‘Vita Vya Ugaidi’: Nyenzo Ya Unyonyaji Wa Marekani

بسم الله الرحمن الرحيم

Tangu mwaka 1979 idara za kijasusi za Marekani na Uingereza zilipokubaliana kubadili maana ya neno “ugaidi” na kulifafanua kuwa ni “utumiaji nguvu dhidi ya maslahi ya watu kwa malengo ya kisiasa”, ulimwengu umeingia katika taharuki kubwa na dhulma zilizopindukia.

Kuanzia hapo Marekani ikashinikiza kutungwa sheria mbalimbali ulimwenguni ili kufikia malengo yake ya unyonyaji na kumpiga vita kila aliyekataa kunyonywa sawa sawa ikiwa ni mtu binafsi, nchi, harakati, chama, kikundi nk.

Nchi zinazopinga unyonyaji wa Marekani kama Korea Kaskazini, China, Iraq, Afghanistan na Libya zimeitwa nchi za kigaidi. Harakati nyingi za Kiislamu kama Hamas, FIS nk. zimetajwa kuwa ni harakati za kigaidi kutokana na ukweli kwamba Uislamu ndiyo adui mkubwa zaidi wa Marekani na mfumo wake wa ubepari baada ya kusambaratika mfumo wa ukomunisti.

Kwahiyo imekuwa kwa upande mmoja propaganda hii chafu inatumika kwa unyonyaji na kuingilia mifumo ya ulinzi ya nchi nyingine, na kwa upande mwingine kupiga vita Uislamu. Ndiyo tunaona nchi za Kiislamu na Waislamu ndiyo walengwa wakubwa ili kuweka udhibiti wa Marekani katika nchi hizo huku ikiendeleza unyonyaji wake.

Hii ndiyo sababu takriban kila chama cha kisiasa cha Kiislamu au harakati ya Kiislamu hupachikwa nembo ya ugaidi hata zile zisozotumia mabavu wala silaha.

Viongozi katika mataifa masikini nao wamelazimishwa kuuwa, kutesa, kupoteza, kudhalilisha watu wao kwa hongo ya misaada (ya kupambana na ugaidi) na kubakia madarakani wakiathiri mahusiano ya kijamii na wakibakisha joto la chuki ndani ya nyoyo za waathirika kuwa bomu linalosubiri muda tu kuripuka.

Kama Waislamu ni lazima tupinge fikra hii hatari ambayo imeendelea kuwa ni kisingizio cha kutuuwa, kututesa, na kutunyonya kwani sisi ndiyo wahanga na walengwa wa mwanzo wa vita hivi na sheria zake ulimwenguni. Pia tuna jukumu la kulingania Uislamu ili utabikishwe kivitendo kwa kupatikana kiongozi wa Kiislamu wa kiulimwengu (Khalifah) atakayetetea na kuhami damu na heshima ya Uislamu, Waislamu na wanadamu kwa jumla.

Mwisho, tunasema kuwa Uislamu upo mbali kabisa na mtazamo unaolazimishwa na Marekani, washirika wake na wapambe wake wa kuunasibisha Uislamu na vurugu la ugaidi la kuathiri mali na maisha ya wasio na hatia.

Imeandikwa na Said Bitomwa

Risala ya Wiki No. 79

08 Dhu al-Qi’dah 1441 / 29 Juni 2020 Miladi

https://hizb.or.tz/

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir

#KomeshaUkandamizajiWaKisheriaNaUtekaji
#StopOppressiveLawsAndAbduction

Maoni hayajaruhusiwa.