Nasaha za Ikhlasi Kwa Wanaounga Mkono na Wasiounga Mkono Maulidi
بسم الله الرحمن الرحيم
Tukiwa katika mwezi wa Rabi ul Awal (Mfunguo sita) aliozaliwa Mtume wetu mtukufu (SAAW). Hapana shaka sote twajua uwepo wa mizozo na mivutano isiyo yalazima baina ya baadhi Waislamu kuhusu sherehe ya Maulidi.
Si lengo la maandishi haya kuonesha nani yupo sahihi na nani hayupo sahihi kuhusu suala la maulidi baina ya pande mbili. Sababu ni kwamba hili ni jambo lenye kukubali ikhtilafu, hivyo, tutawaachia watu na misimamo yao.
Sababu za ikhtilafu ni kuwepo tofauti katika uwezo wa kufahamu nususi za kisheria na ni jambo lipo na pia limedokezewa katika Quran Tukufu:
هُوَ الَّذِي أَنزَلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ مِنْهُ آيَاتٌ مُّحْكَمَاتٌ هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ وَأُخَرُ مُتَشَابِهَاتٌ ۖ
“Yeye Peke Yake Ndiye Ambaye Aliyekuteremshia Qur’ani ambayo katika hiyo kuna aya zenye maana yaliyo wazi; hizo ndizo msingi wa Kitabu (ambao unategemewa ikitokea chochote kinachohalifiana nao kinarudishwa na kuoanishwa nazo.)
Na katika hiyo (Quran) kuna aya zingine mutashãbihãt: (zinazoleta na kubeba zaidi ya maana moja (haiwezekani kujua maana iliyokusudiwa, isipokuwa kwa kuziambatanisha na muḥkam:) ( Surat Imran: 7)
Hivyo, kudai kwaamba hakuna ikhitilafu katika jambo la mawlid ni kuleta ikhtilafu kubwa kuliko hiyo inayopingwa.
Jambo la kusikitisha katika qadhia ya ikhtilafu ni uwepo wa matumizi mabaya ya ikhtilafu, imma kwa nia mbaya au kwa bahati mbaya. Kama vile kuzuwa vurugu baina ya Umma kwa jambo lenye kukubali ikhitilafu, au kuingiza kwenye ikhtilafu mambo ambayo hayakubali ikhtilafu kwa kutumia mlango wa uwepo wa ikhtilafu.
Lengo la makala hii ni kuonesha namna sherehe za mazazi ya Mtume SAAW yanavyobebwa vibaya kwa pande zote mbili, wanaounga mkono na wanaopinga:
1. Kwa Wanaounga mkono sherehe za mazazi ya Mtume SAAW:
a.Kutanguliza mambo ya mubaha kuliko ya wajibu. Mfano, kutokusanya nguvu na mali kwa ajili walimu wa madrasa na kuboresha madrasa lakini kutumia nguvu kubwa na mali nyingi kwenye sherehe za maulidi.
Kwani uwezekano wa kufanya sherehe isiyo na gharama kubwa tena ya muda mfupi ni jambo linawezekana, kama kutoandaa chakula nk. na huenda wakapata picha halisi ya wanaohudhuria kwa mapenzi ya Mtume SAAW na wanaohudhuria kwa sababu zao.
b. Baadhi ya sherehe hizo za maulid kutojali ratiba za swala na ibada nyengine. Hili ndio jambo baya zaidi, vipi tumo katika kumsifia Mtume SAAW kuchukue nafasi, kuliko kutekeleza maagizo aliyokuja nayo Mtume SAAW ?
c. Jukwaa la mazazi ya Mtume SAAW aliyekuja kupambana na ukafiri kutumiwa kukuza agenda za kikafiri kama vyama vya siasa vya kikafiri vinavyotangaza wazi kwamba itikadi yake ni kutomtambua Allah Taala katika nyanja za maisha, yaani wanakusudia haki na milki ya Allah Taala ni ndani ya kuta nne za majengo ya ibada tu.
Hakika hii ni aibu sana na ni kesi kubwa Siku ya Qiyama kutumika jukwaa la Mtume SAAW kwa matumizi dhidi ya Mtume SAAW.
Katika watu waliomtesa Mtume SAAW ndani ya Makka ni akina Abuu Jahali ambao nao walikuwa na itikadi inayofanana na leo kwamba Mungu Muumba asihusike katika maisha yao ya siasa, uchumi, utawala, jamii, adhabu za wahalifu, haki na wajibu nk.
Basi vipi watu walioshikilia itikadi ya Abuu Jahali ima kwa kujua au kutojua (kwani baadhi yao bado ni Waislamu na sio kwamba wameritadi) wapewe nafasi ya kunadi sera zao katika jukwaa la Mtume SAAW au kuombewa dua waweze kuendeleza mifumo yao isiyo na dini ?
d.Majukwaa kama haya ya maulidi yanafuatiliwa na Umma wa Kiislamu na kuyategea masikio, basi katika majukwaa kama haya kutozungumzwa mada zenye kuhuisha fikra, ari, na hamu kwa Umma wa Kiislamu kuwa pamoja pasina kujali ikhtiafu zetu za rangi, kabila, madhihab, au hii mipaka bandia iliyochorwa na wakoloni, ni matumizi mabaya ya majukwaa hayo ya mwezi kama huu wa mazazi ya Mtume SAAW.
