Tanzania Na Vurugu Baada Ya Uchaguzi Wa 2025
بسم الله الرحمن الرحيم
Habari:
Jumatatu, 03/11/2025, Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha pili. Uchaguzi ulioambatana vurugu kuanzia 29 Oktoba 2025 zilizosababisha hasara kubwa kwa maisha, mali na miundombinu ya Umma. (DW).
Maoni:
Hii si mara ya kwanza Tanzania kupitia vurugu za uchaguzi tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995. Ghasia zimekuwa sehemu ya kila uchaguzi mkuu, miongoni mwa vurugu mbaya zaidi ilikuwa mwaka 2000 visiwani Zanzibar ambapo watu 35 waliuawa, 600 kujeruhiwa na takriban 2000 kuomba hifadhi nchini Kenya (Human Rights Watch)
Vurugu katika chaguzi za kidemokrasia ni matukio ya kawaida duniani kote. Kwa mfano, kuanzia Disemba 2007 hadi Februari 2008 nchini Kenya watu zaidi ya 1,200 waliuawa na kiasi cha watu 350,000 walilazimika kuachwa bila makazi, Côte d’Ivoire mwaka 2010 ambapo watu takriban 3,000 waliuawa, Senegal mwaka 2012 ambapo watu 15 au zaidi walifariki na vurugu za Msumbiji za mwaka 2024 ambapo zaidi ya watu 50 wameuawa. Hiyo ni mifano michache tu.
Ripoti za kilimwengu zinakadiria kwamba vurugu za uchaguzi hutokea kwa takriban asilimia 19 ya nchi duniani, na katika asilimia 58 ya chaguzi za barani Afrika. Tumeshuhudia jambo hili hata katika nchi zinazochukuliwa kama vinara wa demokrasia kama Marekani katika uchaguzi wa mwaka 2020, baada ya kushindwa Trump kwa mara ya kwanza, mwaka uliofuata mnamo Januari 6, wafuasi wake walifanya vurugu na kuleta machafuko katika jengo la Bunge la Congress (Capitol Hill) na kusababisha vifo kadhaa.
Chanzo kikuu cha vurugu katika chaguzi wa kidemokrasia, ambayo ndio nidhamu ya kisiasa ya mfumo wa kibepari, hutokana na asili na maumbile ya mfumo huo ulivyo.
Mfumo wa kibepari ulichipuka kutokana na usekula, itikadi dhaifu, tete, isiyoingia akilini na isiyokuwa na thamani ya kiroho (kidini), ikilenga juu ya kitu kimoja tu, nacho ni ‘maslahi’ kuwa ndio kipimo cha matendo yote. Katika hali kama hii vurugu ni jambo lazima kutokea, kwani waumini wa demokrasia wako tayari kufanya lolote kwa ajili ya kuyafikia maslahi.
Bila ya kusahau kwamba mfumo wa kibepari unashikilia fikra za Machiavelli za kutumia njia yoyote kama vile kusema uongo, kuua, kuleta mifarakano baina ya watu, kuharibu mali za Umma na mali binafsi nk. ili kufikia malengo yanayohitajika.
Aidha, mataifa ya Magharibi yaliyoleta demokrasia ya vyama vingi walilenga kuwadanganya watu kwa kuwaonyesha kwamba mfumo huo (wa vyama vingi) ni ‘ukombozi wa pili’ ilhali ni uwongo wa wazi wazi kabisa.
Kauli mbiu ya uongo ya ‘ukombozi wa pili’ kupitia demokrasia ya vyama vingi inafanana na kaulimbiu ya awali ya ‘uhuru’. Zote zililenga kuwalaghai watu hasa wa mataifa yanayoendelea na kuwaondoa katika jambo msingi la kupigania suluhisho la kweli na la kimsingi la kung’oa mfumo wa kibepari, ambao ndio chanzo cha maangamizi yote katika mataifa yote.
Amma kauli mbiu ya ‘Uhuru’ katika miaka ya 1950-60 ililenga kubadilisha mtindo wa ukoloni mkongwe kwa ukoloni mpya (ukoloni mamboleo) kupitia mawakala wa ndani kwa jina la kutoa uhuru.
Baada ya miaka ya uhuru wa bendera, watu waling’amua kuwa hakukuwa na mabadiliko kama walivyotarajia, na walichoshwa na watawala wakala wa magharibi makatili waliokuwa wakitawala kupitia mfumo wa chama kimoja, mataifa ya Magharibi kwa hila walileta demokrasia ya vyama vingi ili kuwapozapoza watu. Katika demokrasia ya vyama vingi watu wamefinyangwa kuamini kwamba kubadilisha sura ya mtawala kutaleta mabadiliko kwenye nchi.
Vipi mabadiliko yatakuja bila mabadiliko msingi ya kimfumo kutoka kwenye mfumo wa ubepari ambao bado unadhibiti kila nyanja za nchi zinazoendelea, na kufanya kazi usiku na mchana kunyonya rasilimali zetu kwa njia yoyote hata kusababisha ugomvi baina ya raia, mgawanyiko, vita ili kufikia tu ajenda yao ya kikoloni. Kama tunayoyashuhudia nchini Kongo, Sudan, Msumbiji nk.
Zaidi ya hayo, vurugu baada ya uchaguzi nchini Tanzania na sehemu nyingine sio tu zinafedhehi demokrasia kama mfumo wa vurugu na machafuko, bali pia zinafunua uwongo wa propaganda ya Magharibi ya vita dhidi ya ugaidi ambayo imekua ikilenga kwa chuki Waislamu na Uislamu ulimwenguni kote, kwamba wana vurugu, ilhali tunaona wafuasi wa demokrasia na wanaharakati wake bila ya aibu wakiunga mkono wazi wazi vurugu, na wengine kushiriki kwenye vurugu hizo za kishenzi.
Kwa kukhitimisha, Tanzania, mataifa yanayoendelea, na ubinadamu kwa ujumla hawatapata amani na utulivu kamwe chini ya mfumo batili wa kidemokrasia. Badala yake ubinadamu unahitaji mabadiliko msingi yanayotokamana na mfumo wa Uislamu ambao imeutawala ulimwengu kwa makarne kwa haki na uadilifu kwa watu wote bila ya ubaguzi.
Imeandikwa na Said Bitomwa
Mwanachama wa Afisi ya 𝐇𝐢𝐳𝐛 𝐮𝐭 𝐓𝐚𝐡𝐫𝐢𝐫 𝐓𝐚𝐧𝐳𝐚𝐧𝐢𝐚
Kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir
Maoni hayajaruhusiwa.