Hizb ut Tahrir Tanzania Yazindua Kampeni ya Miaka 100 ya Kuangushwa Khilafah
بسم الله الرحمن الرحيم
Jana tarehe 01 Rajab 1442 Hijri / 13 Februari 2021 Miladi, wanaharakati wa Hizb ut Tahrir Tanzania walifanya amali ya visimamo na mabango katika mikoa mbali mbali katika uzinduzi wa kuanza rasmi kampeni ya: “Miaka 100 ya Kuangushwa Khilafah” Tukio lilitokea mwezi wa Rajab 1342 Hijri/ Machi 1924 Miladi
Siku moja kabla ya amali hiyo, Ijumaa tarehe 30 Jumada al-Akhir/ 12Februari 2021 kwa kutumia majukwaa ya Ijumaa wanaharakati hao walizungumza na hadhira katika misikiti mbali mbali wakifikisha risala kitaifa kuitangaza kampeni hii ya kilimwengu.
Miongoni mwa maeneo yaliyozinduliwa kampeni jana ni jiji la Dar es Salaam, nje ya Msikiti wa Kichangani (Magomeni), Msikiti wa Mtoro (Kariakoo), Msikiti Idrissa (Kariakoo) na Masjid Nur, Mbande Mbagala.
Kwa upande wa Zanzibar Misikiti ya Mchangani na Mbuyuni (Unguja mjini) Masjid Qatar Chake chake (Kisiwani Pemba), pia baadhi ya misikiti mashuhuri mikoani Mwanza na Tanga.
Amali hiyo ya kisimamo na mabango iliambatana na risala fupi kuwakumbusha Waislamu juu ya machungu na hali ya msiba mkubwa unaopitia Umma kwa kukosekana Khilafah, jukumu la kisharia kwa Umma kuirejesha dola hiyo, na pia kutoa mwito kwao kujumuika na Hizb ut Tahrir kwa kufanya kazi nayo na kuinusuru, kwa kuwa Hizb ut Tahrir ina uwezo wa dhati kuukomboa Umma kwa kupitia Uislamu.
Kampeni ya Miaka 100 ya Kuangushwa Khilafah itaendelea ulimwenguni kote katika kipindi chote cha mwezi wa Rajab ikihusisha amali mbali mbali za kiwango cha kieneo na kilimwengu.
Masoud Msellem
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari
Hizb ut Tahrir Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.