Hoja Za Kiakili Juu Ya Uwepo Wa Mwenyezi Mungu
بسم الله الرحمن الرحيم
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la watu wanaodai kukanusha uwepo wa Mungu Muumba wa Kila kitu. Aidha fikra hizi ni kongwe katika Ulaya na zimeanza kuenezwa kwa kasi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
Chanzo cha fikra hizi ni Ulaya ya Magharibi ambapo baada ya kushuhudia dhulma kubwa na unyonyaji uliofanywa na mabwenyenye kwa kusaidiwa na kiasi kikubwa na kanisa katoliki walianza kuchukia na kupuuza dini na fikra ya uwepo wa Mungu katika maisha yao.
Fikra hizi zikashika hatamu karne ya 18 hususan baada ya Mapinduzi ya Ufaransa yaliyokuja baada ya mapinduzi ya Uingereza. Mabadiliko makubwa ya kuondoa dini katika utawala na maisha yakatokea, na taratibu baada ya kukomaa ubepari kutokamana na mfumo wa ukabaila, na huo ubepari na ukiristo baada ya kushindwa kutatua matatizo ya binadamu, uliibuka mfumo mpya wa Ujamaa ambao wenyewe ndiyo uliweka wazi itikadi yake ya kukana uwepo wa Mungu.
Hata baada ya kuanguka ujamaa katika karne ya 20 na kuvunjika kwa Umoja wa kiSovieti mwaka 1991 tayari jamii kubwa ya Ulaya ilikuwa imeathirika na fikra hizi zisizo na msingi wowote.
Kufuatia hali hii kuendelea na kuathiri sehemu kubwa ya ulimwengu kwa sasa tumeleta hapa baadhi ya hoja za kiakili tu zinazofidisha juu ya uwepo wa Mungu Muumba, Mwenyezi Mungu, Allah Taala.
Ni kinyume na uhalisia kukataa uwepo wa Mwenyezi Mungu
Fikra na uhalisia ni vitu vinavyoenda sambamba. Fikra hutumika kuelezea uhalisia wa jambo, na pindi fikra inapoonekana kuwa kinyume na uhalisia, hapo huwa fikra hiyo si sahihi.
Fikra kuwa viumbe vyote viliibuka tu kutokana na mada bila ya kuwa na Muumbaji yaani Mwenyezi Mungu kama ilivyosemwa na Karl Marx ni fikra inayopingana na uhalisia. Fikra hii si sahihi na inapingana na uhalisia kwa sababu mada ni kitu halisi ambacho uwepo wake lazima kuwepo kwa chimbuko (chanzo) lake. Kwahiyo, ni wazi kuwa hii mada inayosemwa kuwa ndiyo chanzo cha uhai na viumbe, yenyewe pia ni kiumbe na ina chanzo chake, jambo ambalo wameshindwa kulielezea wanaopinga uwepo wa Mwenyezi Mungu.
Kila kiumbe ni tegemezi
Kila chenye kudhihirika huwa ni tegemezi. Kwahiyo viumbe vyote ni dhihiriko lililo na utegemezi kwa Muumba wao. Hivyo ,amejikuta binadamu akiwa ni mtegemezi mwenye udhaifu, na hii ndiyo hali ya viumbe wote huhitaji nguvu nje yao kuishi. Hii inaonesha wazi kuwa yupo mtegemewa wa viumbe wote ambaye ndiye anayeamua umri wao wa kuishi, namna yao ya kuishi, nk.
Kila kiumbe kina chanzo na hakuna kitu kinapatikana tu kwa bahati mbaya.
Baada ya kuwa viumbe na wanadamu huchukua sura ya kuwa ni tegemezi, ni wazi kuwa kila kinachotegemea kina chanzo chake (source and effect). Akili ya mwanandam inalazimisha uhalisia kuwa kitu chochote na uhalisia wowote (reality/effect) kwa kufuatilia sababu (reasoning) huwa kina chanzo chake (source).
Kwahiyo, kwa kutumia kununi hii, ni wazi kuwa viumbe vyote vina chanzo chake na ni tegemezi juu ya chanzo hicho, na huwa ni kinyume na uhalisia kukataa ukweli huu. Hii ni hoja inayoonesha kuwa Mwenyezi Mungu yupo na ndiye chanzo na mtegemewa wa kila kitu.
Udhaifu wa sayansi katika kufikiria uwepo wa Mwenyezi Mungu
Sayansi huelezea mada na sababu za kimada pekee, kwavile hakuna mada nyuma ya mada ndiyo imekuwa vigumu sayansi kufafanua chanzo cha mada na hivyo kuita mada ndiyo chanzo chenyewe.
Njia pekee ya kufahamu kilicho nyuma ya mada ni kufikiri kwenye tija (rational thinking) ambayo msingi wake mkubwa ni sababu (reasoning). Kwa kutumia fikra tunagundua kuwa mada pia ina chanzo (imeumbwa) kwa vile ni kitu na hii inalazimisha uhalisia kuwa Mwenyezi Mungu yupo.
Kutokuonekana si hoja ya kutokuwepo Mwenyezi Mungu
Hoja ya kuwa Mwenyezi Mungu hayupo kwa sababu haonekani kwa macho ni dhaifu sana. Mwanadamu ana akili uwepo wa vitu vingi bila ya kuwa na uwezo wa kuviona kwa macho mfano akili, roho,nk. bali kwa kuona athari zake tu.
Kimsingi uwepo wa kitu unathibitisha uwepo wa mmiliki wake au aliyekitengeneza. Mfano, mtu akinunua simu ya mkononi kutoka China ataamini kuwa simu ile haijajiibukia tu bali yupo aliyeitengeneza na ataitumia simu ile kwa kufuata maelekezo ya mtengenezaji hata kama hajamuona!
Hii pia inathibitisha kuwa Mwenyezi Mungu yupo pamoja na kuwa haonekani, Yeye ni mtukufu sana na sio kiumbe.
Ama kwa upande wa Quran Tukufu imetudhihirishia wazi kuwa binadamu na kila kitu kimeumbwa na Mwenyezi Mungu na Yeye ni wa enzi wa milele, alikuwepo kabla ya kila kitu na ndiyo chanzo cha ulimwengu, binadamu na uhai. Anasema Allah SWT:
أَوَلَا يَذۡكُرُ ٱلۡإِنسَٰنُ أَنَّا خَلَقۡنَٰهُ مِن قَبۡلُ وَلَمۡ يَكُ شَيۡـٔٗا
Je! hakumbuki mwanaadamu ya kwamba tulimuumba kabla, na hali hakuwa chochote? (Maryam: 67)
Ahmad Ally
Risala ya Wiki No. 123
11 Jumada al-thani 1443 Hijri /14 Januari 2022 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.