Mwito Kwa Waislamu Kusimama Kidete Kulinda Aqidah ya Kiislamu
بسم الله الرحمن الرحيم
Wakati wanaharakati wa Hizb ut Tahrir Tanzania tukiwa katika kumi la mwisho la kampeni ya miezi miwili (Muharram- Safar 1447 H) ya kulinda na kutetea aqidah ya Kiislamu dhidi ya fikra za ‘Dini mseto’ Upagani au Dini za mababu nk. Fikra chafu, batil zinazotokana na ajenda ya kikafiri. Ni wajibu Waislamu hususan wadau wanaouhudumia Uislamu kushiriki kikamilifu katika mchakato huu kwa kutumia mbinu zote ambazo ni halali kwa mujibu wa sheria za Kiislamu.
Na ni kosa kubwa na dhimma nzito mbele ya Allah SWT kunyamazia uvamizi dhidi ya suala nyeti la aqidah ya Kiislamu. Basi jee huwa dhimma kubwa kiasi gani ikiwa Muislamu ni mshiriki katika kukuza moja ya fikra hizo?
Umma wa Kiislamu ukumbuke kwamba vita baina ya haki na batil ni jambo endelevu kinachobadilika ni mbinu na mipango ya makafiri kwa mujibu wa zama, muda, eneo nk. Kama Allah Taala alivyotaja ndani ya Quran Tukufu:
بل نقذف بالحق على الباطل فيدمغه فإذا هو زاهق
Bali tunailembea haki kwenye batili na ikaiangamiza na tahamaki ikaipoteza”
Kwa hivyo, jukumu la kubomoa na kupambana na batil linaangukia mabegani mwa waliobeba haki ambao ni Waislamu. Na wajibu zaidi huangukia mabegani kwa wasomi au wanaojishughulisha na kuhudumia Uislamu, kama taasisi za kidini nk.
Vita ya makafiri dhidi ya Uislamu haijawahi kusimama tangu zama za Mtume SAAW na baada yake, na vitaendelea mpaka Siku ya Mwisho
Ndani ya Makka Makuraishi walisimama kidete kuzuiya Uislamu usichipuke kisha kutaka kuzuiya dola ya Kiislamu isisimame. Mbinu yao ya awali ilikuwa kudharau, kisha propaganda, mateso kwa Waislamu nk.
Kwa upande wa Madina, mayahudi, wanafiki, waarabu na washirikina walisimama kidete kutaka kung’oa dola ya Kiislamu na kuzuiya kupanuka kwa Uislamu na dola ya Kiislamu. Walitumia mapambano ya kifikra, unafiki, fitna nk. Na walipo shindwa wakaungana na waraabu washirika katika vita. Mfano, Vita vya Ahzaab.
Aidha, katika zama za Khilafah Rashidah, vita ilikuwa kufarikisha Umma wa Kiislamu, kudhoofisha dola ya Kiislamu na kuiangusha. Maadui walikuwa ni wanafiki wapya waliosilimu kinafiki kutoka miji nje ya Bara Arabu. Walichofanikiwa tu ni kuuwa watawala watatu wa Kiislamu Omar, Othman na Ally (ra).
Kisha zama za Ummawiya na Abassiya, vita dhidi ya Uislamu ilikuwa ni kuharibu fikra na fahamu sahihi za Kiislamu kwa kutunga Hadithi za uongo na kuzua mijadala kwamba aya za Quran zinagongana nk. Na maadui walikuwa mazandiki.
Baadae zikafutia na zama za uadui wa Vita vya Msalaba na Wamongoli. Wao lengo lao ilikuwa ni kuangusha dola ya Kiislamu na kuwafukuza kabisa Waislamu katika miji yote waliyoifungua. Na mbinu yao ilikuwa ni vita na uharibifu. Hali ikaendelea hivyo mpaka kufikia zama za Khilafah Uthmaniya, na hasa karne ya 18 mpaka 19.
