24 Ramadhan
بسم الله الرحمن الرحيم
Siku kama hii 24 Ramadhan 2 Hijria alifariki dunia Abu Lahab. Bwana huyu licha ya kuwa ammi yake Mtume SAAW lakini mara baada ya Mtume SAAW kupewa Utume alisimama kuwa adui asiye na mfano kwa Mtume SAAW, Uislamu na Waislamu.
Abu Lahab ambaye jina lake ni Abd al-ʿUzzā bin ʿAbd al-Muṭṭalib alifanya kampeni kubwa ya kumpaka matope katika kumpinga Mtume SAAW. Itakumbukwa wakati Maqureishi walipowatenga na kuwawekea vikwazo Bani Hashim, Abu Hashim alikuwa mtu pekee kutoka kabila hilo la Bani Hashim kuunga mkono hatua hiyo dhidi ya ndugu zake. Pia Abu Lahab alikuwa mstari wa mbele miongoni mwa waliokula njama kutaka kumuuwa mtume SAAW wakati akiwa kalala nyumbani kwake.
Katika harakati zote upinzani wa Abu Lahab alishirikiana kikamilifu na mke wake Umm Jamil , binti wa bwana Harb bin Umayya (dada wa Abu Sufyan). Bibi huyo nae alishiriki kikamilifu kwa kufanya kila linalowezekana katika kufanikisha mateso, idhilali na kumkwamisha Mtume SAAW.
Katika tukio fulani la Mtume SAAW kuwalingania makureishi, Abu Lahab aliingilia ulinganizi wake na kumlaani Mtume SAAW kwa kumwambia (tabban laka) yaani ‘umeangania Muhammad’, baada ya tukio hilo Allah Taala akateremsha Surat Al-Masad (Tabatiyada) kumtangazia Abu Lahab na mkewe maangamizi. Katika ukweli na miujuza ya Quran, baada ya kushuka sura hiyo ya kumlaani Abu Lahab, aliendelea kuishi zaidi ya miaka kumi hakusilimu, na hatimae akafa kafiri.
Aidha, mara baada ya kuteremka Surat Al-Masad iliyotangaza maangamizi, Abu Lahab na mkewe Ummu Jamil wakawataka watoto wao wa kiume ambao ni Utba na Utayba ambao walikuwa ni waume wa mabinti wawili wa Mtume SAAW(Ruqayya na Umm Kulthum) toka kabla ya Uislamu, wawape talaka mabinti hao, na wakafanya hivyo kwa maagizo ya wazazi wao.
Katika watoto watatu wa kiume wa Abu Lahab, wawili walisilimu (‘Utba and Mu’attib ) walisilimu na kuwa mstari wa mbele kumnusuru Mtume SAAW katika Vita vya Hunayn. Na katika mabinti watatu wa Abu Lahab mmoja (Durra) alisilimu.
Abu Lahab hakushiriki katika Vita vya Badr kutokana na ugonjwa, lakini alimtuma bwana ‘As bin Hisham bin Mughira, mtu mwenye deni lake ashiriki vita vile kwa niaba yake ili iwe fidia ya deni lake, na bwana yule akashiriki.
Abu Lahab alifariki dunia baada ya siku chache tangu kumalizika Vita vya Badri, mwaka wa 2 Hijria.
Alifariki kutokana na maradhi mabaya ya kuambukiza yanayoitwa ‘adasa’. Kwa khofu ya kuwaambukiza wengine watu waliiwacha maiti yake uwanjani kwa siku kadhaa mpaka ikawa inatoa harufu. Baada ya hapo maiti hiyo ikatolewa nje kidogo ya Makka ikafunikwa kwa mawe na kutupwa mahala pa masafa.
24 Ramadhan 1441 Hijria – 17 Mei 2020 M
Maoni hayajaruhusiwa.