Kuangazia Mkutano Wa Nishati Afrika “Mission 300”
بسم الله الرحمن الرحيم
Tarehe 27 na 28 Januari, 2025 ulifanyika Mkutano wa nishati Afrika au Mission 300. Mkutano huo uliwakutanisha maraisi 21 wa nchi za Afrika, viongozi wa biashara, washirika wa maendeleo, na wadau wakuu katika juhudi za kuwafikishia umeme wakazi wa Afrika. Mkutano ulilenga kuangazia namna bora ya kufikia lengo la kuwafikishia umeme watu milioni 300 katika bara la Afrika ifikapo mwaka 2030. Mwishoni mwa mkutano kulitolewa tamko la pamoja la utekelezaji lililoitwa “Tamko la Nishati la Dar es Salaam”
Itakumbukwa kwamba miongoni mwa Malengo ya Milenia yaliyobuniwa mwaka 2000 na kutekelezwa mpaka 2015 yalilenga kuimarisha upatikanaji wa nishati kupitia lengo lake la “kuimarisha mazingira”. Mpaka malengo haya yanafikia tamati mwaka 2015 na kubuniwa malengo mapya yaliyoitwa Malengo ya Maendeleo Endelevu ambayo nayo yamebakisha miaka mitano yafikie tamati kwa sababu yalibuniwa mwaka 2015 na kupangwa kufanyiwa kazi mpaka mwaka 2030, nayo kupitia lengo lake la “nishati mbadala kwa gharama nafuu” nayo pia yanalenga kutatua changamoto za nishati bila mafanikio.
Upatikanaji wa umeme wa uhakika ni muhimukwa ukuaji wa kiuchumi wa Afrika. Ukosefu wa umeme wa kutosha unapunguza pato la ndani la Afrika kwa asilimia 2 hadi 4.
Kwa mujibu wa Shirika la Nishati la Kimataifa (International Energy Agency) kati ya mwaka 2019 na 2021, idadi ya watu barani Afrika wanaoishi bila ufikiaji wa umeme iliongezeka kwa 4%. ambapo ni zaidi ya watu milioni 600 hawana nishati hiyo katika bara la Afrika.
Na kwa upande wa Tanzania zaidi ya nusu ya wakaazi wake hawana umeme.
Hii inaonesha wazi ni kwa kiasi gani mikakati hii ya kibepari huanzishwa na kuisha imuda wake, ihali Afrika ikiendelea kuwa katika ukosefu wa nishati hiyo.
Kwa upande mwengine, ukiangalia kwa makini Mkutano huu utaona wazi wazi hali ya utegemezi wa wazi wa Bara la Afrika kwa wakoloni wa kimagharibi, kwani taasisi za kikoloni za kifedha ndiyo zinazofadhili mradi huu wa misheni 300 kwa kiasi kikubwa. Benki ya Dunia inapanga kutenga dola za Marekani bilioni 48 katika ufadhili wa mradi huu hadi mwaka 2030 ili kuharakisha usambazaji wa umeme. Ufadhili huo unalenga kutoa umeme kwa watu milioni 250 na nishati safi ya kupikia kwa watu milioni 50 na zaidi.
Taasisi ya Rockefeller ya Marekani itatoa msaada wa kiufundi wa dola za Marekani milioni 20 ili kuandaa mipango ya nishati mahususi ya nchi. Kadhalika, serikali za nchi kadhaa ikiwemo Ufaransa zinatarajiwa kutoa mchango katika mradi huu. Hii inaonesha wazi kuwa licha ya bara la Afrika kupata “uhuru wa bendera” katika miaka ya 1960, bado lipo katika dimbwi kubwa la utegemezi wa mataifa ya kikoloni ya Magahribi, ambapo mipango ya kikoloni na utegemezi kwao hailengi ila maslahi ya kinyonyaji kwa wakoloni tu, na kamwe haitazaa matunda chanya, zaidi ya kuwa mzigo wa hali ngumu na madeni yatakayowaelemea raia wanyonge.
Afrika lau ingekuwa huru na imebeba mfumo thabiti ingeweza kujinasua na ukosefu wa nishati na umeme kwani ina rasilimali nyingi muhimu kwa ajili ya uzalishaji wake. Asilimia 60 ya nishati ya jua ulimwenguni inapatikana Afrika. Mpaka mwaka 2012 hifadhi ya gesi asili iliyogundulika Afrika ni futi za ujazo trilioni 625, hifadhi ya makaa ya mawe takribani tani bilioni 16.4, hifadhi kubwa ya nishati ya upepo ambapo Afrika ina uwezo wa kuzalisha GW 100 lakini ni GW 5-6 pekee ndiyo huzalishwa kupitia nishati ya upepo.
