Ujumbe wa Hizb ut Tahrir Tanzania Wapeleka Risala Maalumu kwa Mufti Mkuu na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania
بسم الله الرحمن الرحيم
Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Jana tarehe 19 Februari 2024 Sheikh Mussa Kileo, Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano ya Hizb ut Tahrir Tanzania aliongoza ujumbe wa watu watatu akiwemo Masoud Msellem, Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari Hizb ut Tahrir Tanzania uliokwenda Afisi ya Mufti kumfikishia risala ya nasaha ya kimaandishi iliyopokewa na afisi ya Katibu wake kwa niaba yake.
Risala hiyo ni kuhusu namna jamii ya Kiislamu isivyoridhishwa na ukimya wa Mufti na BAKWATA au kutoa kwao kauli zisizostahiki kuhusiana na qadhia mbalimbali za Waislamu za kitaifa na kimataifa.
Risala ya Ujumbe huo ilihusu qadhia zifuatazo:
1. Mauaji Yanayoendelea ya Halaiki yanayotendwa na kijidola bandia cha Mayahudi kwa Waislamu wa Palestina:
Licha ya kuwepo upazaji sauti juu kilimwengu kutoka kwa Waislamu na wasiokuwa Waislamu katika kulaani na kufedhehi ukatili, dhulma na mauaji ya maelfu, wengi wakiwa wanawake na watoto kutoka kwa kijidola bandia cha Israili, bado Mufti na BAKWATA wamekuwa kimya.
2. Kufungwa kwa Kituo cha Al-Habash, Madrasa ya Wanawake ya ndani ya Dodoma:
Mnamo tarehe 02/02/ 2024 serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliamua kukifungia chuo cha wanawake cha Al-Habash kilichokuwa maeneo ya Songambele na Nkuhungu mkoani Dodoma, katikati ya Tanzania kwa madai kwamba kinaendeshwa katika mazingira hatarishi. Madrasa hiyo ina jumla ya wanafunzi wa kike 132 kuanzia umri wa 13-20. Kwa bahati mbaya BAKWATA ilitoa kauli isiyo muwafaka kufuatia qadhia hii kuiunga mkono hatua ya serikali, ikipuuza ukweli kwamba qadhia ya msongamano wa wanafunzi wengi na usalama duni wa kiafya umeenea hata katika shule za Umma . Hata hivyo hatujaona serikali kuifungia shule yoyote.
3. Kuvunjwa Msikiti wa wanafunzi, Bagamoyo:
Mnamo tarehe 06/02/2024 serikali iliuvunja msikiti wa wanafunzi uliopo Shule ya Sekondari ya Tawalanda, Chalinze, Bagamoyo, mkoa wa Pwani. Msikiti huo ulijengwa mwaka jana ambao uliwapa wanafunzi fursa ya kufanya ibada katika mazingira ya hapo hapo shuleni badala ya wanafunzi kwenda msikiti wa kando kidogo. Uongozi wa Shule ulipata baraka kutoka kwa serikali ya eneo kufanya ujenzi huo. Wakati ujenzi ukiendelea, ghafla wafadhili wakaitwa na mamalaka ya Chalinze na kusimamishwa.
Hatujamsikia Mufti wala BAKWATA kutoa kauli za kupinga hatua ya kuvunjwa msikiti huo.
4. Wanafunzi wa Kiislamu kuzuiliwa kufanya ibada/ swalah
Malalamiko juu ya jambo hilo yamekuwepo kwa muda mrefu, na wazazi na walezi wa wamekuwa wakionesha kutoridhishwa jambo hilo kwa watoto wao. Video fupi iliyosambaa karibuni ikimuonesha mzazi akilaumu hatua ya kuzuiliwa watoto wake kufanya ibada katika wilaya ya Manyoni, mkoani Singida ni moja ya mifano mingi ya uwepo wa jambo hilo. Kwa bahati mbaya na kwa masikitiko makubwa mmoja wa maafisa wa BAKWATA ndani ya wilaya ya Manyoni alijaribu kukanusha lisilokanushika akimpachika mzazi aliyepaza sauti juu ya qadhia hiyo ya kuzuiliwa na kunyimwa watoto kufanya ibada kwamba ni muongo.
Ujumbe wa (Hizb ut Tahrir) ulimtaka Mufti na BAKWATA kuchukua hatua za haraka na stahiki kuyakabili mambo hayo (yanayowasibu Waislamu) kwa kuwa wao wamekubali kuchukua dhamana ya Uislamu na Waislamu wa Tanzania na kwamba kwa jambo hilo watakuwa wenye kuwajibishwa (mas’ul) Siku ya Kiama. Hivyo wanapaswa kuhakikisha yafuatayo:
a. Qadhia za ndani na nje kama suala la Gazza zizungumziwe kwa upana na kwa mtazamo sahihi wa Kiislamu, na pia Waislamu wahamasishwe kufanya hivyo kupitia majukwaa yao mbalimbali kama khutba za Ijumaa nk.
b. Kushinikiza ili chuo cha wanawake cha Al-Habash kifunguliwe na kupewa walau muda fulani kuweza kuboresha hali na mazingira ya usalama wa kiafya, kupunguza msongamano mkubwa wa wanafunzi nk. Visingizio vilivyotolewa na serikali vya kukifungia kituo hicho vinagongana na uhalisia wa vituo vingi vya kielimu zikiwemo shule nyingi za Umma, na hatujaona vituo hivyo kufungiwa na wanafunzi wake kurejeshwa majumbani kama ilivyofanywa kwa kituo hiki cha Madrasa ya Al-Habash
c. Msikiti wa Shule ya Sekondari ya Talawanda, Chalinze, Bagamoyo uendelee kujengwa, na wanafunzi wapewe fursa huria ya kuutumia kufanyia ibada bila ya pingamizi.
Kuhusiana na wanafunzi kuzuiliwa kufanya ibada ya swalah, tunamtaka Mufti na BAKWATA yafuatayo:
Kushinikiza kwamba suala la wanafunzi kubakia shule baada ya muda uliopangwa na serikali liwe jambo la khiyari. Pia wanafunzi waruhusiwe kuswali kila siku na sio siku ya Ijumaa pekee. Mitihani ya majaribio kwa wanafunzi ifanywe siku za kawaida za masomo na sio siku za Jumamosi, ambapo wanafunzi hunyimwa fursa ya kujumuika na familia na kushiriki madrasa za masomo ya kidini.
Masoud Msellem
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari
Hizb ut Tahrir Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.