Kurtadi Msanii Hajji Adam Na Kuasisi Kanisa Lake: Mwendelezo Wa Upagazi Wa Fikra Dhidi Ya Uislamu

بسم الله الرحمن الرحيم

Karibuni msanii wa filamu Tanzania au bongo movie aliyekuwa Muislamu kwa jina Haji Adam ametangaza rasmi katika Redio ya Times FM. kuwa ameshauwacha Uislamu na ana nia ya kuanzisha kanisa lake ambalo watoa sadaka ndogo na sadaka kubwa wote watapewa hadhi sawa.
Lazima iwe wazi kuwa kazi zinazoitwa kazi za usanii sio chochote zaidi ya kuwa jukwaa la kueneza ufuska,uovu, kuharibu vijana wa Kiislamu, bali vijana jumla. Lakini Waislamu ndio walengwa zaidi kwa kuwa wao wana muongozo.
Kwa msingi huo, usanii ni medani ya wazi ya kupambana dhidi ya Uislamu.
Quran Taukufu Inasema:
وَإِن يَكَادُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَيُزْلِقُونَكَ بِأَبْصَارِهِمْ لَمَّا سَمِعُوا الذِّكْرَ وَيَقُولُونَ إِنَّهُ لَمَجْنُونٌ
“Na waliokufuru hukaribia kukutelezesha kwa macho yao, wanaposikia mawaidha, na wanasema: Hakika yeye ni mwendawazimu”
(Surat Al-Qalam: 51)
Aya hii inatupa ishara kwamba mipango na mikakati ya makafiri kuwatelezesha Waislamu kuwatoa
katika imani yao ni jambo endelevu.
Mtume SAAW katika Hadithi ndefu anasema:
ثبت عنه ﷺ في حديث طويل: يصبح الرجل مؤمنًا ويمسي كافرًا، ويمسي الرجل مؤمنًا ويصبح كافرًا، يبيع دينه بعرض من الدنيا قليل
“(Zitakuja zama) Ataambaukiwa mtu asubuhi akiwa Muislamu na atatuliwa na jua (ataingiliwa na
jioni) akiwa kafiri. Pia ataingiliwa na jioni mtu akiwa Muislamu, na atapambaukiwa akiwa kafiri.
Atauza mtu dini yake kwa thamani duni ya kidunia”
Leo hii dunia inashuhudia kuibuka kwa makundi mengi hususan ya vijana wanaopinga na kutukana
dini kwa matusi ya mitindo mbalimbali.
Kwa mfano:
a. Hufanya maigizo ya vichekesho (comedy) mbalimbali yenye maudhui ya kukejeli na kukebehi dini.
b. Hubuni maswali yenye kuwatia shaka shaka wafuasi wa dini na uwepo wa Muumba.
c. Hujaribu kukosoa vitabu vya dini ilhali wao si wajuzi wa elimu ya dini
d. Hutangaza hadharani, tena kwa kujifakhiri kuachana na dini na kudai dini ni utumwa
e. Hutukana dini kwa kila aina ya matusi katika majukwaa mbali mbali, kila wakipata fursa.
Baadhi ya mbinu zao:
• Kutangaza imani za kiajabuajabu kama vile alivyofanya Afande Sele kwa kudai jua ndio Mungu wake.
• Kuikosa adabu dhati ya Mungu kama alivyohubiri Harmonize kwamba Mungu ni mwanamke.
• Kumlazimisha Mungu matakwa ya kijinga, kama kauli ya kijahili ya msanii Nay wa Mitego kwamba ukimuomba Mungu asipokujibu, huyo sio Mungu, tafuta Mungu mwingine.
• Wengine kuacha Uislamu kimya kimya kama Roma mkatoliki, Rose Muhando nk.
• Kuimarisha mavuguvugu ya harakati za kimataifa za ‘dini mseto’ kama alivyowahi kutangaza kijana Mchungaji Godlove (mkristo), kwamba makanisa yao hayachagui wafuasi wa dini. Au kama anavyohubiri kijana huyu Haji Adam ambaye asili ni Muislamu nk.
• Kuibuka wimbi la kampeni ya dini za kiafrika za kuabudu mizimu na kuachana na dini wanazoita zimekuja kwa majahazi. Ilhali wafuasi hao hao wa dini za mizimu wanaunga mkono na wako kifua mbele na fikra za kimagharibi na mfumo wake thaqili wa kibepari zilizokuja kwa ndege, wala hawana pingamizi juu ya hilo.
• Kuanzishwa majukwaa ya mijadala inayoitwa ya mijadala ya fikra huru yenye malengo ya kutukana dini kama wafanyavyo baadhi ya vijana mitandaoni kwa jina la ‘wachokonozi’ wanaotukana dini zote kwa hoja ya mijadala ya kielimu na fikra huru lakini malengo makuu ni Uislamu
Kampeni hizi zipo dunia nzima si hapa Tanzania tu, na kuna makundi mengi sana katika mitandao kwa jamii na lugha zote. Zinazoitwa hoja za makundi hayo yote zinafanana ikiwa ni ishara kwamba wapo chini ya kundi moja, usimamizi mmoja, mfadhili moja na malengo mamoja ya kufanana.
