Funzo La Kisiasa Siku Za Mwisho za Khalifah Umar bin Khatwab
Katika mwaka wa 23 Hijiria mwishoni mwa mwezi wa Dhul-hijjah siku ya Jumatano Khalifah Umar R.A alijeruhiwa vibaya kwa dhoruba kali ya upanga wakati alipokuwa akiswalisha swala ya alfajiri.
Dhoruba kali ya upanga aliyopigwa kwa uadui na uovu na Abu Lu’u Lu’u (laana ya Allah iwe juu yake) lilikuwa ni jaribio lililokusudiwa kumuuwa kabisa, na kwa masikitiko makubwa baada ya siku chache tu alifariki dunia.
Alifariki dunia katika mwezi wa Muharram siku ya Jumapili, siku nne tu baada ya kumalizika mwezi wa Dhulhijjah akiwa na umri wa miaka 63. Huku kifo chake kikiacha msiba mkubwa usiomithilika kwa Umma mzima wa Kiislamu.
Khalifah Umar R.A atakumbukwa daima kwa mengi katika zama za Khilafah yake kuanzia msimamo wake thabiti katika Uislamu, ujasiri, uadilifu , ucha Mungu na kufanya fathi/ ufunguzi katika maeneo mbali mbali kwa kueneza nuru ya Uislamu mashariki na magharibi kutokana na kuandaliwa mazingira mazuri na Khalifah aliyemtangulia Abubakar RA, ambae kwa bahati mbaya yeye binafsi hakuweza kufungua miji mingi kutokana na kukabiliwa na wimbi kubwa la matatizo ya ndani.
Moja katika tukio kubwa la kihistoria ambalo milele Umar R.A atakumbukwa ni kitendo chake cha ujasiri kinachodhihirisha kupevuka kwake kisiasa kwa kuandaa mazingira mwanana yaliyosahilisha kupatikana Khalifah baada ya kufariki kwake.
Siku chache kabla ya kifo chake katika hali ya kuwa na majeraha makali kama aliyoyapata, Waislamu walimkabili Umar RA awapendekezee mtu wa kushika wadhifa wa Khilafah baada yake. Umar RA aliwajibu yafuatayo:
‘Kama nitamteua mtu baada yangu hakutokuwa na kasoro yoyote katika hilo kwa vile Abubakar aliniteuwa mimi baada yake, nae alikuwa mbora kuliko mimi. Lakini kama sitoteuwa mtu baada yangu, hakutokuwa na kasoro yoyote kwani Mtume wa Allah hakuteuwa mrithi wake, nae alikuwa mbora kuliko sisi sote’ (mimi na Abubakar)
Hatimae baada ya maswahaba kumshikilia na kumsisitiza sana awateulie wa kuishika nafasi baada yake kwa kuchelea kwao Umma kusambaratika na kupelekea kuzuka fujo na vurugu. Umar alimchagua sahaba mashuhuri Suhaib Al- Rum kuwa Amiri wa muda ili asimamie zoezi zima la kumchagua Khalifah kwa kipindi chote cha mchakato wa kumtafuta , pia alimtaka awe imamu wa swala zote za jamaa kwa kipindi chote cha kujeruhiwa kwake, kadhalika alimpa jukumu awe imamu wa jeneza lake lau atafariki dunia. Na zaidi akampa mamlaka yote ya kumtia adabu ya atakaekwamisha zoezi au kuleta upinzani baada ya kupatikanwa Khalifah.
Kwa hivyo, Umar akawateua Ali bin Abi Twalib, Uthman bin Affan, Abdulrahman bin Auf, Talha, Zubeir na Saad bin Abi Waqas. Maswahaba hawa sita aliwaweka chini ya usimamizi wa Suhaib kama Amiri wa muda ili mmoja wao awe Khalifah baada yake baada ya kuupitia mchakato wa uchaguzi. Na Umar akawaeleza wazi kwa matamshi ya kihistoria alipotamka:
‘Enyi kundi la Muhajirina Hakika Mtume wa Allah alikufa na aliridhika na nyie nyote sita. Nimelifanya suala la Khilafah ni suala la mashauriano miongoni mwenu , ili kwamba muweze kuchagua mmoja miongoni mwenu kama Khalifah. Kama watano miongoni mwenu wakikubaliana juu ya mtu mmoja, na mmoja akapingana nao basi muuweni, kama wanne wakiwa upande mmoja na wawili wakiwa upande wa pili na kupinga, basi wauweni hao wawili, na kama watatu wakiwa upande mmoja na watatu wako upande mwengine basi Abdul Rahman bin Auf atakuwa na kura ya kukata shauri na Khalifah atachaguliwa kutoka kundi lake, katika hali kama hiyo wauweni watatu waliobaki lau watapinga kwa kuleta upinzani’. (Tariukh- Twabbary)
Baada ya kufariki Umar R.A, na kufuatia mchakato aliouweka wa kutafutwa Khilafah baada yake, Waislamu kwa umoja wao waliwafikiana kumchagua Uthman bin Affan RA kuwa Khalifah baada ya Umar na akapewa rasmi ba’iya/ kiapo cha utii na Waislamu ,na akashika hatamu za uongozi wa dola ya Kiislamu.
Katika qadhia hii tunajifunza namna Waislamu wa wakati huo walivyojengeka katika upeo wa hali ya juu kabisa katika siasa za Kiislamu. Siasa zilizoongozwa na fikra sahihi za Kiislamu kiasi kwamba wakati wote Umma ulihisi uhai wake unapokuwa unasimamiwa mambo yake na kiongozi wa Kiislamu ambae ni Khalifah, na kamwe hawakuruhusu Umma ubakie bila ya mchunga kama hali yetu tulivyo leo.
Ni Umma ndio uliomtaka Umar RA aandae mazingira ya kupatikana kiongozi baada yake nae akachukua jukumu hilo kwa kumteuwa Amiri wa muda kusimamia mchakato mzima wa kuteuwa Khalifah mpaka kukamilika kwake .
Ufahamu huo unatokana na msingi kabambe na thabiti alioutandika Mtume SAAW pale aliposema:
“Walikuwa mayahudi wakisimamiwa mambo yao na Mitume kila alipokuwa akifariki Mtume wakiletewa Mtume mwengine, na baada yangu hakutakua na Mtume bali kutakua na makhalifa.” Maswahaba wakamuuliza: “jee unatuamrisha nini juu yao”, akawajibu SAAW: “wapeni ba’iya mmoja baada ya mwengine.”
Kwa hivyo, kutoa ba’iya kwa Khalifaha ni wajibu lakini wajibu huo hauwezi kutekelezeka ila kwa kupatikana Khalifah. Hivyo ni jukumu la Umma kumtafuta Khalifah ili kuweza kutoa kiapo cha utii juu yake, kwa sababu katika sharia ya Kiislamu kuna qaida / kanuni inayosema:
“kila kinachopelekea wajibu kukamlika huwa nacho ni wajibu”
#UislamNiHadharaMbadala
05 Septemba
Maoni hayajaruhusiwa.