Uislamu na Utumwa
بسم الله الرحمن الرحيم
Tarehe 2 Disemba ni Siku ya Kukomeshwa Utumwa Kimataifa. Ni siku ambayo kimataifa huadhimishwa kwa kukomeshwa utumwa miaka ya nyuma, lakini pia huchukuliwa kuwa ni muda wa kutathmini mapambano dhidi ya utumwa mambo leo.
Katika hali kama hiyo ni vyema kufafanua namna Uislamu ulivyoangazia suala la utumwa kwa kina, kwa kuwa ni jambo maarufu sana kusikia au kuandikwa katika vitabu kadhaa kuhusu uhusiano kati ya Uislamu na utumwa. Kwa bahati mbaya waandishi wengi wamekuwa wakiandika kinyume na uhalisia wake, ima kwa chuki dhidi ya Uislamu au mapenzi ya Uislamu lakini si kwa ufafanuzi mzuri hasa katiki nukta ya waarabu na utumwa.
Mpenzi wa Uislamu hukataa kata kata waarabu kuhusika na utumwa. Jambo ambalo huwa ni kiroja kukataa kuhusika kwa baadhi ya watu binasfi wenye asili za kiarabu. Lakini kwa upande mwingine wenye chuki za Uislamu khasa na waarabu jumla huwa wanaandika kombo pale wanapozungumzia utumwa wa miaka ya 1800’s na kujifanya wamesahau kutaja vinara na magaidi wa utumwa ambao ni Uingereza, Marekani nk. Waandishi hawa hujisahaulisha kwa lengo la kuonesha Uislamu na uarabu ndio chanzo cha utumwa. Hapa yapasa kuwa wazi mambo kadhaa yafutayo:
1. Uhusiano Kati Ya Uislamu Na Uarabu
Uhusiano ulipo ni wa kuchukuwa lugha tu ya kiarabu na si zaidi. Yaani Uislamu haukuchukua mila, fikra wala sheria za waarabu. Bali umechukuwa lugha tu, na ilkuwa lazima iwe hivyo kwani Allah Taala kwa matashi yake mwenyewe alitaka Mtume wa mwisho SAAW atoke katika jamii za waarabu. Hivyo haitarajiwi Mtume huyo ambaye ni mwarabu apewe mafundisho kwa lugha ya kilatini au kisukuma kwani ni lugha asizozijua.
Kwa kuwa mafundisho hayo lazima kwanza yeye ayafahamu vizuri kisha ndio afikishe kwa wengine. Japo mafundisho hayo yalihusu ulimwengu mzima na si waarabu peke yao. Hivyo kwa udhati Mtume SAAW licha ya kuwa ni muarabu anakuwa si Mtume wa warabu. Bali ni Mtume wa jamii zote lakini ametoka katika jamii za kiarabu. Kama vile mbavyo Tanzania raisi wake anaweza kutokana na jamii za kimakonde, kizaramo, kihaya nk, lakini hawi raisi wa makabila hayo, bali huwa ni raisi wa wote wanaojiita au kujinasibisha na utanzania.
Hivyo Mtume wa mwisho SAAW mafundisho yake ya Uislamu hayana uhusiano na uarabu, ila kwenye lugha tu na si zaidi. Na ndio maana wapinzani wa mwanzo wa Mtume SAAW walikuwa ni waarabu. Lakini wafuasi wake wa mwanzo pia walikuwa waarabu. Kwani hao ndio aliokuwa nao karibu zaidi.
Kwa bahati mbaya, kuna wenye chuki za Uislamu wao huchukua baadhi ya tabia mbaya za watu binafsi kutoka jamii za kiarabu na kuhusisha na Uislamu husukumwa na kwa roho zao mbaya na bughdha yao dhidi ya Uislamu na Waislamu.
- Uislamu Umeukuta Utumwa
Umekuja Uislamu na ukakuta watumwa na utumwa upo, tena katika kilele cha juu, ikiwa ni sehehmu ya mila na desturi za waarabu na wasio kuwa waarabu wakijihusisha na matendo ya utumwa kwa kiwango kikubwa.
Hapa ni muhimu na pakaririwe mara kadhaa kichwani, kuwa Uislamu umekuja na umekuta utumwa. Aidha, Uislamu umekuta utumwa ukiendeshwa na tawala za waarabu na wasiokuwa waarabu pia miongoni mwa watu binafsi katika waarabu na wasiokuwa waarabu.
Uislamu umekuta waarabu wakijihusisha na utumwa na wakiona ni fakhri na si aibu. Kwa hivyo, kwa ufupi utumwa ulikuwepo kabla hata ya kuzaliwa Mtume SAAW. Na alipokuja Mtume SAAW alipambana na mila hizi chafu kama tutakavyoona mbele.
- Vipi Watumwa Walikuwa Wanapatikana Kabla Ya Kuja Uislamu?
a. Vita: baada ya vita vya kikabila tahamaki mateka wa kutoka pande mbili wanaangukia kwenye utumwa wa milele na kuwa dhalili na mustadhafu mikononi mwa waliowateka. Wao na kizazi chao chote atakachokizaa kule utumwani. Na hii ndio iliyokuwa njia kubwa ya kupatikana watumwa.
b.Kununua: Hii ilikuwa mzee anaweza kuuza watoto wake kuwafanya watumwa kwa atakaewanunua.
c.Deni : mdaiwa alikuwa akishindwa kulipa deni, uamuzi unapitishwa awe mtumwa wa mdai.
d. Umasikini: Mtu alikuwa anaweza kupigwa na njaa akaamua kwenda kwa tajiri na kuomba awe mtumwa angalau apate tonge kwa uhakika wa kila siku.
e. Kupotea: Maisha wa waarabu yalikuwa ya dhiki na kutangatanga kutoka kwenda kutafuta huku na kule. Katika hali kama hiyo lau mmoja akipotea na kutokea katika jamii fulani, walikuwa wanaweza kumteka na kumfanya mtumwa
wao.
