Je Ubepari Na Demokrasia Yake Imeikomboa Magharibi Na Dunia Kiujumla?
بسم الله الرحمن الرحيم
Tangu kumakinishwa demokrasia katika Ulaya katika karne ya 18, baada ya Mapinduzi ya Ufaransa ya mwaka 1789 mpaka karne hii ya 21, Ulaya imepitia tabu, majanga, misukosuko, unyonyaji na kila uovu usiosemekana kwa watu wa hali ya chini.
Jambo hilo linaleta mjadala juu ya uhalisia na uhalali wa mfumo wa maisha wa Kibepari na nidhamu yake ya kiutawala ya Kidemokrasia, je vimeweza kuikomboa Ulaya?
Ukitazama kwa kina utagundua kuwa demokrasia haijaikomboa Ulaya hata kidogo bali imeizidishia dhiki zaidi ya ilizokuwa nazo kabla ya kumakinika kwake. Wamagharibi walitunisha misuli yao karne ya 19 kwa ukoloni mkongwe, vita na mauwaji yaliyobadili rangi ya bahari na wakaendelea baada ya hapo mpaka leo kwa ukoloni mamboleo, vita na mauwaji wakidai eti kusudio ni kuikomboa dunia, Ulaya na dunia nzima, je ulimwengu umekombolewa au Ulaya imekombolewa na demokrasia?
Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha ya kwa asilimia 10 ya wamarekani wanamiliki asilimi 69.8 ya utajiri wa nchi. Na asilimia 90 iliyobaki wanamiliki asilimia 30.2 ya utajiri wa nchi iliyobaki. Kwahiyo kuna wimbi kubwa la utabaka na umasikini miongoni mwa wamarekani, watu wengi ni masikini wa kutupwa, na wachache sana ndio matajiri wasio na mfano. Hali hii si kwa Marekani tu bali nchi zote duniani.
Wanawake, wanawake, wanawake! tumeona jamii kubwa iliyonyanyasika Ulaya kwa muda mrefu ni hawa wanawake, hawakutambulika kama raia, walitakazwa kutembea mitaani, bila shaka walinyanyasika kwa kila namna.
Sasa je uhuru usio na mipaka waliopewa na ubepari umewakomboa?
Kutolewa ndani ya majumba na kuingizwa viwandani karne ya 19 wakafanya kazi kwa kushindanishwa na wanaume. Kwa kutafuta wepesi wa kupata fedha wakavuliwa nguo na umalkia wao kuanzia karne ya 20.
Wanawake hawa wanadiriki kuandamana huko Marekani ili kupitishwa sheria ya kuruhusu utoaji mimba, hawawezi tena kubeba jukumu lao la kimaumbile la kuendeleza na kuonea huruma kizazi, kwa sababu hakuna wa kusimamia maisha yao (ili wapate wasaa wa kuzaa na kukuza kizazi) bali wanawajibu wa kutafuta tonge la chakula wao wenyewe punde tu wakitimu miaka 18.
Ulaya ya leo hakuna kuombana chumvi, hakuna ujamaa, ujirani, wala furaha ya maisha. Nchini Marekani kati ya watu kumi, wanne hawana makaazi (homeless), na “homeless” huishia kuwa ‘teja’ mla unga kulingana na hali ya maisha. Hivyo, jitihada za kuwakomboa zinagonga mwamba. Wanaishiwa kustiriwa na wageni ambao wengi wao huwa na migahawa kwa mabaki ya pizza, bugger na sambusa kuwasitiri siku hata siku.
Kodi zinavunja migongo yao, afufuke leo Julius Caesar aliyetoza kodi kwa jasho na damu atashangaa ulimwengu wa leo. Leo hii kuna kodi, kuna bili, kuna ushuru na kuna tozo. Ulaya na Marekani hata asiye na uhakika wa kula yake analipa kodi, bili ndio maisha yenyewe walimwengu leo hii wanatafuta ili walipe bili, bili ya maji, bili ya umeme, bili ya gesi, bili ya simu, nauli, marejesho ya mikopo nk. Kisha tunadanganywa kwa nafuu ya uchumi kitakwimu.
Haya na mengine mengi yanayofana yanaonesha kuwa watu wa Ulaya hawajapata ukombozi kiimani, kisiasa, kiuchumi na kijamii, tangu kuanza kwa tawala za kimabavu za wafalme wa kishirikina, wakaja wafalme kwa hadaa za Ukiristo, na sasa eti watawala wa kidemokrasia bado changamoto ni zile zile. Licha ya miziki, pombe, utajiri kama inavyodaiwa bado hawana furaha, wala amani ya nafsi.
Watu wa Ulaya na Marekani hata wakija kutalii katika nchi changa ni katika njia ya kuwapumbaza na kuwaliwaza na makucha makali ya mfumo wao wa ubepari .Kimsingi wamejawa na huzuni, mawazo na kukosa mwelekeo bila shaka mawazo wanayojazwa na watawala wao ambao wanaona kujikwamua kwao ni kuendelea kuunyonya ulimwengu wa tatu huku wakiwaficha raia wao uhalisia kwani iwapo watapata mwanya tu basi wataripuka na kutambua ukombozi wa kweli ambao ni Uislamu.
Ni wajibu wetu Waislamu kuulingania Uislamu kama mfumo mbadala wa maisha kiimani, kisiasa, kiuchumi, kijamii, na kiutawala ili walimwengu wapate suluhisho la kweli. Hatuoni aibu namna makafiri na ukafiri wao walivyobeba misimamo yao na kuipenyeza katika mabadiliko ya kisiasa karne kwa karne hadi kufikia kufaulu na kuwa vinara wa ulimwengu.
Vipi sisi wenye haki, wenye Imani ya sahihi, wenye uwajibu juu ya Allah S.W.T kuwa tubebe Uislamu. Jee tunashindwa kukemea batili ili tukomboke na kuwakomboa wengine.
Tukiendelea hivi Allah SWT atawainua watu ndani ya jamii ya wamagharibi wakaubeba Uislamu, wakampenda Allah SWT naye akawapenda, na akawanusuru kama alivyoahidi. Kwani haikuwa hivi kwa wana wa Israel walipo pewa fursa ya ungofu na kupendelewa Manabii A.S na mwishowe bahati ya mkombozi wa zama za mwisho Mtume Muhammad S.A.W ikaangukia kwa waarabu waliozungukwa na ujinga (jahiliyyah) na ushirikina, ikawa hata ndio sababu ya wa Israel kumpinga. Na kwa muda mfupi tu Dini ya Allah ikatawala dunia, na ndio kawaida ya haki, haichukuwi muda mrefu kuleta mabadiliko tofauti na batili ambayo huchukuwa muda mrefu kukubalika na watu.
Risala ya Wiki No. 117
20 Rabi’ al-thani 1443 Hijri / 25 Novemba 2021 Miladi
Maoni hayajaruhusiwa.