa nchi zao walishughulishwa kwa kiwango kikubwa kwenye biashara hii chafu huku mufakirina/ wanafikra wao wakitawanya maandiko ya uwongo kuwa waarabu/Waislamu ndio waliokuwa wanafanya biashara hii.
Yakisiwa watu zaidi ya milioni 189 walichukuliwa toka Afrika kwenda kupelekwa kufanya kazi kwenye mashamba ya wazungu ndani ya Bara la Amerika. Zaidi ya asilimia 70 ya watu hao waliotekwa bila ya ridhaa yao walifariki kwenye safari wakiwa kwenye meli za watumwa.
Hali ya leo
Hiyo ilikuwa nyuma, je wamagharibi wamebadilika? Kiukweli hawajabadilika kwani tukiangalia mataifa ya kibepari hayajabadilisha kipimo chao cha matendo ambacho ni ‘maslahi’ ya kushikika tu na wala hayana ubinadamu hata kidogo. Tunaona takriban serikali zote za kibepari zinatoa msaada kwa serikali dhalimu ya Israel ambayo bado inaendelea kushikilia ardhi ya Al-Quds kimabavu na kuendelea kuwakandamiza na kuwauwa wazawa wa hapo bila ya kuchukua hatua yoyote ya maana. Aidha, bado serikali za kimagharibi zinaiachia serikali ya India kuendelea kulikalia kimabavu jimbo la Kashmir na bila ya kuchukua hatua yoyote ya kinguvu ya kutatua uvamizi huo.
Hitimisho
Suluhisho lipo kwenye Uislamu pekee, kwani tumeona kivitendo namna ambavyo utawala wa Kiislamu (Khilafah) ulipoifungua miji mbalimbali ulimwenguni kamwe haukuwadhulumu wenyeji wala kuwatenza nguvu kuwanyonya rasilimali zao, bali uliwaacha waishi salama usalimini ukiwatazama kwa jicho moja tu la uraia na sio dini, kabila wala rangi zao.
#UislamuNiMfumoMbadala
09 Agosti 2018
Kaema Juma
Maoni hayajaruhusiwa.