Kwa bahati mbaya sherehe na majukwaa haya kuanzia mara nyingi mwanzo mpaka mwisho hakuna hata dua ya kuwaombea Waislamu wanaodhulumiwa kama mauaji ya mayahudi ndani ya Gaza, Kashmiri, Burma, Turkistan Mashariki nk. Lakini badala yake utasikia dua za kuwaaombea wanasiasa ambao hawana haja na dua hizo bali ni kujipendekeza tu, kwani karibu kila mwanasiasa ana mganga wake, je mwenye mganga ana haja na dua? Na vipi mtu anaombewa dua apate kendeleza maasi? Kwani siasa na hukmu zisizokuwa za Kiislamu ni maasi ya wazi, na hili halina ikhtilafu kwa wasomi wote wa Kiislamu.
e. Majukwaa haya ya mazazi ya Mtume SAAW hutumika kurusha vijembe kwa makundi yenye kupinga sherehe hizi kuliko kuelimisha Umma, kwani wapingao sherehe hizi hoja zao zinajulikana, na tayari zimeshapingwa. Na pia waungaji mkono sherehe za maulidi na wao hoja zao zinajuulikana. Sasa kwanini kusitumike majukwaa haya kuamsha Umma badala ya mivutano?
f. Ukweli halisi wa faida ya kumbukumbu ya uzawa wa Mtume SAAW haufafanuliwi vizuri na kwa kina. Bali kinachodhihirika ni kusemwa kipande, na kipande kufichwa au kuachwa kwa bahati mbaya. Bali ukweli hasa uzawa wa Mtume SAAW ilikuwa ni kuchomoza nuru mpya ya mfumo wa Uislamu, dini iliyokusanya roho na siasa. Yaani ni ujio wa mfumo wa maisha wenye nidhamu ya utawala, siasa, uchumi, jamii nk.
Na hii ndio sababu ya uadui wa Makuraishi kwa Mtume SAAW na masahaba wake.
Na lau Uislamu ungekuwa dini ya kiroho tu kama vile unavyohubiriwa na baadhi leo basi wakina Abuu Jahali na wenzake wasingekuwa na sababu ya kupambana na Uislamu, kwani Mtume SAAW hakuwahi kattu kuabudu masanamu na makuraishi hawakumfanyia uadui kwa hilo. Hii ikiwa ni dhahiri uadui wao uliibuka katika muktadhaa wa kupingwa sera zao za kisiasa, uchumi, utawala nk.
2. Kwa Wanaopinga sherehe za mazazi ya Mtume SAAW
a.Amma wapingao maulidi nao wanaangukia mule mule katika makosa ya kukaza misuli katika mambo yenye ikhtilafu ki-sheria na kulegeza misuli katika mambo ambayo uwajibu wake hauna ikhtilafu.
Mfano, yupi awezaye kusema kulingania Uislamu kama mfumo wa maisha sio wajibu? Bali utawaona kundi hili wao wamechagua Sunna mbili tatu na kuzifanya ndio bakora ya kuwachapia Waislamu ambao hawajajifunga na Sunna hizo, ilhali Waislamu wengine nao wamejifunga na Sunna zingine.
b.Kuona uharamu wa sherehe za maulidi ni dhambi kubwa kuliko Umma wa Kiislamu ulivyowatupa mkono Waislamu wa Palestina, Yemen, Sudan, Kashmiri nk. japo hata kwa dua. Huku kundi hili lipingalo maulidi wakitetea watawala wa nchi za Kiislamu kwa kutopeleka majeshi yao kunusuru Waislamu, bali hata maswaibu yanayowagusa Waislamu wa maeneo yetu ya karibu, wao hawana uchungu nayo labda yakigusa wafuasi wao.
c. Kukataa kwamba jambo hili halina ikhtilafu, kwa hoja kuwa Mtume SAAW hakufanya, huku na wao wakifanya ambayo Mtume SAAW hakufanya kama sherehe za tahfidhi Quran nk.
d. Kuunga kwao mkono tawala ambazo zinagongana na aqida ya Kiislamu na wakihimiza zipendwe zitiiwe na zienziwe, ihali aqida waliyoibeba ya Kiislamu inakataa misimamo hiyo. Kwani aqida ya Kiislamu haiwezi kuunga mkono itikadi inayosema Allah Taala hana nafasi katika maisha ya siasa, utawala, uchumi, jamii nk.
Ni matarajio makubwa kwamba Umma wa Kiislamu utazibeba nasaha hizi kwa ikhlasi na uchamungu na kuzifanyia kazi, ambapo kazi kubwa, ya wajibu na nyeti inayotukabili kufanya ulinganizi wa kurejesha tena maisha ya Kiislamu kwa kurejesha dola ya Kiislamu ya Khilafah.
Sheikh Ramadhan Moshi
Risala ya Wiki No. 219
10 Rabi’ al-awwal 1447 Hijri/ 2 Septemba 2025 Miladi
Afisi Ya Habari – Hizb Ut Tahrir Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.