Kuangazia Mafanikio ya Risala ya Uislamu

Kama Ummah bora tulioletwa kwa ajili ya kuunusuru ubinadamu kuna haja na jambo muhimu kufanya tafakuri ya kina namna mfumo wetu wa haki wa Uislamu ulivyoleta athari kubwa kwa wanadamu sio tu katika Bara Arabu bali takriban ulimwengu mzima

Uislamu ulianza kuwatoa waarabu katika ujinga wa kiza wakiwa watu duni wasio na ghera ya chochote zaidi ya husuma na vita vya kikabila baina yao kwa maslahi binafsi. Kisha ukawapandisha na kuwafanya kuwa watawala wa ulimwengu na watu waliostaarabika, wakieneza Uislamu mashariki na magharibi.

Mara tu baada ya Mtume SAAW kuingia Madina na kuasisi dola ya mwanzo ya Kiislamu, aliandaa mazingira ya vita vidogo vya Ghazwatul Abwa kwa lengo la kudhoofisha uchumi wa makureish kwanza, na kisha kuandaa vita vikubwa rasmi katika mwaka wa 2 Hijriya, yaani Vita vya Badri.

Chini ya Uislaamu waarabu, waafrika, wazungu nk. waliunganishwa pamoja chini ya dola kubwa ya Kiislamu ikitabikisha Uislamu kimfumo na kuwatoa watu kutoka katika zama za kiza (dark ages). Ikawa serikali ya Kiislamu ya Khilafah ndio muangalizi na msimamizi wa masuala ya ndani na kimataifa, bila ya kutaja namna ilivyokuwa dola ilivyokuwa imara kifikra, yenye ushawishi mkubwa na kumiliki nguvu za kijeshi zilizotumika kuwasulubu maadui, kuangusha tawala zao za kikafiri na kuwakomboa wanadamu kutokana na ila aina ya dhulma na ukandamizaji kabla ya kuangushwa dola hiyo mwaka 1924 Miladia.

Waislamu daima walibeba ujumbe wa Uislamu na bendera yake wakijua ni wajibu wao kuwafikishia walimwengu kwa ufafanuzi ulioambatana na huruma na mapenzi kama unavyofundisha. Hawakujinasibisha Waislamu na utaifa, uzalendo au misimamo ya ukabila kama leo hii, ambapo leo Saudia kwa wasaudia, Misri kwa wamisri, Iran kwa wairani nk. Bali Waislamu zama hizo walijitolea kama Ummah mmoja kwa muhanga wa hali ya juu kwa kuacha majumba yao na kueneza ujumbe wa Uislamu waliokalifishwa na Allah Taala.

Lengo la risala ya Uislamu halikuwa kuasisi Dola ya Himaya ya Kibeberu (Empire), ambapo kama wangetaka wangeanzisha kwa jina la uarabu, na hapana shaka wangeishi kwa starehe na upumbazo japo kwa muda, kama tunavyoshudia leo mataifa ya kibeberu yakiongozwa na Marekani yanavyoishi kwa kueneza ukafiri, fikra zake, kunyonya na kudhulumu rasilmali za mataifa dhaifu kila mahala bila aibu.

Bali lengo la ujumbe wa Uislamu lilikuwa wazi na bayana kama anavyosema mmoja wa makamanda wa Kiislamu wa jeshi la Khilafah pindi walipoifungua/ fathi dola ya Wafursi (Iran na Iraq kwa sasa) ambapo Kamanda Rabii Ibn Amir aliwaeleza majemadari wa kifursi walipomuuliza lengo la ujio wao, kwa kusema:

“Allah ametuamrisha kutoka nje ili kuwakomboa wanadamu kutoka kuwaabudu viumbe na kuwaleta kumuabudu Allah pekee na kuwatoa katika mtazamo finyu kuhusu huu ulimwengu na maisha yake na kuwa na mtazamo wa maisha ya baadae baada ya kufa “

Kwa ujumbe wa Uislamu daima Waislamu walikuwa wakiishi na wengine bila ya ubaguzi wala kufanya utabaka nao, hapakuwa tofauti baina ya mkomboaji na mkombolewa, ilikuwa vigumu kuwatofautisha raia na kiongozi, daima viongozi walikuwa wapo kuwatumikia raia katika kila hali na bila ya ubaguzi uwe wa kikabila, kieneo au kidini. Kinyume kabisa na uongozi katika zama zetu ambapo huchukuliwa kuwa ni fursa mwanana (golden chance) ya kujinufaisha mtu binafsi, familia yake na wapambe wake.

Leo wakati tukishuhudia kutamalaki kwa mfumo wa dhulma wa kibepari (capitalism), lazima tuwe na yakini kwamba kitu kilicholeta mafanikio makubwa kwa Ummah wetu zama zilizotangulia ni Uislamu pekee kupitia dola yake ya Khilafah ambapo uliweza kuwatoa watu kutoka katika viza na kuwaleta katika nuru kwa idhini ya Mola SW na kuwanyanyua kufikia kilele cha uongozi wa ulimwengu na ustaarabu kwa wanadamu.

Leo kwa kujitenga na Uislamu kumeufanya Umma wetu kurudi nyuma licha ya nguvu ya tareekh yetu yenye kung’ara na rasilmali zilizosheheni katika ardhi zetu.
Si waarabu walioinuka kwa kupitia uarabu wao kwa majukwaa kama Jumuiya ya Nchi Kiarabu/ The Arab League na mengineyo, bali wamekuwa watu duni wanaodhalilishwa na wakoloni makafiri, wakinyonywa, kufedheheshwa na kudharauliwa.

Aidha, waafrika nao licha ya jumuiya yao ya Umoja wa Afrika na majukwaa mengine pia wameshindwa kikamilifu kujikomboa na kuepukana na dhulma za ubepari na ukoloni. Yote ni kwa kuwa majukwaa hayo ni ala tu za wakoloni kwa ajili ya kusahilisha kuwatawala, kuwanyonya na kuleta mgawanyiko baina yao.

Ulimwengu wote kwa jumla unahitaji kurudi tena nuru ya Uislamu kupitia dola yake ya Khilafah inayostahiki kuanzia katika ardhi kubwa za Waislamu, kisha kusambaa kila mahali kuwakomboa wanadamu na kuwaunganisha watu wote chini ya kivuli cha kheri na uadilifu bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Abdul Karim Manyuka
Risala ya Wiki No. 60
30 Swafar 1441 hijri 29 /10/2019 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
https://hizb.or.tz/

Maoni hayajaruhusiwa.