Mapambano ya makafiri katika karne 18 mpaka 19 yalikuwa na malengo kuangusha dola ya Kiislamu ya Khilafah na adui mkubwa alikuwa nchi za Ulaya hususan Uingereza. Na hatimaye wakafanikiwa kuiangusha Khilafah. Mbinu yao kubwa ilikuwa vita vya kifikra, kuendesha kampeni ya kushawishi kujitenga miji ya Kiislamu kunako Khilafah ya Uthmaniya, miito ya uzalendo na ubaguzi, kuunda vibaraka katika ardhi za Waislamu nk.
Vita vya makafiri bado vinaendelea ambapo katika karne ya 20, vimejikita na shabaha ya kuzuiya kurudi tena Uislamu kama nguvu ya kutawala dunia kwa kuharibu fikra sahihi za Kiislamu.
Kufikia lengo hilo makafiri wamepanga mambo mengi. Haya ni mfano tu:
1. Kuharibu na kuzikoroga fikra za Umma wa Kiislamu kama:
a. Fikra ya uzalendo ili kuzuiya umoja wa Umma
b. Fikra za kutenganisha dini na maisha, yaani kuutenga Uislamu na utawala
c. Kupiga vita Uislamu wa kisiasa na kuunga mkono Uislamu wa kiroho tu, yaani kuufanya Uislamu kama ukristo
d. Kuasisi harakati za kuungana na wanasiasa katika siasa zao za kidemokrasia.
e. Kuasisi harakati zenye kupambana na Waislamu tu, hasa Waislamu wenye mawazo ya kutaka kurudisha nguvu za Waislamu duniani.
2. Vita vinavyoitwa vya Ugaidi
a. Kuasisiwa kwa makundi ya kigaidi ili kuleta machafuko na kunasibishwa Uislamu na machafuko hayo.
b. Kutumika ugaidi kama bakora ya kufunga midomo Waislamu kuzungumza Uislamu kama mfumo wenye kukusanya roho na mada, imani na maisha, ibada na siasa nk. Hatimae Waislamu wamekuwa wahudumu wa siasa za kidemokrasia, kwani siasa ni maisha huwezi kuiepuka, ikiwa sio ya Kiislamu utashika isiyo ya Kiislamu.
c. Kufanywa ugaidi ni kibali cha kudhulumia Waislamu, yeyote awae, ana kosa au hana kosa, na wengine kuogopa kumtetea.
d. Kudhibitiwa kwa taasisi za Kiislamu, shule hata misikiti kwa kutumia ya tishio la ugaidi
e. Kuvunja ari ya vijana wa Kiislamu kuhudumia dini yao, na kuona afadhali kujiingiza kwenye mambo ya kipuuzi kama michezo, kamari nk.
Katika hali kama hii ni wajibu kwa kila Muislamu hususan wabeba da’awa kujifunga kibwebwe katika kulinda na kutetea aqidah ya Kiislamu, kwani kukaa kimya au kushughulika na mambo madogo madogo au mambo ya ikhtilafaat tu na hali Umma unapotezewa aqida yao ni dhimma kubwa sana Siku ya Qiyama.
Watumishi wa Uislamu na Waislamu jumla wasichoke kujadiliana na wafuasi wa fikra hizo za hatari kwa njia ya kistaarabu, hoja na busara.
Bali kubwa na nyeti zaidi kwa Waislamu ni kushiriki katika mchakato wa kurejesha tena dola ya Kiislamu ya Khilafah Rashidah ili ije kulinda kikweli aqida ya Kiislamu, na kuuokoa ubinadamu na dini na fikra za kuchanganyikiwa ambazo leo ubepari unazipigia debe na kuzidhamini.
Risala ya Wiki No. 217
19 Safar 1447 Hijri / 13 Agosti 2025 Miladi
Maoni hayajaruhusiwa.