Kuibuka kwa magenge hayo ni moja ya mbinu za mabepari wakoloni, na baadhi ya sababu ni hizi:
Kwanza, dunia inashuhudia kupitia katika kipindi kibaya sana cha mchafukoge wa maisha jumla katika siasa, uchumi, jamii, sheria nk. Kwa ufupi, kunadhihirika wazi wazi kufeli mfumo wa kibepari. Na tayari kuna vuguvugu kubwa la kutaka mabadiliko na chanzo cha tatizo kimeshajuulikana ambacho ni mfumo katili wa kibepari, huku kampeni za kupinga ubepari zimepamba moto kila mahali. Kwa hivyo, kuibua makundi hayo na kampeni hiyo ni kama kuwashughulisha na kuwaondoa watu katika reli. Kama inavyotumika michezo na zinazoitwa burudani mbali mbali kufikia malenngo hayo.
Pili, mabepari wanajua hakuna mfumo mbadala zaidi ya Uislamu. Hivyo, ujanja wao wa kuendesha kampeni za kutukana dini zote ni danganya toto na kujificha gongo wazi kwa kuwa malengo yao makuu ni Uislamu na vijana wa Kiislamu.
Tatu, kuibuka kwa mfumo wa kibepari kulitokana na kupindua kanisa kutoka katika utawala. Hivyo, ni kweli kabisa asili mfumo huo una chuki kali na uadui juu ya dhana nzima ya dini. Lakini kampeni yao leo hawapambani tena na kanisa, kwa kuwa mabepari wameshafanikiwa kitambo kulifanya kanisa na kuligeuza kuwa moja ya matawi yake matiifu kukuza ubepari na fikra zake chafu ikiwemo ushoga. Hali hiyo hawajafanikiwa na hawatofanikiwa kwa Uislamu. Kwa hivyo, iwe wazi kuwa katika mchakato wa mapambano haya mlengwa mkuu ni Uislamu na sio ukiristo wala vijidini vyengine kama ubudha, uhindu, uyahudi nk. Kwa kuwa hivyo, tayari viko mifukoni mwa mabepari kitambo.
Tahadhari kubwa kwa Umma wetu
Wakati tukimnasihi Hajji Adam kwa ikhlasi kurudi katika Uislamu na kutubu kwa Mola wake, tunapenda kuwaeleza masheikh, maduaat, maustadh na Waislamu jumla lazima wajue kwa kina kwamba kuna kampeni kubwa ya kidunia ya kuwaritadisha Waislamu kwa kupitia watu maarufu kama wasanii, watangazaji, wanasiasa, wanamichezo nk. Na nchi za Arabuni kuna bomu kubwa la kuritadi Waislamu linalosubiriwa kuripuka hususan nchini Saudia ambapo kuna maelfu ya vijana waliokumbwa na kampeni ya kuratidishwa inayoratibiwa na watawala Ibn Saud.
Kwa kampeni hiyo wameshatekwa akili vijana hao ambao wanasubiri muda muwafaka tu kujidhihirisha hadharani zaidi kurtadi kwao ( japo tayari baadhi wameshaanza kujitangaza). Hao ndio kundi linalomuunga mkono mtawala muovu anayevuruga Uislamu mwana mfalme wa Saudia,Muhammad Ibn Salman
Pia masheikh na maustadh wajue kwamba tuna changamoto na mapungufu ya kutowajenga Waislamu kuufahamu Uislamu kimfumo na kuitetea aqida yake kiakili. Anayofanya msanii Haji
Adam na wenzake inawezekana ni natija ya jambo hilo. Lazima Umma ujengwe kuubeba Uislamu kwa hoja za kiakili na kuweza kuutetea na sio kujengwa kuwa ni dini kiurithi au kimila.
Mwisho kwa kumalizia, masheikh, maustadh na Waislamu jumla lazima waelewe kuwa kukosekana chombo (dola ya Kiislamu ya Khilafah) cha kuhifadhi aqida ya Uislamu kumepelekea Uislamu kudharauliwa na kukebehiwa kila mahala na kila siku. Aidha Uislamu unachukuliwa kuwa ni ‘dini poa’ yaani unayoweza kuingia na kutoka kama chumbani kwako.
Pia kwa kuwa hakuna wa chombo cha kutia adaabu waliortadi na wanaokebehi Uislamu, sio tu baadhi wanartadi, bali wanajifakhiri kwa kurtadi kwao. Kwa hivyo, lazima tushiriki katika mchakato wa uwajibu wa ulinganizi kuirejesha tena dola ya Kiislamu ya Khilafah ili ije ilinde aqida ya Kiislamu na kuwatia adabu wote wanaoikosea adabu.
Risala ya Wiki No. 191
04 Rabi’ al-awwal 1446 Hijri | 06 Septemba 2024 Miladi
Afisi Ya Habari – Hizb Ut Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.