Fadhaa Ya Elimu Ya Kibepari

بسم الله الرحمن الرحيم

Wakati huu ambapo shule zipo karibu kufunguliwa baada ya kipindi cha mapumziko ya mwisho wa mwaka kwa wanafunzi, pia ni kipindi hiki ndio muda wa harakati na pirikapirika kwa wazazi na walezi wa wanafunzi kujiandaa kwa muhula mpya wa masomo ya mwaka mpya ambao utaanza sio muda mrefu.
Kwa masikitiko makubwa mfumo wa elimu wa kibepari unaoongozwa kwa misingi ya usekula, badala ya kuleta utulivu, faraja na sakina ya nafsi kwa wanafunzi, wazazi, walezi na jamii nzima umekuwa chanzo cha fadhaa, khofu na kuchanganyikiwa kwa wadau wote, iwe wanafunzi, wazazi, wazee na jamii kwa jumla.
Baadhi ya fadhaa na kuchanganyikiwa kunakotokana na mfumo wa kielimu wa kibepari ni kama yafuatayo:
1. Kugeuzwa elimu kuwa biashara na uwepo mfumo mbaya wa kiuchumi kumepelekea Jamii kuhangaika na kutapatapa katika utafutaji wa malipo ya ada, gharama za vifaa, kama sare mpya, madaftari, vitabu nk. kwa ajili ya watoto wao.
2. Kushindwa shule za Umma / serikali kutoa elimu ya kiwango stahiki hali inayopelekea kuhangaika na kutapatapa wazazi na walezi ili kuwapatia watoto wao shule za kibinafsi ambazo ni bora kuliko shule za Umma.
3. Kwa Waislamu wengi kutojua au kwa wamiliki wa mashule binafsi hususan yaliyobeba lakabu za Kiislamu kimakosa au kwa makusudi kuwaoneshwa wazazi, walezi, wanafunzi na jamii kwa jumla kwamba hukmu ya kisharia kwa elimu za kisekula ni jambo la faradhi. Jambo ambalo sio keli. Na hilo limepelekea:
• Kuchanganyikiwa kwa wazazi, walezi na wanafunzi kwa kuekeza juhudi kubwa kwa ufahamu kwamba elimu hizo ni faradhi, hivyo wao wamo katika ibada tukufu ya faradhi. Kimsingi elimu hizo ni mubaha.
4. Kunasibishwa elimu na ufanisi wa kimaisha, upeo wa kiuchumi na kuongezeka rizki, nako kumepelekea haya:
• Wazazi kuwekeza jitihada kubwa kiasi cha kuchanganyikiwa na kutumia rasilimali nyingi kuwasomesha watoto, na pale watoto hao wanapopata matokeo kinyume na matarajio yao, hilo huwapa hali ya kuchanganyikiwa kupita mipaka kwa wanafunzi, wazazi na walezi kwa kudhani kwamba wameshakosa fursa ya ukombozi wao wa rizki.
• Aidha, dhana ya elimu na rizki huzua tafrani kiasi kikubwa kwa kuharibu muamala mwema na mahusiano mahala pa kazi baina ya mwajiri na mwajiriwa (industrial relations) kwa kuwa mwajiri hutaraji uaminifu katika kazi yake ilhali mwajiriwa ana dhana kwamba ajira ndio chanzo cha rizki yake, iwe kwa kusaidia ndugu, kujenga, kuowa na kuhudumia familia, hata kama anacholipwa ni kiasi kidogo, mwajiriwa hulazimisha kuweza kupata hata kwa njia zisizo halali, ilimradi apate kazini hapo. Kwa kuwa huona kazi hiyo ni matunda ya elimu yake.
Hayo ni baadhi ya madhaifu yanayozua fadhaa na hali ya kuchanganyikiwa wazazi na wazee, hali inayotokomana na mfumo mbovu wa kielimu wa kibepari. Badala ya elimu kuwa faraja, kuwaletea watu utulivu, uchamungu na kuthaminiana imeleta natija ya mateso ya nafsi na hangaiko.
Ni wajibu Umma wetu kufanya kazi bila ya kuchoka wala kusita ili kurejesha maisha ya Kiislamu, ambapo Khilafah itatandika nidhamu bora ya kielimu yenye kufungamanishwa na Allah Taala isiyokuwa, mzigo, khofu wala fadhaa kwa wazazi na walezi.
الَّذِينَ آمَنُوا وَتَطْمَئِنُّ قُلُوبُهُمْ بِذِكْرِ اللَّهِ أَلاَ بِذِكْرِ اللَّهِ تَطْمَئِنُّ الْقُلُوبُ (الرعد: 28).
“Wale walioamini na wakatuliza nyoyo zao kwa ukumbusho wa Mwenyezi Mungu. Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndio nyoyo hutulia” (Ar-raad: 28)
Risala ya Wiki No. 122
27 Jumada al-awwal 1443 Hijri /31 Disemba 2021 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.