Disemba 861 Kumbukumbu ya Khalifah Al-Mutawakkil

بسم الله الرحمن الرحيم

Mwezi wa Disemba mwaka 861 Miladia alifariki dunia Khalifah Al-Mutawakkil ʽalà Allāh (المتوكل على الله). Huyu ni Khalifah wa kumi wa Abbasiya. Jina lake kamili ni Abu al-Faḍhl Jaʽfar ibn Muḥammad al-Muʽtaṣim billāh, alizaliwa Februari / Mach 822 Miladia, aliushika Ukhalifa baada ya kifo cha Khalifah Al-Wathiq.
Khalifah Al-Mutawakkil alifanya kazi kubwa ya kurejesha utengamano, kuhifadhi hadhi ya wanavyuoni, kupambana na uasi nk. Aidha, aliondosha hali ya kulazimishana katika matawi ya Aqida, amma kuifanya misimamo hiyo kuwa tabanni za dola kama walivyofanya baadhi ya makhalifah waliomtangulia.
Itakumbukwa ni Khalifa huyu ndio aliondoa hali ya kuwabanabana wanavyuoni kutokana na misimamo yao ya kutokubaliana na misimamo ya watawala waliotangulia katika masuala ya matawi ya aqida. Al-Mutawakkil alimuachia huru Imam Ahmad ibn Hanbal aendelea na misimamo yake baada ya kuwa katika udhibiti chini ya makhalifah waliotangulia waliokuwa wakilazimisha misimamo ya matawi ya kiakida kama vile (Quran kuwa kiumbe au la).
Khilafah Al- Mutawakkil pia alipambana na uasi na kurejesha mshikamano wa dola kwa kiasi fulani. Mnamo mwaka 851–852 / 237 Hijri alipambana na Warmenia walioasi kiasi cha kumuuwa Wali wa Khalifah.
Katika hali kama hiyo Khalifah alimtuma kamanda wake Bugha al-Kabir kukabiliana na wimbi hilo na kufanikiwa kulizima na kumtia nguvuni kiongozi wa uasi huo bwana Ishaq ibn Ismail katika mji wa Tiflis na kumuwa.
Pia, Khilafah ya Al- Mutawakkil ilifanikiwa kuzima uasi katika maeneo ya Homs, Syria ndani ya mwaka 854–855 / 240 Hijria
Bila ya kusahau kuwa ndani ya mwaka 241 Hijria Khalifah Al-Mutawakil alidhibiti uasi wa watu wa jamii ya Beja waliokuwa wakiishi Misri Ukanda wa Juu (Upper Egypt) walipogoma kutoa zakat. Khalifah alimtuma kamanda wake Al-Qummi kwenda kuidhibiti hali na kufanikiwa, na jamii hiyo ikaendelea kutoa zaka kama kawaida.
Hao ndio makhalifah walioubeba Uislamu chini ya nidhamu yake ya utawala ya Khilafah baada ya kuondoka Mtume SAAW.
24 Disemba 2020
Masoud Msellem

 

Maoni hayajaruhusiwa.