Kupaa Bei Ya Mafuta Tanzania: Chanzo Mfumo Wa Ubepari
بسم الله الرحمن الرحيم
Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Kupanda kwa bei karibuni kwa nishati ya mafuta nchini Tanzania kumeleta ziada ya hali ngumu na mbaya ya kiuchumi ukisukuma mfumuko wa bei kwa kiwango cha 3.8 (ndani ya Aprili2022) katika kila bidhaa ikiwemo kupanda kwa nauli za dala dala na katika majiji, pia kwa usafiri wa mabasi ya masafa marefu, kupaa huko bei za bidhaa muhimu kumepelekea kupanda kwa gharama ya maisha na ugumu wa kiuchumi hususan miongoni mwa wananchi walio wengi ambao ni masikini.
Serikali inaihusisha hali hii na vita vya Urusi na Ukraine ambavyo vimetikisa uchumi wa kilimwengu kutokana na kupanda kwa bei ya nishati ya mafuta, na hivyo pia kuathiri Tanzania. Raisi Samia Suluhu Hassan alisema kati kati ya mwezi Machi 2022.
“Hili sio suala la viongozi. Ni hali ya kilimwengu….. bidhaa zote zitapanda bei, nauli zote zitapanda, kila kitu kitapanda bei juu.”
Suala la uagizaji wa bidhaa za mafuta ya petroli Tanzania chini ya mfumo wa uagizaji wake kwa wingi uliopo tangu mwaka 2011, unaelekeza kuwa uagizaji wa bidhaa za nishati ya mafuta ya petroli ufanywe kwa kupewa fursa waagizaji wachache walioteuliwa.
Zaidi ya hayo, serikali imeweka kodi nyingi katika mchakato wa uagizaji wa petroli kama Tsh 920 kwa lita ya petrol, Tsh 800.13 kwa lita ya diesel and Tsh 745.77 kwa lita ya mafuta ya taa. Kodi na tozo hizo zikihusisha upakuzi bandarini, ushuru, Mamlaka ya Kusimami Uzito na Vipimo (WMA), Mamlaka ya Viwango (TBS) , Mamlaka ya Bandari (TASAC), Mamlaka ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mamlaka ya Barabara Vijijini (TARURA) nk.
Mnamo tarehe 10/05/2022 serikali imethibitisha kutoa ruzuku ya Tsh 100 billioni kama hatua ya kuokoa hali, hatua ambayo kiudhati haitoweza kubadilisha hali, kwa kuwa ruzuku ya Tsh 102 billioni mwaka jana ilipelekea kupungua kidogo sana kwa bei za 29.38 kwa petroli kwa lita, sh 30.05 kwa lita ya diseli na 26.99 kwa lita ya mafuta ya taa katika lita bilioni 3.8 za ptroli, diseli na mafuta ya taa zilizotumika Tanzania katika mwaka 2021.
Kwa hivyo, jambo hilo halikuweza kusaidia sana ndani ya mwaka uliopita, ni wazi halitoweza pia kusaidia katika mwaka huu. Na katika mustakbal tatizo litaendelea kujiri tena na tena kutokana na sababu zifuatazo:
a. Sera ya kiuchumi wa kibepari inayobinafsisha bidhaa za nishati ya mafuta:
Ubepari uko tofauti kabisa na Uislamu, unaruhusu nishati ya mafuta na uchimbaji wake kuwa mali ya kibinafsi inayoweza kumilikiwa na watu binafsi, taasisi na kampuni binafsi. Matokeo yake sera hii ya kidhalimu ya uchumi wa kibepari na makampuni yao makubwa ya kimataifa inawanyima Umma mali yao na kuipeleka katika mikono ya wachache kwa kisingizio cha ubinafsishaji na uwekezaji, huku ukiuwacha ulimwengu na watu jumla katika mashaka kutokana na umaskini pamoja na ukweli wa kuwepo utajiri huo mwingi wa nishati kwa ajili ya Umma mzima.
b. Qadhia ya kuhodhi kwa sarafu ya Dolari ya Marekani:
Mfumo wa kiuchumi wa kilimwengu umejengwa juu ya dhulma katika kuendesha biashara ya kimataifa kwa kuufungamanishwa na sarafu ya nchi moja (dolari ya kimarekani) ambayo huondoa kabisa mamlaka za nchi kufanya maamuzi yao. Ulimwengu hususan nchi zinazoendelea zinakabiliwa na hali tete ya kiuchumi na majanga leo kama mfumuko wa bei kutokana na kukabwa na minyororo ya sarafu ya dolari ya kimarekani.
c. Kuwepo urasimu wa kupewa fursa wachache katika kuagiza bidhaa za petroli:
Hali hii inatoa fursa kwa makampuni ya kibepari kuwa na ubwana katika biashara yote (ya nishati ya mafuta), kuhamasisha uwepo wa rushwa katika idara za serikali na kupelekea makampuni yanayoagiza (mafuta) kwa na udhibiti kamili wa sekta hiyo, hali inayopelekea kukosekana kwa bidhaa hiyo (kijanja) mara kadhaa.
d. Uwepo wa kodi na tozo nyingi za serikali kama vyanzo vya mapato:
Pamoja na ukweli wa mataifa yanayoendelea kuwa na utajiri mkubwa ikiwemo maliasili na maadini, mathalan Tanzania inakisiwa kuwa mrundiko mkubwa wa dhahabu wa ounce 45 milioni (1,275 tonnes), ikiwa ni nchi ya tatu kwa wingi wa dhahabu katika Afrika baada ya Afrika ya Kusini na Ghana, lakini kutokana na kukosekana kwa mfumo wenye nuru (Uislamu) na uwepo kwa unyonyaji wa kibepari wa madola ya kimagharibi mataifa hayo yanashindwa kufaidika vyema na rasilmali hizo, kiasi cha kuona suluhisho pekee la serikali kupata mapato ni kwa kila uchao kuasisi kodi mpya ambazo hupelekea mashaka juu ya mashaka kwa wananchi ambao wengi wao ni wanyonge.
Changamoto zote hizo tulizotaja (juu) zinasababishwa na kitu kimoja tu, nacho ni mfumo wa kibepari. Mfumo unaotenza nguvu nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania na kuwafanya watu wa (madola hayo yanayoendelea) kuwa katika hali ya kutapatapa kutokana na minyonyoro thaqili ya uchumi wa kimagharibi.
Ni wazi kwamba ubinadamu unahitaji mfumo wa uadilifu na insafu ambao ni Uislamu, kwa kupitia dola yake ya Khilafah itaukomboa kikamilifu kutokana na uovu, ukatili na unyonyaji wa kiuchumi na kuupeleka katika mafanikio na saada ya kweli katika maisha ya dunia hii na maisha yajayo ya akhera.
Masoud Msellem
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari
Hizb ut Tahrir Tanzania
KUMB : 1443/05 – Jumanne, 24 Shawwal 1443 H / 24/05/2022 M
Maoni hayajaruhusiwa.