Funzo Kutoka Janga la Karbala

Kitendo cha Yazid Muawiya kumuuwa kinyama na kikatili Imamu Hussein ra. mjukuu na kipenzi cha Mtume saaw akiwa pamoja na familia yake na Waislamu zaidi ya 70 katika msafara wake katika eneo la Karbala (Iraq) ni katika matukio machungu, mabaya, yanayotia majonzi na kuhuzunisha kusiko na mithili.

Imamu Hussein ra. alitoa muhanga nafsi yake na watu wake kwa kusimama kidete kulinda hukmu ya kisharia ya kuhifadhi na kutetea haki ya Ummah wa Kiislamu kuchagua Khalifah kwa mujibu wa ba’iya ya kisheria (kiapo cha utii ) na sio kulazimishwa, kuporwa uongozi kwa nguvu au kuufanya kuwa urathi wa kifamilia kama alivyofanya Yazid bin Muawiah kwa kulazimisha kwa nguvu.

Imamu Hussein ra. Alisimama kidete kulinda na kutetea heshima na haki hiyo ya Umma isiporwe, akielewa kwa kina ustawi na utengamano wa Waislamu ni kuwa na kiongozi wao (Khalifah) aliyechaguliwa kwa mujibu wa sharia.

Imamu Hussein ra. alibeba jambo hilo kuwa ni qadhia nyeti ya kufa na kupona, ambalo lau hawakurejeshewa Ummah, hali ya Waislamu na Uislamu wao utaporomoka.

Muda mchache kabla ya Imamu Hussein ra. kuuwawa kikatili alitoa kauli ya kishujaa na kihistoria ya kudhihirisha kuwa uongozi ndio uhai wa Ummah kwa kusema:

“Ikiwa dini ya Muhammad haitoweza kusimama ila kwa mimi kuuwawa , enyi panga njooni mnichukue”

10 Muharamu 61 Hijiria

#UislamuniHadharaMbadala

Maoni hayajaruhusiwa.