Mgogoro Wa Ziwa Nyasa Kati Ya Malawi Na Tanzania Ni Dhihirisho La Ukoloni

بسم الله الرحمن الرحيم

Habari:
Hivi karibuni nchini Malawi kumeripuka wimbi kubwa la ukosoaji mkubwa wa ramani za Tanzania zinazoonesha kuwa mpaka kati ya Tanzania na Malawi ukiwa katikati ya Ziwa Malawi (Nyasa).
Maoni:
Sakata hili limeibuka kufuatia hatua ya wiki chache zilizopita za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya Tanzania kutoa agizo kwa walimu wote nchini Tanzania katika ramani zao kama nyenzo za kufundishia, watumie ramani zinazoonesha mpaka kati ya Tanzania na Malawi ukiwa katikati ya Ziwa Malawi (Nyasa), badala ya ramani ya awali inayoonesha ziwa lote kuwa ni mali ya Malawi kama inavyodaiwa na Malawi.
Ukoloni umeacha urithi mbaya wenye madhara makubwa kwa mataifa ya Afrika na kwingineko ulimwenguni yakiwafanya raia (wa nchi zilizokoloniwa) kukabiliana na migogoro mingi ya mipaka, na katika baadhi ya matukio kusababisha vurugu, vita na uharibifu mkubwa.
Afrika mashariki, kuna matukio kadhaa ya migogoro ya mipaka ikiwa ni pamoja na mgogoro kati ya Somalia na Ethiopia (unaoendelea tangu 1960), Kenya na Sudan Kusini(unaoendelea tangu 1963)na Kenya na Somalia(1963-1981). Migogoro mingine ni kati ya Ethiopia na Sudan (kuanzia 1966 hadi 2002), Tanzania na Malawi (unaoendelea tangu 1967) na Uganda na Tanzania (1974–1979) na kadhalika.
Kabla ya uvamizi wa wakoloni wagharibi na kugawanywa bara la Afrika miongoni mwao hapakuwa na mzozo wowote mkubwa kati ya sehemu hizi mbili (Tanzania na Malawi) au sehemu yoyote ya ziwa juu ya umiliki wake.
Wenyeji wa pande zote za ziwa walitumia pamoja rasilimali kutoka katika ziwa kwa amani, kila sehemu ilifurahia na kunufaika na matumizi yake kama uvuvi, umwagiliaji, matumizi ya maji nyumbani nk.
Kufuatia uvamizi wa wakoloni katika Afrika mwishoni mwa karne ya 19, Malawi ilinyakuliwa na Uingereza, ilhali Tanzania (Tanganyika) ikinyakuliwa na Ujerumani.
Wakoloni hao wawili walitia saini Mkataba wa Heligoland-Zanzibar wa mwaka 1890, ambapo mpaka kati ya koloni la Uingereza la Nyasaland (Malawi) na koloni la Ujerumani la Afrika Mashariki (Tanganyika) uliwekwa kwenye mwambao wa ziwa.
Kulingana na mkataba huo, ziwa lote likawa sehemu ya Malawi. Hivi ndivyo kwa mara ya kwanza ukoloni ulivyotengeneza tatizo hili au mgogoro huu.
Baada ya uhuru wa bendera ya nchi hizo mbili (Malawi na Tanzania) katika miaka ya 1960, wakoloni waliendeleza mgogoro kupitia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria ya Bahari wa mwaka 1982 ambao unatambua katikati ya ziwa (Nyasa) ndio mpaka kati ya Malawi na Tanzania.
Malawi ilipinga Mkataba huo wa Umoja wa Mataifa wa Sheria ya Bahari wa mwaka 1982 na Azimio la Cairo, na ilikataa kutambua kufutwa kwa Mkataba wa mwaka 1890 wa Heligoland-Zanzibar kati ya Uingereza na Ujerumani.
Kwa karne suala la kukosekana suluhu (la mogoro huu) limechochea mzozo kati ya pande hizi mbili (Malawi na Tanzania). Juhudi zote za kutatua migogoro huu zilizofanywa na waafrika wenyewe zilishindwa, kuanzia juhudi za makubaliano baina ya nchi hizi mbili, juhudi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na juhudi za Umoja wa Afrika (AU). Na kushindwa kwa (jumuiya hizo) kunaashiria kuwa Afrika bado ipo chini ya ukoloni mamboleo wa wamagharibi ambapo waafrika hawawezi hata kujiamulia mambo yao kama haya. Inabidi wategemee na kusubiri uamuzi kutoka kwa wakoloni wa magharibi.
Inaonekana kuwa chanzo kikuu cha kutokubaliana katika mzozo huu wa Ziwa Malawi ni uwepo unyonyaji wa kikoloni. Mwaka 2012 Malawi ilitoa leseni za utafiti wa mafuta kwa kampuni ya Surestream Petroleum yenye makao yake makuu nchini Uingereza, jambo ambalo lilipelekea Tanzania kupinga hatua hiyo.
Uingereza ambayo (baadae imekuja kuwa) mkoloni mkuu wa mataifa yote mawili (Tanzania na Malawi) badala ya kutatua mgogoro huu wa mipaka, imeliacha jambo hilo bila ya suluhu yoyote fafanuzi, ikiliwachia jambo hilo ni lenye kuning’inia ili siku moja waafrika wauwane wao kwa wao, ilhali wao (Uingereza) wakiendelea kunyonya rasilimali kiulaini.
Hii inaonyesha wazi kwamba wakoloni wanajali maslahi tu ya kinyonyaji, na si wenye kujali ustawi wa waafrika kwa namna yoyote.
Ili kutatua katika msingi wake mizozo ya mipaka, kunahitajika kung’oa moja kwa moja mfumo wa kibepari wa kimagharibi uliozalisha mizozo hiyo ili kuwezesha ajenda yake ya unyonyaji.
Jambo hilo linalowezekana tu kwa kuondosha ubepari kwa mbadala wa Uislamu kwa kusimamisha tena Dola ya Kiislamu ya Khilafah itakayoleta ukombozi wa aina yake katika ulimwengu wa Kiislamu na mataifa mengine yanayoendelea.
Imeandikwa na Said Bitomwa
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Maoni hayajaruhusiwa.