Harakati Za Uhuru Zilikua Hadaa Tu Kwa Umma

بسم الله الرحمن الرحيم

Habari:
Tarehe 14 Oktoba ni siku rasmi ya Mapumziko nchini Tanzania ambayo kila mwaka hukumbukwa kifo cha Julius Nyerere, “baba wa taifa” aliyekufa London mwaka 1999.
Maoni:
Siku hii hupewa muhimu mkubwa sana nchini Tanzania, kwani inaadhimisha maisha na urathi wa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaechukuliwa kama kiongozi bora aliyebeba jukumu muhimu kama mpigania uhuru na aliyebuni nadharia ya kisiasa iliyoboresha mustakabali wa nchi.
Ingawaje Nyerere alitawala kwa mabavu kwa miaka 24 tangu uhuru wa bendera mwishoni mwa 1961 hadi alipostaafu mwishoni mwa 1985, kama wengine wengi wanaoitwa wapigania uhuru, anatukuzwa sana, na kupewa hadhi ya juu katika kiwango tofauti na uhalisia wa mambo.
Picha halisi ya wanaoitwa wapigania uhuru kama Nyerere, ambaye alikuwa mstari wa mbele kuupambania ‘uhuru wa bendera’ inaweza kueleweka vizuri zaidi ikifungamanishwa na muktadha wa kimataifa wa wakati huo.
Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, nafasi za mabwana wakoloni wakongwe, yaani Uingereza na Ufaransa, iliyumba kimataifa. Badala yake, Marekani iliibuka kuondosha na kupinga ushawishi wa mataifa hayo mawili ya kikoloni kimataifa. Licha ya (Marekani na mabwana hao wawili) wote kubeba mfumo mmoja wa kibepari, lakini mataifa hayo yanatofautiana katika maslahi yao ya kitaifa.
Uingereza iliweka mikakati kadhaa kujilinda na hali hiyo ili kudumisha mamlaka na ushawishi wake uliokuwa unafifia katika makoloni yake. Ilichukuwa hatua kama vile kuimarisha jumuiya yake ya Madola (Commonwealth), kutanua kwa uimara mkubwa mtandao wake wa elimu katika shule na vyuo vikuu na kutumia taasisi hizo kufinyanga vibaraka waaminifu iliyo walenga kuwapatiwa uhuru bandia ‘wa bendera’ ili kukabiliana na wimbi la upinzani la kimataifa linaloongozwa na Marekani na kuendelea kuhifadhi ushawishi wake.
Mabingwa wa Uingereza katika tasnia ya elimu katika makoloni ya Uingereza kama Lord Cromer aliyekuwa Misri na Lord Macaulay wa India walifafanua wazi kuwa, lengo la mfumo wa elimu wa Uingereza lilikuwa ni kuendelea kuwabakisha wenyeji wa makoloni yao na sura zao tu, lakini kuwabadilisha tabia na mienendo yao kulingana na tamaduni, sera na mitazamo ya Kiingereza.
Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda katika Afrika Mashariki ilikuwa mojawapo ya mifano mingi iliyochangia katika mkakati huu wa Kiingereza. Ni dhahiri, Nyerere alikuwa mmoja kati ya wale waliopitia mafunzo hayo Makerere, kisha kupata elimu zaidi na kupigwa msasa zaidi huko Edinburgh (Uingereza).
Nyerere alijitolea na kuwa mfuasi thabiti wa Uingereza, kiasi kwamba hata wakati jaribio la kutaka kupinduliwa lilipojitokeza katika miaka ya sitini, Uingereza kwa haraka sana ilikuja kumuokoa ‘kijana wao’.
Aidha, Nyerere alipewa jukumu na Uingereza kwenda Zanzibar haraka ili kurahisisha muungano wa vyama vilivyokuwa vikiitwa vya Kiafrika na Shirazi, na hivyo kuzaliwa Chama cha Afro Shirazi, kilichokuwa kikifanya kazi nyuma ya pazia la Uingereza.
Chini ya mwongozo wa Nyerere, Chama cha Afro-Shirazi kilifanikiwa kuipindua serikali ya Zanzibar, kisha kwa haraka kikaleta Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar kufuatana na maelekezo ya Uingereza.
Bila kusahau jinsi chama hicho ( Afro-Shirazi) kilivyotumiwa kupandikiza chuki na kuendeleza mizozo ya kibaguzi na kupelekea vurugu baina ya Waislamu wa Zanzibar na Umma kwa ujumla.
Kuhusu Tanganyika, Nyerere atakumbukwa jinsi alivyowatenga Waislamu, kuvuruga umoja wao, kuvunja taasisi zao, kuwapuuzilia mbali, licha ya mapokezi mazuri na mwanana waliyompa, heshima kubwa waliyomuonesha, kumtumikia, na kushikana naye bega kwa bega katika harakati za uhuru.
Nyerere aliacha nchi chini ya mamlaka ya Uingereza yaliyofichwa nyuma ya uhuru bandia, aliwapa waingereza kila fursa ya kutumia rasilimali za nchi, huku raia wa kawaida, hasa Waislamu na wasio Waislamu wakipambana na taabu na kutokujua mustakabali wao kimaisha.
Hivi ndivyo, kauli mbiu za ‘uhuru’ na ‘ukombozi’ zilivyotumiwa kuhadaa watu, na Umma ukatengenezewa mashujaa bandia, ambao kwa kweli walikuwa wakala wa wakoloni.
Ukombozi na mashujaa wa kweli watapatikana pale tu Itikadi ya Kiislamu itakaposhika hatamu chini ya Dola yake ya uadilifu ya Khilafah.
Imeandikwa na Said Bitomwa
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir
Kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Maoni hayajaruhusiwa.