Kuangazia Suala La Kutekwa Na Kutoweka Watu Tanzania

بسم الله الرحمن الرحيم

Habari:
Mnamo tarehe 09 Agosti, 2024, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu utekaji na upotevu wa watu unaoendelea kuripotiwa katika maeneo tofauti hapa nchini. Taasisi hiyo iliorodhesha takriban watu 83walioripotiwa kutekwa na kutoweka tangu mwaka 2016.
Maoni:
Tunalani vikali vitendo hivyo ambavyo vimekua vikiongezeka katika kipindi cha hivi karibuni bila vyombo husika vya serikali kuwajibika ipasavyo.
TLS iliripoti zaidi ya matukio 20 za utekaji/kutoweka mwaka 2024 pekee. Watu waliotekwa/kutoweka ni pamoja na wakosoaji wa serikali, wanasiasa, wafanyabiashara, watu wa kawaida wakiwemo watoto wa kawaida na wenye ualbino.
Taarifa za kutekwa/kutoweka kwa watoto zimeripotiwa zaidi katika siku za hivi karibuni na hivyo kuzua hofu miongoni mwa wazazi, kwani wengi wao ni wanafunzi.
Inaaminika kwamba kuna sababu kadhaa za kutekwa na kupotea kwa watu zikiwemo imani za kishirikina zinazochochewa zaidi na ajenda za kisiasa zinazohusiana na uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu 2024 na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025.
Itakumbukwa kwamba mwaka 2015 Bw. Zeid Ra’ad Al Hussein, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, alionya kwamba kuongezeka kwa mauaji ya albino nchini Tanzania kunaweza kuwa na uhusiano na kampeni za Uchaguzi Mkuu zilizokuwa zinaendelea mwaka huo
Inasemekana kuwa baadhi ya wanasiasa wanaamini kuwa kupata baadhi ya viungo vya mwili wa albino kwa ajili ya ushirikina kunaweza kuwafanya washinde katika uchaguzi.
Ukosoaji wa serikali, biashara ya binadamu, biashara ya viungo vya binadamu, uhuni, uasherati na ubakaji pia zinaweza kuwa sababu za kutekwa na kutoweka kwa watu.
Matukio haya ya kikatili yanafedhehi ukweli kwamba serikali za kidemokrasia za kibepari hazijali ustawi wa watu jumla, ikiwa pamoja na masuala nyeti kama vile usalama wa watu. Ni aibu kwamba, licha ya kujirudiarudia kwa matukio haya kila mwaka au ndani ya miezi kadhaa, bado haijafanywa jitihada za kutosha kupambana na kuzuia matukio haya.
Zaidi ya hayo, inaashiria kwa uwazi ubaya wa mfumo wa mfumo wa ubepari, miongoni mwa fikra za mfumo huo ni fikra ya ‘manufaa ya kibinafsi’ ambayo yamewafanya watu wawe na uroho na pupa kujali maslahi yao kibinafsi tu na faida ya kimada bila kujali ya madhara ya yanayoweza kuletwa kwa watu wengine.
Wakati tukiitaka serikali kama msimamizi wa umma kuingilia kati kwa njia zote zinazowezekana ili kukomesha vitendo hivi vya kinyama, ni muhimu ieleweke wazi kwamba ni chini ya dola ya Kiislamu tu (Khilafah) ndipo ambapo usalama wa kweli wa watu utapatikana kupitia utekelezaji wa sheria za Mwenyezi Mungu zinazosimamia haki bila kuzingatia manufaa.
Imeandikwa na Said Bitomwa
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania
Kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Maoni hayajaruhusiwa.