Demokrasia ni Kuabudu Viumbe Badala ya Allah Taala
بسم الله الرحمن الرحيم
Kampeni kali ya madola ya kibepari ya kueneza nidhamu/taratibu yao fisidifu ya Kidemokrasia imewachanganya baadhi ya waislamu hadi kufikia kuihalalisha nidhamu hiyo, na wengine kuinasibisha na Uislamu kamwe. Ilhali nidhamu hii ni haramu kwa dalili wazi wazi za moja kwa moja za kukata (qatwii).
Zaidi ya yote ni dhana ya kigeni hata isiyojuulikanwa kabisa katika mfumo wa Uislamu. Mwanachuoni mkubwa maarufu Ibn Taymiyah (Rahimahullah) katika kitabu chake cha ‘Majmua Al-Fatawa’ amesema kwamba, majina yamegawika katika mafungu matatu: majina yanayotambuliwa na sharia ya kiislamu kama Salat na Zakat, majina yanayotambuliwa katika lugha ya kiarabu na kadhalika kuna majina yanayojuulikanwa kwa mujibu wa mila na desturi za watumiaji.
Tamko la ‘Demokrasia’ si tamko la sharia ya kiislamu wala si tamko la lugha ya kiarabu bali hujuulikanwa maana yake na makusudio yake kwa mujibu wa waasisi na watumiaji wake. Kwa hivyo ni makosa kuwasaidia wenyewe kufasiri tamko lao.
Kwa mujibu wa wenye tamko hili, Demokrasia ni tamko la kigiriki [kiyunani]lililoundwa kwa maneno mawili. Yaani ‘Demo’ lenye maana ya ‘Watu’ na ‘Cracy’ lenye maana ya ‘Utawala’ au ‘Mamlaka’.Likikusudiwa kuwa na maana ya ‘Utawala wa watu’. Akabainisha na kuweka wazi zaidi maana hii mmoja miongoni mwa Rais wa Marekani Bwana Abraham Lincoln aliposema:
‘Democracy is the rule of the people by the people for the people’
‘Demokrasia ni utawala wa watu, uliowekwa na watu kwa kwa ajili ya watu’
Hii ikiwa na maana kwamba watu wenyewe ndio chimbuko la nidhamu [sheria] katika maisha yao.
Yafaa pia ikumbukwe kwamba tamko‘Demokrasia’ ni Istilahi maalum, yaani ni neno au tamko lililopewa na kujengwa juu ya maana makhsusi iliyokusudiwa na wenyewe.Na mifano ya istilahi zipo nyingi katika maisha yetu ya kila siku. Kwa mfano katika
Uislamu unapotaja istilahi ya ‘Swala’ maana yake huwa ni moja tu, ambayo ni ‘ibada makhsusi yenye kuambatana na vitendo maalum kwa utaratibu maalum na muda maalum.’
Kwa hivyo, daima kila istilahi huchukuliwa kwa maana ile ile iliyokusudiwa na wenye istilahi husika. Na ndio maana katika fani ya misingi ya Sharia za Kiislamu [Usulu-l fiqh] kuna kanuni [qaida] inayosema kwamba: ‘Hakuna mzozo katika istilahi’ Ikiwa na maana kwamba watu wakikubaliana wao wenyewe kwamba tamko fulani [Istilahi] juu ya maana fulani,haiwezekani watu wengine kuibadilisha maana hiyo.
Kwa msingi huu, kwa kuwa wanademokrasia wenyewe wamewafikiana juu ya tamko hilo kwa maana tuliyokwishaitaja, hiyo ndio itakuwa maana yake ambayo ufafanuzi wake hukusudiwa, kuwa nidhamu maalum inayomruhusu mwanadamu kutunga sheria anazotaka yeye mwenyewe na kuzitawalisha kama muongozo wake katika maisha yake ya kila siku. Kwa hivyo ni uwongo wa wazi kama wanavyodai makafiri na wakala wao kwamba demokrasia ni uchaguzi wa ‘wengi wape’ na au ‘kumchagua unaemtaka tu’. Bali ukweli hasa wa Demokrasia ni mfumo wa kumpa mwanadamu mamlaka kamili ya utungaji sheria badala ya Allah Taala.
Hali hii ni kinyume kabisa na Dini yetu tukufu ya Uislamu ambapo sheria lazima zitokane na Allah Taala pekee. Kama anavyosema:
إِنِ الْحُكْمُ إِلاَّ لِلَّه….ِ
…’Hapana hukmu ila ya Allah tu’…’[Tmq 12:40]
Hii ni kwa sababu Yeye pekee ndie alieumba ulimwengu, binaadamu na uhai na kuleta nidhamu makhsusi isiyobadilika ya kimaisha ili mwanaadamu apeleke maisha yake kwa kupitia nidhamu hiyo.Kwa hivyo inakuwaje tena mwanadamu amma ajitungie au awatungie wanadamu wengine sheria?Kitu ambacho ni haki ya Allah Taala pekee. Kama anavyotangaza:
ِْ أَلاَ لَهُ الْخَلْقُ وَالأَمْرُ تَبَارَكَ اللَّهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ
…‘Zindukeni uumbaji ni wake Yeye na amri [sheria]pia ni zake Yeye.Ametukuka kabisa Allah, Mola wa viumbe vyote’[Tmq 7:54]
Huu ni ushirikina wa wazi na suala ambalo halikinaishi akili, kwamba kitendo cha kumleta mwanadamu duniani afanye Allah Taala, na kumpangia namna ya kuishi katika hii dunia apange mwengine yaani mwanadamu mwenyewe au mmoja ampangie mwengine.