Na njia nyingine kadhaa wa kadhaa ila tumetaja chache tu.
Msimamo Wa Uislamu Kwa Utumwa
Baada ya Mtume SAAW kupata mafundisho kutoka kwa Allah Taala mwanzoni mwa kipindi cha miaka 13 hakugusa mambo haya ya utumwa kwa ukali. Bali kwa nasaha tu, kwani kuondosha hali hii isiyofaa kwa binadamu panahitajika vitu viwili vya lazima. Kwanza: elimu husika juu ya ubaya wa utumwa. Pili: nguvu kwa watakaokaidi kujiepusha.
Kwa kutumia msukumo wa elimu hiyo kwa miaka 13 kabla hajamiliki serikali alikuwa akitumia nasaha na ushauri ili watumwa waachiwe huru kama itakuwa unawamiliki. Akinasihi kuachwa huru watumwa au wakombolewe toka kwa matajiri kwa kupewa uhuru wao. Kama alivyo fanya sahaba wa Mtume SAAW, Abuu bakar ndani ya kipindi cha miaka michache aliweza kuwakombowa kwa kununua watumwa sita na kuwapa uhuru.
Lakini baada ya Mtume SAAW kupata serikali yake ndani ya Madina akakaza kamba katika kufafanua jambo hili. Huku serikali yake yenye uadilifu ikilisimamaia kulifuta kabisa hata kwa nguvu kwa atakayekaidi kufuata.
Hatua Ulizochukua Uislamu Kupambana na Utumwa
1. Kupiga mafuruku kitendo cha kuuza, kununua au kufanya mtu mtumwa. Kwa wale waliokuwa wameshapata au kuwa watumwa basi.
2. Kutangaziwa ujira mkubwa wa pepo kwa watakaowaacha watumwa huru. Na zipo aya nyingi na hadithi zenye kutangaza zawadi hiyo ya pepo kwa watakaowaachia huru watumwa.
3. Kupiga marufuku kumpa kazi nzito mtumwa. Na lau ukimpa kazi nzito lazima na wewe mwenyewe ushiriki ufanye.
4. Ukapiga marufuku kumbagua mtumwa katika kula, kunywa na kuvaa. Na hivyo mtumwa ale, anywe na avae nguo kama anavyovaa bwana wake kwa uzuri na hadhi.
5. Ukapiga marufuku kumpiga mtumwa. Na lau unampiga serikali inaingilia kati na kumuacha huru kwa nguvu utake usitake
6. Kupiga marufuku kumuita kwa lakabu ya utumwa. Bali umwite jina lake au umwite rafiki yangu.
7. Ukapiga marufuku kumdhalilisha mtumwa kwa aina yoyote ile na ukigundulikana dola inachukua nafasi yake.
8. Kwa wale watumwa wa kike ukimuingilia tu kisha kuwa huru, na anakuwa mkeo, ukifariki dunia anakurithi na nakuwa huru milele.
9. Uislamu ukatoa takhfifu kwa deni. Kwamba endapo mdaiwa akashindwa kulilipa kwa wakati, basi asubiriwe mpaka apate wasaa au asamehewe kwa kupewa sadaka. Pia lau mtu atakufa na deni, basi kizazi chake hawafanywi watumwa bali huondowa dhima kwa maiti na deni hulipwa na warithi wake na kama hawana uwezo hulipwa na dola ya Kiislamu.
10. Kukawekwa faini ya kuwaachia huru watumwa kwa baadhi ya makosa. Yaani Uislamu ukaorodhesha baadhi ya makosa ukiyafanya tu basi kafara yake umuache mtumwa huru. Kama unaye au ukamnunue kisha umpe uhuru wake.
Mfano wa baadhi ya makosa hayo:
a. kumtukana mkeo. Yapo aina ya matusi ndani ya Uislamu endapo ukimtukana mkeo kwa matusi hayo basi adhabu yake umuache mtumwa huru. Kama vile kumnasibisha mkeo kuwa ni mama yako nk.
b.Ukiuwa mtu kwa bahati mbaya bila kukusudia. Kama na kutumia kitu ambacho asili hakiuwi. Kama vile kumrushia mtu mto wa kulalia halafu mto umuangushe afariki dunia nk.
Kwa hatua hizi za Dola ya Kiislamu Waislamu na baadhi ya waarabu wakawa na wakati mgumu sana katika kukabiliana na suala la utumwa. Kwa kuona hakuna tofauti kati yao ambao ni mabwana na watumwa wao. Hivyo, wengi wao kama sio wote wakaamua kuachana na utumwa moja kwa moja.Tahamaki Uislamu ukafuta kabisa utumwa kukawa hakuna mtumwa kabisa.
Imeandikwa na Ustadh Ramadhan Moshi
Makala hii iliyohaririwa kidogo iliandikwa miaka kadhaa nyuma na Ustadh Ramadhan Moshi anaeshikishiliwa kwa kesi ya kubambikiziwa ya ugaidi kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.
Allah Taala amtoe yeye na Waislamu wote kama yeye kutoka katika mikono ya dhulma. Amiin.
Maoni hayajaruhusiwa.