Kutumia Ushawishi Na Umaarufu Kwa ajili ya Uislam

 Allah SW. Ametutunuku neema namna kwa namna, lakini ni wale wenye kuzingatia tu ndio wanaogundua thamani ya neema hizo na kuzitumia kwa mujibu wa matakwa ya Allah Taala. Miongoni mwa neema hizo ni umaarufu, hali ya kuwa na ushawishi na sauti katika jamii yako, kiasi cha kuweza kuathiri kifikra na kimawazo wanajamii waliokuzunguka. Maswahaba (ra) walituonesha mifano hai jinsi walivyozitumia neema hizo za vipawa vya umaarufu kiasi cha kuwapelekea kufaulu kukubwa duniani na akhera na mpaka leo tarekh haijawasahau ingawa makafiri wamefanya juu chini kuondosha athari yao.

Kusilimu kwa masahaba  wakubwa Usaid bin Khudhwair na Sa’ad bin Mu’adh (ra) kuliwafanya wawili hao watumie neema ya ushawishi na sauti yao kwa watu wao kuwafikishia Uislamu na kuwasilimisha karibu watu wao wote, hadi  kupelekea kusiwe na nyumba hata moja ndani ya Madina ila kuna watu waliomkubali Mtume SAW na ujumbe wake.

Anasema Ibnu Is-haaq akionesha jinsi walivyosilimu Bani Abdul-Ash-hal  kutokana na ushawishi wa Saad bin Muadh, nanukuu: “ Pindi aliposimama Saad mbele ya Bani Abdul-Ash-hal  alisema:

Enyi Bani Abdul Ash-hal vipi munavyonielewa? Wakamjibu hakika wewe ni Chifu (kiongozi) wetu na mbora wa rai kwetu, akasema (Saad) nakwambieni kwangu mimi, mke na mume ni haramu hadi mumuamini Allah SW na Mtume wake. Wakasema, (watu wake) tunaapa kwa Allah SW hatopatikana katika koo yetu mwanamume au mwanamke isipokuwa amesilimu”

Mashujaa hawa ndio walioweka makubaliano na kumpa nguvu  Mtume SAAW kwa bai’a ya kwanza iliyofungwa katika msimu wa Hijja huko Minna mwaka wa 12 wa Utume na kwa kutumia ushawishi walionao kuifanya daawa ya Mtume SAAW kukubalika kwa haraka Madina kisha wakarudi tena Makka kutoa ‘bai’a ya pili’ katika siku za Tashriq mwaka wa 13 wa Utume, iliyopelekea kuasisiwa dola ya mwanzo ya Kiislamu.

Tukio jengine linalonesha jinsi maswahaba ra. walivyotumia ushawishi wao na kuleta mafanikio makubwa ambayo kila mmoja wetu anayatamani ni namna walivyotumia ushawishi wao kumkataa Abdallah bin Ubey bin Saluul na kumunga mkono Mtume na daawa yake, hali iliyomfanya Abdallah bin Ubay bin Saluul  hana namna ila abakie kuwa mnafiki, kwa kuwa hana wa kumuunga mkono.

Leo Waislamu wenye ushawishi, kauli na umarufu wa kila aina kuanzia siasa, michezo, biashara, koo, elimu, utangazaji, cheo na mfano wake wajifunze kwa masahaba waliotangulia kwa  kutumia nafasi hizo ambazo ni neema ya Allah Taala na mtihani kwao kwa ajili ya Uislamu hususan kwa ulinganizi wa kuleta mabadiliko ya kweli yatakayokomboa Waislamu na wanadamu kwa jumla.

Amesema Allah Ta’ala katika Surat at-Attakathur

ثُمَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ “

‘Kisha mutaulizwa kutokana na neema ( mulizopewa)

(102:8)

#UislamNiHadharaMbadala

 

Afisi ya Habari –  

Hizb ut- Tahrir Tanzania

14 Dhul Hijjah 1439 Hijri 1439 Hijri    | 25-08- 2018 Miladi

https://hizb.or.tz/

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.