Janga La Bir- Maun (Safar 4 Hijri)

بسم الله الرحمن الرحيم

Moja katika matukio ya kuhuzunisha katika tareekh ya Uislamu ni janga la mauaji waliyotendewa Waislamu katika eneo la Bir-Ma’una (Kisima cha Ma’una). Mauaji haya yaliotokea katika zama za Mtume SAAW ndani ya mwezi kama huu wa Safar.

Itakumbukwa kwamba siku chache kabla ya janga hili pia makafiri wa Banu Lihyan walitenda mauaji kama haya (Ar-Raji)’. Makafiri walitaka kupatiliza mtihani wa Waislamu kushindwa katika Vita vya Uhud ili kuwadhoofisha na kuwamaliza kabisa.

Mauaji ya Bir- Ma’una yalijiri baada ya Abu Bara wa kabila la Bani Amir kumtaka Mtume SAAW ampatie masahaba wake wakahubiri dini katika eneo lao la Najd. Mtume SAAW alisitasita juu ya usalama wa masahaba zake lakini Abu Bara akamuahidi kulinda usalama wao. Kuna kauli kwamba masahaba hawa walikuwa 40 au 70, na takriban wote walikuwa wanavyuoni, mafuqaha na mahafidhul Quran wakubwa.

Kwa ufupi, msafara huu ulikuwa timu nzito ya wataalamu. Kiongozi wa msafara alikuwa Al-Mundhir bin ‘Amr ra. Ansar wa kabila la Banu Sa‘ida. Walipofika eneo la Bir-Ma’una (Kisima cha Ma’una) walimtuma mjumbe maalumu kupeleka risala ya Mtume SAAW kwa mmoja miongoni mwa viongozi wa kabila la Bani Amir.

Amir bin Tufayl, kiongozi wa kabila hilo alikataa hata kuisoma risala hiyo tukufu na akaamrisha mjumbe aliyepeleka barua hiyo apigwe mkuki na kuuwawa. Hapo hapo Amir bin Tufail, kwa haraka sana akakusanya kabila lake na makabila mengine ili kuwapiga Waislamu.

Kabila la Bani Amir lilikataa kuingia katika medani ya vita kwa kuzingatia kuwa Abu Bara alikwishachukua dhamana kwa Mtume SAAW kuwalinda masahaba zake .

Bwana Amr bin Tufail, hakuvunjika moyo akachukuwa usaidizi wa kabila jingine la Bani Salim pamoja na makabila mengine kuwashambulia Waislamu. Msafara wa masahaba ukawa hauna namna ila kupigana mpaka wakafa mashahid takriban wote isipokuwa mmoja tu.

Ka‘b bin Zaid bin An-Najjar ra. ndie aliyesalimika na alidiriki kurejea Madina akiwa kajeruhiwa. Mtume SAAW alihuzunishwa sana na khiyana na mauaji haya mawili ya Bir Ma’una na yale ya awali ya Ar-Raji. Kwa kuwa mauaji haya hayakuwa vita kiudhati, bali ni khiyana tu ya makabila, lakini pia si tu Mtume SAAW alipoteza masahaba zake waliokuwa wanavyuoni wakubwa.

Hivyo, bila ya kuchelewa Mtume SAAW akiwa mwanasiasa thabiti na kiongozi jasiri akachukua hatua za kisiasa, kiibadat na kijeshi kukabiliana na hali hiyo. Akapata maelezo ya kina juu ya tukio hili kutoka kwa Amr bin Umayyah ambae alikuwa karibu na eneo lilipotokea. Upande wa dua aliomba dua kali kwa siku 30 kumkabili Mola, Mwenye Nguvu dhidi ya uovu, khiyana ya makabila haya.
Hatimae, miezi michache katika mwaka ule ule wa 4 Hijria baada ya kumaliza kuwapiga na kuwatimua mayahudi wa Bani Nadhir, Mtume SAAW akatuma jeshi katika mji wa Najd kupambana dhidi ya makabila haya na mengineyo ili kukomesha kabisa maonevu, dhulma na usaliti wao.

Hali iko kinyume na watawala wa ulimwengu wa Kiislamu leo. Waislamu wanaangamizwa mbele ya macho yao kama wanavyoangamizwa Waislamu wa Gazza na mayahudi na washirika wake kwa mauaji ya halaiki ilhali Misri, Jordan, Lebanon nk. wanakodoa macho, bali baadhi ya watawala wanawasaidia mayahudi kuwamaliza Waislamu. Vivyo hivyo, Waislamu waliangamizwa na Marekani katika Iraq ilhali Saudia na Iran zikikodoa macho na Saudia kutoa ardhi yake kufanikisha hilo.

Pakistani ilikuwa kimya kwa maangamizi ya Waislamu wa Afghanistan na bado inakodoa macho tu bila ya hatua thabiti kuikomboa Kashmiri kutoka kwa dhulma ya mabaniani. Bila ya kusahau Bangladesh namna ilivyowaacha mkono Waislamu wa jamii ya Rohingya wa Myanmar wanaochinjwa kama kuku na kuangamizwa na washirikina (mabudha).

Kwa ufupi, Umma unahitaji kiongozi mkweli ambaye ni Khalifah ili kuja kuwakomboa na mauaji, dhulma, mateso idhilali nk. na hauahitaji vibaraka waliopo leo katika ulimwengu wa Kiislamu ambao ni wakala wa madola ya kibepari kama sio watumwa kamwe.

Shime Umma wa Kiislamu tufanyeni kazi ya wajibu ya kulingania Uislamu ili kurejesha tena dola ya Khilafah Rashidah iwe mbadala wa vibaraka tuliowekea na makafiri katika ulimwengu wote wa Kiislamu.

Risala ya Wiki No. 188
15 Safar 1446 Hijri / 20 Agosti 2024 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut Tahrir Tanzania
#AqsaCallsArmies

Maoni hayajaruhusiwa.