Hijja Na Mafunzo Yake
بسم الله الرحمن الرحيم
Hijja ni ibada ya kale kabisa iliyoanzia tangu zama za Nabii Ibrahim As. na kuendelea hadi sasa. Ibada hii lau Waislamu watayazingatia mafunzo yake kwa makini itawafanya wawe wachamungu na kuweza kupata radhi za Allah SW hapa duniani na kesho akhera. Ibada hii asili yake ni amri ya Allah SW kwa Nabii wake Ibrahim AS pale alipowaamrisha IbrahimAs na mwanawe nabii Ismail As waisimamishe nyumba ya Al- Kaabah na kisha atangaze kwa watu wote kuizuru. Anasema Allah Taala:
وَأَذِّنْ فِي النَّاسِ بِالْحَجِّ يَأْتُوكَ رِجَالاً وَعَلَى كُلِّ ضَامِرٍ يَأْتِينَ مِنْ كُلِّ فَجٍّ عَمِيقٍ
“Na (Tukamwambia) “Utangaze kwa watu habari za Hijja, watakujia (wengine) kwa miguu na (wengine) juu ya kila mnyama aliyekonda (kwa machofu ya njiani) wakija kutoka kila njia ya mbali” (22:27)
Kwa akili ya kawaida mtu atafikiria kuwa kujenga msikiti porini na kisha uwaite watu kwa ajili ya ibada ni suala la kiwendawazimu, lakini kipenzi chetu Nabii Ibrahim As alijenga na kutangaza bila kutazama hali ilivyo, kwa kuwa amekinai kuwa hiyo ni amri ya Allah Taala ambayo inahitaji kutekelezwa tu. Akili haina nafasi ya kuhoji amri za Alllah Taala bali kazi ya akili ni kufahamu tu amri hiyo na muhusika hana budi kutekeleza tu. Kwa mfano tunaona tendo la kumchinja mwanao ni baya na ovu na haliingii akilini lakini kumbe sheria ya Allah Taala ikija hutekelezwa tu kama alivyotekeleza Ibrahim na Ismail As. Na kamwe akili haina nafasi ya kuhoji kwani mafanikio yetu yapo kwenye kumtii Allah Taala tu na sio kwa kufuata akili zetu.
Tunaona, Nabii Ibrahim As alipopewa agizo na Allah Taala kuwa amuweke mkewe na mwanawe Ismail As porini hakuhoji bali alitekeleza hilo kwa kujua Allah Taala yupo pamoja nao kwa kule kutii kwake amri yake.
Aidha, ibada hii inatukumbusha namna Manabii Ibrahim na Ismail As. walivyokuwa wanyenyekevu kwa kutii amri za Allah Taala hata ikibidi kupoteza vipenzi vyao na roho zao. Walitekeleza amri ya kutoa muhanga huku wakiwa na yaqini kuwa atakaechinja atateketeza uhai wa mwanawe, ilhali mtoto akijua atapoteza uhai wake. Lakini hawakujali matokeo hayo ila walichokijali ni kupata radhi za Allah Taala tu.
Tukio la Nabii Ibrahim As. kupambana na shetani kwa kumpiga mawe wakati shetani alipojaribu kumhadaa kwa kumkataza asimchinje mwanawe ni dalili ya mapambano ya kudumu baina yetu na shetani na kila aina ya sera, nidhamu na mfumo wa kishetani.
Waislamu tunatakiwa tujifunze kupitia tukio la kuchinja mnyama kwa kuwa tayari kutoa muhanga hata roho zetu ikibidi kuinusuru dini ya Allah Taala na matukufu yake, bila ya kujali matokeo yake.
Kwa upande mwengine, ibada hii inatuonyesha namna gani mwanaadamu anavyotakiwa kuchukuwa hatua zake za kibinaadamu katika kukabiliana na matatizo mbali mbali kisha ndani yake ndimo hupatikana msaada wa Allah SW. Hili linadhihirika katika tukio la kuhangaika mama Hajjar As. kwenda baina ya milima miwili ya Swafa na Marwa ili kumtafutia mwanawe maji, kisha Allah Taala akampatia maji chini ya miguu ya mwanawe (Zam- zam). Vipi basi leo Waislamu watarajie msaada na nusra ya Allah Taala bila ya kutekeleza kwa vitendo amri za Allah Taala au huku wakishika njia batil? Basi tujue kuwa nusura ya Allah SW ipo kwa wanaomtii na wanaotekeleza mzunguuko wa kibinadamu kama walivyoamrishwa.
Tukio la kusimama Arafah linatufundisha kuwa ipo siku watu watasimamishwa mbele ya Allah SW na kuhesabiwa matendo yao. Basi jee tumejitayarisha vipi na siku hiyo ambayo atakaeokoka ni yule aliyemuitikia Allah Taala tu peke yake?
Hijja inatuonyesha uwezo wa Waislamu kuamrisha na kuwalazimisha makafiri jambo na matakwa yao. Jambo ambalo huwezekana tu pale tunapokuwa na nguvu za kiutawala wa dola. Hili limefanyika wazi pale Mtume SAAW alipomuamrisha Sayyidna Ali RA. akawasomee washirikina aya kuwapiga marufuku wakome kuja hijja na kutufu Al-Kaabah kijahilia.
Zaidi ya hayo pia hijja inatukumbusha kusimamisha dola ya Kiislamu ya Khilafah ili kuondoa usimamizi wa ibada hiyo kwa utawala wa kitwaghuti wa sasa. Je hatuoni leo, namna wanavyoidogosha na walivyoisimamisha ibada hiyo ati kwa visingizio cha Corona ilhali mikusanyiko mingine ya kifuska inaendelea kama kawaida. visivyo vya msingi. Pia utawala wa kitwaghuti wa kifalme wameifanya hijja mradi wao kwa kila hujaji anayekwenda kuhiji analazimika kununua viza ya kuingia ardhi tukufu,huku si kuwadhulumu Waislamu? Je hii sio bid’aa?
Bila ya kutaja udhaifu wa utawala huo katika kusimamia usalama kiasi cha kupelekea kupotea maisha ya mahujaji kwa maelfu kama ilivyotokea Septemba 2015 (1436 Hijri)
kufuatia msongamano wa Mahujaji katika mji wa Mina uliotokana na uzembe wa dola dhalimu ya Saudia
Ni wajibu Waislamu tumuitikie Allah SW ili kuondosha dhulma hizi na bidaa hii kwa kurejesha tena serikali yetu ya Kiislamu (khilafah) ili tuweze kuchukua mafunzo ya hijja kivitendo na kuhiji bila ya kudhulumiwa kwa kutozwa visa, kugawanywa na kuwanufaisha madola ya kikafiri na vibaraka wao.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ
“Enyi mlioamini! Muitikieni Allah na Mtume wake anapokuitieni katika yale yatakayokupeni uhai mzuri (wa duniani na akhera)” (8:24)
Maoni hayajaruhusiwa.