Kukamilika na Kutimia Ramadhani

بسم الله الرحمن الرحيم

Mazingatio ya Ramadhani – 3

Quran ilipotuwajibisha kufunga Ramadhani imegusia juu ya mambo mawili makubwa:
Jambo la kwanza, kukamilisha idadi ya siku za kufunga:
وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ ……
“basi atimize hisabu”
Hapa tunasisitizwa kutimiza idadi kama inavyotakikana na sharia ya Swaumu ya Ramadhani.
Jambo la pili Quran imetuwajibisha pia tuitimize saumu :
ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ
“Kisha timizeni Saumu mpaka usiku”.
Tamko kukamilisha (kamala) hapa ni kwa upande wa idadi ya (quantitiy) ya siku. Na tamko tamma ni kutimia kitu kwa kiwango thabiti kilichokusudiwa cha kitu husika (quality), ikihusisha kila sifa iliyomo ndani ya kitu chenyewe.

Kwa mfano, ukisema timu ya mpira imekamilika. Ina maana idadi ya wachezaji wa timu hiyo iko sawa. Si lazima wawe wachezaji hao ni mahodari, mahiri na wenye kiwango katika uchezaji wao. Lakini utakaposema timu imetimia, ina maana idadi iko sawa, lakini pia wachezaji hao wamesheheni kila aina ya sifa ya uweledi katika fani ya uchezaji mpira.

Allah Taala katika muktadha wa Swaumu kataja mambo yote mawili yapatikane ili Saumu iwe yenye kuleta uchamungu kikweli. Na hii ni dalili kuwa Quran ni maneno ya Allah Taala, kiasi kwamba kuna uangalifu wa hali ya juu katika kuteua maneno ili kufikisha ujumbe uliokusudiwa.

Leo Swaumu zetu zinakamilisha idadi ya siku, lakini zina mapungufu katika kutimiza kiwango cha udhati wa Swaumu yenyewe. Hatusemi kuwa tusifunge hashalilah! lakini haya lazima tuyatafakari kwa kina.
Kwa kukosekana mtawala wa Kiislamu (Khalifah) Swaumu zetu zinapita katika mitihani migumu katika kila hali. Tunafunga ilhali tumezunguukwa na mazingara machafu kuanzia watu kutembea uchi, kula mchana, kubanwa kiuchumi nk. Leo tunahitaji tuwe na mtawala ili kuja kuwafunga minyororo mashetani wa kibinadamu ambao hulazimu wafungwe na wanadamu wenzao. Baada ya kufungwa minyororo mashetani wa kijini.

Jee nani atadhamini mazingira rasmi ya Kiislamu kuihifadhi Swaumu ya Ramadhani?
Yote haya majibu yake ni uwajibu wa Waislamu sote kufanya kazi ya kurejesha tena dola ya Kiislamu ya Khilafah ili ije kuisimamia Ramadhani na ibada nyengine zote zifikie kilele cha ukamilifu na utimilifu.

Masoud Msellem
04 Ramadhan 1440 Hijri / 9 Mei 2019
#RamadhanNaMuongozoWaQuran

Maoni hayajaruhusiwa.