Demokrasia Haijali Maisha Wala Mali Ya Yoyote

بسم الله الرحمن الرحيم

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Kwa mara nyengine tena Tanzania imekumbwa na vurugu za baada ya uchaguzi kwa siku kadhaa tangu Oktoba 29, 2025 na kusababisha kupotea kwa maisha ya wengi na uharibifu mkubwa kwa mali binafsi na miundombinu ya Umma.
Tangu uchaguzi wa kwanza wa rais wa vyama vingi uliofanyika Tanzania mwaka 1995, suala la vurugu baada ya uchaguzi limekuwa ni suala la mara kwa mara na la kudumu kila baada ya miaka mitano. Hata hivyo, vurugu za mwaka huu ni kubwa na kusambaa hata kuliko zile vurugu mbaya za mwaka 2000, ambapo zaidi ya wafuasi 40 wa upinzani (CUF) Zanzibar waliuwawa kwa kupigwa risasi, kupatikana majeruhi zaidi ya 600, na takriban watu 2,000 walikimbia kutaka hifadhi nchi ya jirani ya Kenya.
Vurugu ni jambo la kimaumbile na lipo ndani ya msingi wa demokrasia na chaguzi zake, kwa namna ifuatayo:
1. Demokrasia ambayo ni nidhamu ya kisiasa ya mfumo wa kibepari imejengwa juu ya kipimo kimoja tu matendo yake, nacho kipimo hicho ni ‘maslahi’ . Hivyo, mtu hutenda au kujizuiya kutenda ili apate maslahi yake. Si jambo la kushangaza kwa mfuasi wa demokrasia iwe serikali au upinzani kutenda au kuhamasisha wengine kutenda ili kufikia ambayo maslahi yao. Kwa msingi huu, vyama vyote vya kidemokrasia havipo kutumikia ustawi wa watu, bali ni njia ya kiuchumi kwa wanasiasa, iwe kwa kupata ruzuku ambazo ni mali ya na Umma, kutarajia uteuzi, kutumia misaada kutoka kwa wakoloni, kutafuna michango kutoka kwa wafadhili, nk.
2. Mfumo wa kidemokrasia unashikilia fikra batil na za kishetani za Machiavelli, ambapo fikra hizo huhubiri: ‘Njia huhalalisha lengo na lengo huhalalisha njia’’. Hii ina maana kwamba katika demokrasia, kila kitu kinaweza kufanywa, kama vile kuua, kuchochea mgawanyiko kwa msingi wa mihemuko ya kidini na kibaguzi wa kimaeneo, uongo au kitu kingine chochote bila kujali madhara yake, kwa sharti tu malengo kusudiwa yanafikiwa. Kimsingi, katika demokrasia, hawazingatii dhana ya halali kisheria au kutofaa kisheria. Kilicho muhimu kwao ni chochote kinachopelekea kufikia malengo yao.
3. Demokrasia ya vyama vingi ililetwa na wamagharibi kwa maslahi yao wenyewe, na si kwa maslahi wala maendeleo ya nchi zetu kama ilivyodhaniwa na wengi kwa kiwango kwamba baadhi ya watu kuchanganyikiwa kwa matumaini makubwa, wakipoteza muda mwingi, kuvuja majasho, wengine hata kupoteza maisha kwa kutarajia mabadiliko. Badala yake (demokrasia ya vyama vingi) ililetwa na wamagharibi kama mtego na udanganyifu kwa kubadilishabadilisha sura ya utawala. Kwa sababu ( wamagharibi) waligundua kwamba watu wamechoshwa na kulikuwa na malalamiko yanayoongezeka kutokana na ukatili wa mfumo wa chama kimoja uliolindwa nao (wamagharibi). Iliingizwa (sera ya vyama vingi) kama mbinu nyingine ya kuimarisha ukoloni mamboleo na kuwaondosha watu kuyaona mambo katika mtazamo mpana wa kimfumo. Ikawa sasa, watu badala ya kupambana kuondoa mfumo mbaya wa kibepari, wakawa wanatumia nishati zao katika suluhisho la uwongo la kubadilishabadilisha sura za watawala.
Zaidi ya hayo, kwa mifano mingi kupita ( sera ya vyama vingi) na visingizio vyengine mataifa ya Magharibi yanachochea mizozo ya kiraia na vurugu ili kufanikisha ujanja na unyonyaji wao wa rasilimali ( nchi changa). Mifano hai ni kama: Sudan, Kongo, Yemen, Somalia nk.
Ni dhahiri kuwa mfumo kama huo (wa ubepari) hauwezi kuepuka migogoro isiyokwisha, magomvi na vurugu zisizoisha, dhaifu. Lakini kubwa zaidi, mfumo huo haona uwezo na sifa ya kumtumikia binadamu kwa haki.
Muda umewadia kwa kila mtu makini, mwenye fikra makini na mwenye shauku ya kutaka kuleta mabadiliko ya kweli kujizuiya kushiriki au kuunga mkono mihemuko batil ya kidemokrasia. Kwa Waislamu, wajifunge na wajibu wa kufuata njia sahihi ya Kiislamu ya kuletea mabadiliko kama ilivyofundishwa na Mtume (SAAW ) ili kurejesha tena Dola ya Kiislamu ya Khilafah inayopaswa kuanzia katika ulimwengu wa Kiislamu.
Amma kwa wasio Waislamu, muda umewadia kwao kutafakari juu ya mfumo mbadala wa Kiislamu na njia yake ya mabadiliko, kisha kuukubali na kujitenga na ufisadi na udanganyifu wa kidemokrasia.
Masoud Msellem
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari
Kumb: 1447 / 03
14 Novemba 2025 M. / 23 Jumada I 1447 H.

Maoni hayajaruhusiwa.