Alhamdulillah! Hatimaye Wanachama Wetu Watatu Waachiwa Huru
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
بسم الله الرحمن الرحيم
Hatimaye wanachama watatu wa Hizb ut Tahrir Tanzania, Ust. Ramadhan Moshi Kakoso (45), Waziri Mkaliaganda (37) na Omar Salum Bumbo(55) waliotekwa na kubambikiwa kesi ya ugaidi na kuwekwa kizuizini kwa miaka minne na nusu wameachiwa huru siku ya Jumatano tarehe 23 Februari,2022.
Siku rasmi ya kuachiwa kwao ilikuwa iwe tarehe 22 Februari,2022 lakini kutokana na masharti yenye taklifu yaliyojitokeza yalipelekea kuchelewa kwa siku moja zaidi.
Katika kipindi chote walichokuwa kizuizini hawakupewa dhamana wala kesi yao kusikilizwa kwa kisingizio cha ‘upelelezi unaendelea’ na zaidi walinyimwa haki zao msingi kama kutembelewa na ndugu na kunyimwa nafasi ya kupelekewa chakula bora cha nje ya mahabusu.
Kuachiliwa kwao huru kumekuja baada ya miaka mingi ya kuwa kizuizini bila kesi yao kusikilizwa ambapo hatimaye Upande wa Mashtaka (DPP) umekiri kuwa hawana ushahidi wowote wa kuendelea na mashtaka husika dhidi yao
Hizb ut Tahrir Tanzania, Waislamu kiujumla na wapenda haki wote wamefurahia kuachiwa huru ( watatu hao) na kurudi kwa familia zao zilizokuwa zinawasubiri kwa hamu.
Katika hali hiyo, tunapenda kuwashukuru kwa dhati wote waliochangia na kushiriki katika kampeni rasmi na zisizo rasmi zilizopelekea kurejeshewa uhuru wao, shukrani hizi zikijumuisha baadhi ya Wanachuoni wa Kiislamu, Maustadhi, Maimamu wa misikiti na Waislamu kiujumla kwa dua zao na uungaji mkono wao. Pia tunashukuru baadhi ya vyombo vya habari, wanaharakati, wanasheria,wanasiasa nk. kwa kupaza sauti zao, rai na ushauri.
Tunasisitiza zaidi kuwa, kuachiwa huru kwa wanachama wetu watatu na kushindwa Upande wa Mashtaka kuleta ushahidi dhidi yao baada ya miaka minne na nusu ya kinachoitwa “uchunguzi” inaonesha wazi kuwa watatu hao hawana hatia kama ambavyo tumekuwa tukilisema hilo muda wote, kuwa watatu hao ni watu wanaojulikana kuwa wapenda amani na wanafamilia wanaojihusisha na Hizb ut Tahrir ambayo imeshikamana na njia isiyobadilika nay a wazi ya kuleta mabadiliko (ya Kiislamu) katika jamii iliyofuatwa na Mtume Muhammad (saw), inayojifunga kikamilifu na harakati zake kifikra na kisiasa tu bila ya kutumia nguvu au silaha.
Pia tunataka haki itendeke kwa wote waliowekwa kizuizini kwa dhulma, wawe Waislamu na wasiokuwa Waislamu, wapewe dhamana haraka iwezekanavyo au waachiwe huru.
Kwa kukhitimisha, tunarejea tena, hali ya kunajisi haki katika mfumo wa kikoloni wa kibepari ni tabia yake ya kimaumbile. Kwa hakika ni katika sharia za wahyi na chini ya kivuli cha dola ya Kiislamu ya Khilafah pekee kwa manhaj ya Utume ndipo uadilifu utakaposimama na kuangazia watu wote bila ya kuzingatia dini zao, rangi, matabaka, jinsia, kabila nk.
Na kauli yetu ya mwisho tunasema Alhamdullilah. Sifa zote njema na Shukran zote njema zinamstahikia Yeye Allah SWT.
Masoud Msellem
Mwakilishi kwa Vyombo vya
Hizb ut Tahrir
KUMB: 1443 / 04 Jumamosi, 25 Rajab 1443 H | 26/02/2022 M |
Maoni hayajaruhusiwa.