Kuingia Mwaka Mpya ni Fitra Inayodhulumiwa
Allah Taala kwa Rehma Zake licha ya kuleta Mitume As. kuwaongoza wanadamu namna ya kumuabudu Mola wao na kuwapa sharia kutoka Kwake ili watu kusimamia maisha yao, pia Akawabakishia ndani ya maumbile ya nafsi zao utambuzi wa kimaumbile ambao huwawezesha kutanabahi na kujua kuwepo kwa Muumba huyo.
Utambuzi huo ndio huitwa fitra. Maana ya fitra ni ile hisia ya utambuzi wa ndani isiyopingika kwenye nafsi ya mwanadamu kuhisi kusiko na shaka kuwepo anayemtenza nguvu mwanadamu bila ya ridhaa yake. Mwenye nguvu huyo hutenda Ayatakayo kwa mwanadamu bila ya mwanadamu kuweza kudhibiti maaumuzi hayo. Huyo ndio Mola, Muumba wa mwanadamu na kila kilichomzunguka. Hisia hii ya kuwepo Muumba huyo anayo kila mwanadamu akipenda asipende. Kilichobakia ni kwa mwanadamu kukiri hadharani utambuzi wa Mola huyo na kujisalimisha, au kujisahaulisha mpaka arudi kwa Mola wake kustahiki adhabu.
Ukiangalia kwa makini maisha yote ya mwanadamu tangu kuzaliwa kwake, kuishi kwake duniani na kumalizika umri wake kwa kufariki ni miongoni mwa mambo ambayo kwa kila mwenye fikra iliyosalimika bila ya chuki, taasub wala kasumba humpelekea kwenye utambuzi wa kuwepo Mola wake yaani fitra. Mwanadamu hakujuwa lini atakuja duniani. Aidha, hajui ataondoka lini. Pia kuondoka kwa walioondoka kabla si kutokana na uzembe. Kwa sababu kama sababu ya kufariki kwa waliotangulia ni uzembe, wapo wazembe wengi ambao bado wanaendelea kuishi. Na lau kama sababu ya wanaoishi duniani leo ni kwa kuwa mahodari, wajanja au kuwa na afya njema, basi walikuwepo mahodari wengi, wajanja na waliokuwa na afya njema lakini leo hawapo wameshafariki. Hili kwa ufupi ni dhihirisho la kuwa mwanadamu hana khiyari katika kuwa na umri mrefu au mfupi, na wala hana athari katika kuendelea kuishi katika maisha haya au kufariki.
Kwa msingi huo, kuingia kwa mwaka mpya, uwe wa kalenda ya Kiislamu au nyengineyo kinachodhihirika ni kusonga mbele kwa umri wa mwanadamu, kuongezeka maisha yake na pia kurefuka muda wa waliotutangulia makaburini. Jambo hilo kamwe mwanadamu hawezi kabisa kuliingilia wala kujipangia kwa namna yoyote. Kwa hivyo, kwa kuingia mwaka mpya na kwa kuwa mwanadamu hawezi kuliingilia suala hilo, ilitarajiwa mwanadamu atanabahi kwa utambuzi wa kuwepo Muumba wake na kujinyenyekeza kwake na sio kufanya vitendo vya fujo, vurumai na ufuska kwa kisingizio cha ati sherehe za mwaka mpya.
Katika mfumo wa kidemokrasia jambo hili ni lenye kutarajiwa. Kwa kuwa ni mfumo wa fujo na ujanja wa kukimbilia kwenye matawi/mitagaa badala ya chanzo. Ilikuwa mfumo huu umuoneshe mwanadamu ikiwa umri wake umeongezeka, jee amechangia chochote katika kuongezeka huko? Na kwa kuwa hana mchango katika hilo hana budi amkiri Muumba ambae ndie Mpangaji wa hayo na mengineyo. Na kilichobakia ni kumnyenyeke Yeye peke yake. Hii ndilo suala la msingi ambalo hupaswa kulikabili kila mweledi na mwenye fikra angafu.
Uislamu umeuita umri wa uzee ulioambatana na udhaifu wa kutoelewa mambo kuwa ni umri mbaya. Kwa sababu katika umri huo mwanadamu anashindwa hata kutambua katika yale aliyokuwa akiyatambua awali. Hii maana yake hata kama umri wa mwanadamu utakuwa ni miaka kumi na tano, lakini akashindwa kuwa na utambuzi thabiti wa mambo, umri huo pia nao ni katika umri mbaya.
Kuingia mwaka mpya chini ya mfumo wa kidemokrasia ni kuzama katika umri mbaya kwa sababu kunamkosesha mwanadamu ufahamu thabiti wa kumfungamanisha na Mola wake aliyemuumba.
#UislamuNiHadharaMbadala
Na Masoud Msellem
Maoni hayajaruhusiwa.