Kufinyanga Familia ya Kiislamu Kuwa Mbali na Umagharibi

بسم الله الرحمن الرحيم

Watoto wetu wa Kiislamu ni sehemu ya jamii kama tulivyo sisi. Wanakulia na kuishi katika jamii zetu ambazo majukumu ya kijinsia yanazidi kuwa na mkanganyiko. Katika hali kama hii ni wajibu wetu kama wazazi wa Kiislamu na sehemu ya Umma kukabiliana na mkanganyiko huu tangu hatua ya awali.
Mfumo wa elimu haungoji hadi watoto wetu wakomae ili kuwafunulia mada kama hizo, bali huwafunulia mapema iwezekanavyo. Muhimu kwetu ni kuhakikisha watoto wetu wanaelewa mtazamo wa Kiislamu juu ya majukumu ya kijinsia na haki za wanawake kwa mujibu wa Imani yetu. Kwa kuwa watoto wadogo hujifunza zaidi kupitia kuwaangalia wazazi wao, ni lazima tuhakikishe tunaelewa kwa uwazi jinsi Allah (SWT) anavyofafanua majukumu na wajibu wetu kama Waislamu.
Miongoni mwa mambo muhimu ya kuwajenga watoto wetu ni pamoja na kuwaelimisha watoto wetu kwamba Allah (SWT) Ameumba jinsia mbili tu, yaani mwanamume na mwanamke, na katu hazifanani jinsia hizi. Anasema Allah (SWT) katika Quran:
وَلَيْسَ الذَّكَرُ كَالأُنْثَى.
“Na mwanamume si kama mwanamke”[TMQ: Ali’Imran:36]
Licha ya utofauti huu wa kijinsia na kiasili, Allah (SWT) amewafanya wanaume na wanawake kuwa sawa kwa baadhi ya mambo. Kwa mfano, wanaume na wanawake wote ni wanadamu, wote ni waja wa Allah (SWT), na wote wawili wana wajibu wa kumuabudu Allah (SWT) pekee. Anasema Allah (SWT):
وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنْ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلاَةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللَّهَ وَرَسُولَهُ أُوْلَئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللَّهُ إِنَّ اللَّهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ (التوبة: 71).
“Waumini wanaume na Waumini wanawake ni marafiki wao kwa wao. Wanaamrisha mema na kukataza maovu na wanasimamisha Sala na wanatoa zaka na wanamtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao – Mwenyezi Mungu atawarehemu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.” [TMQ: At-Tawba:71]
Suala jingine muhimu la kuwafahamisha watoto wetu ni kuhusu utofauti wa majukumu, kwamba wanaume na wanawake wana majukumu tofauti. Katika hili hulazimu kuwafundisha watoto wetu kwamba Allah (SWT) aliyetuumba anatujua zaidi, na hivyo amewapa wanaume majukumu tofauti na wanawake kutokana na elimu yake akiwa Yeye Allah Taala ndio Muumba wa viumbe hao.
Hii maana yake tuwajuze watoto wetu kwamba majukumu haya tuliyowekewa na Muumba yapo ili kutusaidia, wala si kutuwekea vikwazo. Kwa mfano kama Allah (SWT) alivyompa jukumu la usimamizi mwanamume kwa mke wake. Allah (SWT) anasema :
الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ ب
“Wanaume ni wasimamizi wa wanawake…’
” [TMQ: Surah An-Nisa:34].
Kwahiyo, jukumu la baba ni usimamizi na kuhudumia familia yake. Hili haliondoshi ulazima wa baba kumtendea mema na kumheshimu mke wake, kumuoneshe heshima, kwani mkewe ndiye moyo wa nyumba yao, mlezi na mwalimu wa muda mwingi kwa watoto wao, ambaye atawalea kuwa Waislamu waadilifu.
Zaidi ya hayo, lazima baba na mama waweke mkazo juu ya sifa na mtazamo huu kwa watoto wao. Yaani wawafundishe watoto wa kiume wajibu wao katika Uislamu kama wanaume, vivo hivyo kuwafundisha Watoto wa kike majukumu yao kama watoto wa kike.
Kwa upande wa kinamama ni lazima kwao kuwaonesha heshima waume zao, kuwasikiliza, kuwatii na kutunza nyumba yake na watoto wake. Mama anapaswa kubeba maadili haya kwa mabinti zake na kuwafundisha haki zao walizopewa na Uislamu, na pia haki juu yao zilizoamrishwa na Uislamu.
Kwahiyo, wazazi wa Kiislamu wanatakiwa kujua kuwa watoto wao wanahitaji kuandaliwa kuwa na muamko wa yale ambayo Muumba wao amewaamuru wayatekeleze kama wazazi wao.
Aidha, ni lazima kuwapa maarifa haya watoto ili kukabiliana na propaganda ya Ufeminia uanolingania haki na usawa baina ya wanawake na wanaume kwa mujibu wa usekula wa kibepari.
Watoto wa kike lazima wajue jinsi walivyo muhimu kama wanawake wa Kiislamu na jinsi yatakavyokuwa majukumu yao muhimu kama wake na mama. Pia, watoto wa kiume wabebe majukumu kama wanaume katika Uislamu, nao wakijua kwamba ni makaka na siku moja watakua mababa.
Kwa kumalizia ni muhimu zaidi kuwafundisha watoto wetu wa kike na kiume jinsi ya kuishi maisha sahihi ya Kiislamu ili kila mmoja abakie katika haki na majukumu yake bila ya kuhisi kuna ubaguzi au upendeleo.
Risala ya Wiki No. 210
1 Muharram 1447 Hijri / 26 Juni 2025 Miladi
Imeandikwa na Ust. Ally Kamsokole

Maoni hayajaruhusiwa.