Demokrasia Nidhamu ya Undumilakuwili na Migongano

Rais Magufuli karibuni wazi wazi alimshauri waziri wake kuvuta bangi ili awe mkali aweze kuwakabili vyema wakandarasi wanaochelewesha chelewesha miradi ya serikali.

Raisi alitoa kauli hiyo karibuni akiwa ziarani Njombe kwa kumtaka Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Makame Mbarawa atumie kilevi hicho cha bangi ikiwa kufanya hivyo kutamfanya awe jasiri na asietetereka kuukabili uzembe wa wakandarasi.

Aidha, Raisi alitoa tena kauli karibuni zaidi mjini Mbeya inayodokeza kuunga mkono matumizi ya bangi katika ziara anayoendelea nayo mkoani Mbeya, aliposema kuwa wahehe kwao bangi ni kama mboga.

Kauli hizi za raisi kuhamasisha matumizi ya bangi zinafanana pia na kauli kama hizo zilizowahi kutolewa na baadhi ya wanasiasa. Kwa mfano, mwaka 2013 mbunge Ally Kessy (CCM – Nkasi Kaskazini ) aliibua hoja bungeni akiomba serikali kuhamasisha ulimaji wa bangi kama inavyohamasisha tumbaku, kwa kuwa ‘mazao’ yote mawili ni ‘yenye tija’, na aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo wakati huo Adam Malima, akamjibu kuwa utakapofika muda muwafaka serikali itafanya hivyo.

Aidha, nae mbunge Joseph Msukuma (CCM – Geita MP) mwaka 2017 aliwahi kuitaka serikali ihalalishe bangi, akitilia mkazo hoja yake kwamba kuna wabunge wengi tu wanaovuta bangi ilhali wanabeba ipasavyo majukumu yao ya kila siku.

Maumbile ya demokrasia ni nidhamu chafu, iliyokosa haya na yenye migongano, kiasi cha wafuasi wake kuthubutu kutoa kauli au kutenda hata mambo ya kuleta migongano huku wakiwa hawajali juu ya matokeo yake.
Kauli zote mbili za raisi ile ya Njombe na Mbeya zimetolewa katika mikutano ya hadhara, tena ikiwa mubashara katika Tv. ya umma, hapana shaka yoyote lazima kauli hizo zina madhara makubwa katika kuhamasisha uvutaji bangi na matumizi ya madawa ya kulevya kiujumla, hususan kwa vijana ambao ndio rasilmali nyeti kwa ustawi wa kila taifa.

Bila ya kusahau juu ya mgongano unaojitokeza kutokana na kauli hizo, ambapo upande mmoja kuna kampeni ya kupambana na madawa ya kulevya , na upande wa pili kunahamaishwa matumizi yake.

Suala hili pia linadhihirisha namna ndani ya demokrasia, licha ya sheria zitokanazo na binadamu kuchukuliwa ndio kigezo na suluhisho la kisheria, bado wafuasi wake hawaziheshiu wala kuzikinai. Uvutaji bangi ni kosa la jinai Tanzania, basi iweje lihamasishwe, tena uhamasishaji wa hadharani?

Suala la undumilakuwili na kukosekana taasisi thabiti ya kumuhisabu mtawala ni mambo pia yanayoonekana katika qadhia hii, wakati raia wa kawaida kila siku wanapelekwa mchamchaka na vyombo vya dola kwa kisingizio cha kukashifu serikali, lakini hatuoni uwajibishaji kufuatia kauli hizi ambazo zina matokeo mabaya katika jamii.

Mfumo wa Kiislamu sio kama nidhamu ya demokrasia, una sheria imara, zisizobadilika ambazo kila mmoja anawajibika kuzifuata bila ya kuzingatia cheo, nafasi au hadhi yake. Endapo mtu akatoa kauli au kutenda kinyume nazo, huwajibishwa kama inavyostahilki. Mfano mzuri ni kauli ya Mtume SAAW, alipotakiwa awe mpole kwa muhalifu wa wizi, aliyestahiki kukatwa mkono, akatoa majibu Mtume SAAW kwamba:
“Hata angekuwa Fatma bint Muhammad (binti yake ) angemkata mkono”

Zaidi ya hayo kuhusiana na wasimamizi wa masuala ya kiserikali, Dola ya Khilafah huweka mahkama maalumu kuwadhibiti, ambayo kazi yake kubwa ni kuchunga kauli na matendo ya watawala na watumishi wa Umma kwa jumla, pia kuwafuatilia kwa makini kwamba hawatumii madaraka yao vibaya.

Risala ya Wiki No. 39
24 Sha’aban 1440 Hijri /30 Aprili 2019 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
https://hizb.or.tz/
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.