Kuhusiana na mabwawa Afrika ina mabwawa makubwa ya kuvuna umeme wa maji na ina maeneo ambayo yanaweza kutengenezwa mabwawa ya kuvuna maji kwa ajili ya umeme. Kwa mfano, bwawa la Inga la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika maporomoko makubwa ya maji, kando na jiji la Kinshasa lina uwezo wa kuzalisha hadi GW 43.5 na mahitaji ya Afrika ni GW 120. Hii inamaanisha kuwa bwawa la Inga pekee linaweza kuzalisha theluthi au 30% ya nishati ya umeme unaohitajika Afrika. Miaka ya nyuma Inga ilikuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa kuweza kutumiwa na bara zima.
Pia Afrika ina hifadhi kubwa ya 18% ya madini ya uranium duniani ambayo ina uwezo wa kutumika kuzalisha nishati umeme, nyuklia nk. Kwa mfano, ndani ya Tanzania yanapatikana katika mikoa ya Ruvuma, Dodoma, Singida, Manyara na Arusha ambapo mnamo mwaka 2011 aliyekuwa Waziri wa Nishati na Maadini wa Tanzania,William Ngeleja aliwahi kutamka kwamba uchimbaji wa uranium Tanzania utaiweka kuwa nchi ya sita duniani kwa uzalishaji mkubwa wa maadini hayo nyeti.
Kwa hakika, mikakati hii haileti ufumbuzi wa tatizo husika, kwani mipango na programu hizi zinazoitwa za kukomboa Afrika na tatizo la nishati hupangwa na mabepari wakoloni wanaonufaika na matatizo ya Afrika na rasilimali zake na sio kuondoa tatizo. Kwa mfano, makampuni ya kibepari kama ExxonMobil na Total ndiyo wanaonyonya gesi ya Msumbiji, Kampuni ya Rössing ndiyo wanaokwapua uranium ya Namibia nk.
Afrika itajikwamua katika janga kubwa la ukosefu wa nishati ya umeme pale tu mfumo wa Kiislamu chini ya dola yake itakaposhika hatamu, kwa kuwa Uislamu umeweka kila aina ya tahadhari kuhakikisha mwanadamu mmoja hatumii fursa ya rasilmali zilizopo vibaya kibinafsi na kuwanyima wengine kwa kuwadhikisha.
Mfumo wa Uislamu umegawa kwa uadilifu baina ya mali za binafsi, mali za serikali na mali za Umma. Na ukazifanya huduma zote za kijamii ikiwemo vyanzo vikubwa vya kuzalisha umeme kuwa ni mali ya Umma na ukaharamisha kuzifanya milki za kibinafsi.
Akasema Mtume (SAAW):
“Watu ni washirika katika mambo matatu: Maji, moto na malisho ya wanyama”
Na tamko ‘moto’ katika Hadithi hii hujumuisha vyote vinavyozalisha moto ukiwemo umeme.
Kwa hivyo, mtazamo wa mfumo wa Uislamu kwa huduma hii ya umeme ni miongoni mwa mali za Umma (public property) inayohitajika na Umma mzima, na ni lazima na wajibu kwa Khalifah(kiongozi wa dola) katika jukumu lake la kuwatumikia Umma kuwekeza kila aina ya nyenzo na jitihada kuhakikisha wananchi wanaipaita huduma hiyo kiurahisi na sio kibiashara wala kubinafsishwa ili wananchi wasiishi katika dhiki.
Ni wakati muwafaka kwa Umma Afrika kushiriki katika mchakato wa kuu’ngoa kabisa mfumo wa kibepari kwa mbadala wa mfumo imara, thabiti na wa uadilifu (Uislamu). Huu ndio mfumo pekee wenye ghera na uwezo wa kuwahudumia raia wote na kuzitumia vyema rasilmali za Umma kwa uadilifu na insafu, kinyume na ubepari na ukoloni mamboleo ambao umeitosa Afrika katika dimbwi la unyonge, ufukara na dhiki kwa kupora rasilmali zake kwa maslahi ya makampuni yao makubwa ya kibepari. Kisha wakoloni hao hao wanyonyaji ati huzuka na programu na mipango isiyo na tija kama hii ya misheni 300 (mission 300).
Said Bitomwa
Risala ya Wiki No. 201
27 Shaaban 1446 Hijri | 26Februari 2025 Miladi
Maoni hayajaruhusiwa.