Pande Mbili za Kosa Hili
Kosa la kutawaliwa kidemokrasia kwa kumpa mwanaadamu mamlaka ya kupanga utaratibu kwa akili yake ni dhambi kubwa na kosa kwa pande mbili.
Kwanza, ni kosa kwa watawala wanaotunga,kusimamia na kutekeleza sheria hizo.
Allah Taala anasema:
وَمَنْ لَمْ يَحْكُمْ بِمَا أَنزَلَ اللَّهُ فَأُوْلَئِكَ هُمْ الظَّالِمُونَ
‘Na wasiohukumu kwa yale aliyoteremsha Allah Taala hao ndio madhalimu’ [Tmq 5:45]
Pili, kwa wanaotawaliwa ambao wao amma huwapigia kura wabunge au wawakilishi kwenda kutunga sheria mabungeni, au wanaonyamaza bila ya kufanya jitihada yoyote kuibadilisha hali kutoka taratibu za kitwaghuti na kusimamisha sheria za Allah Taala kwa kupitia kusimamisha Khilafah. Makundi yote haya yanaingia katika jora moja la dhambi kubwa kwa kuridhia hali ya mambo ilivyo.Allah Taala anaonya vikali tabia hiyo.
أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ يَزْعُمُونَ أَنَّهُمْ آمَنُوا بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ وَمَا أُنزِلَ مِنْ قَبْلِكَ يُرِيدُونَ أَنْ يَتَحَاكَمُوا إِلَى الطَّاغُوتِ وَقَدْ أُمِرُوا أَنْ يَكْفُرُوا بِهِ وَيُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَنْ يُضِلَّهُمْ ضَلاَلاً بَعِيدًا.
‘Huwaoni wale wanaodai kwamba wameamini yale yaliyoteremshwa kwako na yaliyoteremshwa kabla yako?Nao wanataka wahukumiwe na sheria za kitwaghuti , ilhali wameamrishwa kukataa sheria hizo.Na shetani anataka kuwapoteza upotevu ulio mbali na haki’[Tmq 4:60]
Kutokana na ufahamu wa aya hii, kutamani kutawaliwa na twaghuti kunaingia kupiga kura kwa kumchgua mtu kwenda kutunga sheria bungeni, kadhalika kushawishi wengine kufanya hivyo,au kuridhia kwa kunyamaza kimya kwa kuwepo hukmu zisizokuwa za Allah Taala kwa kutofanya kazi ya kubadilisha hali hiyo.
Ukubwa Wa Shirki Hii
Kuchagua watu kwenda kutunga na kusimamia sheria ni sawa na kujitengezea miungu badala ya Allah Taala.Kwani katika Uislamu jambo hilo ni jukumu na haki ya Allah Taala pekee Ambae ndie huhalalisha na kuharamisha na lau analifanya mwanaadamu huwa katenda dhambi kubwa. Katika Hadithi iliyopokewa na Tirmidh kutoka kwa Adii bin Hatim[ambae mwanzo alikuwa mnaswara] anasema:
‘Nilimsikia Mtume SAAW akisoma aya katika Suratu Tawba inayosema:
اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِنْ دُونِ اللَّهِ
‘Wamewafanya wanavyuoni wao na watawa wao kuwa ni miungu badala ya Allah’
[Tmq 9:31]
‘Nikamwambia lakini hatukuwa tunawaabudu’. Mtume SAAW akasema ‘Jee hawakuwa wakiwahalalishia yaliyoharamishwa na Allah, na kuwaharamishia yaliyoharamishwa na Allah, na nyinyi mkawatii na kuwafuata kwa hayo’
Nikajibu. ‘Ndio’. Mtume SAAW akasema ‘Huko ndiko kuabudu’
Kwa hivyo kwa mujibu wa tafsiri ya aya hii alivyoitowa Mtume SAAW, watu wakitunga sheria na wengine kuwatii,kuridhia na kuwafuata huko ndio kuwafanya miungu, seuze kuwawezesha kwa kuwapa nguvu za kwenda kutunga hizo sheria kwa kuwapigia kampeni na kura.
Sisi kama Ummah mtukufu lazima tuamke na tujitoe katika janga hili ambalo hatupati faida katika maisha haya mafupi ya duniani na kubwa zaidi ni maangamizo kesho akhera na badala yake tufanye kazi kurejesha KHILAFAH ili ije isimamie sharia zetu tukufu kwa ukamilifu wake.
Khamis Saleh
Maoni hayajaruhusiwa.