Jicho Langu Kwa Juhudi za Almarhum Sheikh Kilemile
بسم الله الرحمن الرحيم
Moja katika murua mwema tuliofundishwa na Mtume wetu SAAW ni kutaja wema wa maiti zetu. Jambo hilo, baada ya kutanguliza tena mkono wa taazia kwa wahusika wote wa msiba huu mkubwa limenisukuma nami kuandika japo kwa uchache juu Sheikh Suleiman Kilemile nikiwa mmoja wa wanafunzi wake, lakini pia uwepo wa usuhuba na muamala mwema baina yetu.
Nilianza kumsikia Al- Marhum Sheikh Suleiman Kilemile kupitia kipindi cha Dakika Tano cha Qur’ani tukufu cha Redio Tanzania katika miaka ya 80. Kilikuwa ni kipindi kifupi mno cha dakika tano, wakati wa saa kumi na moja alfajri, lakini ufupi wa kipindi hicho haukumzuiya Sheikh kwa uwezo mkubwa kuzitumia vyema dakika zile chache kufikisha ujumbe wenye ufafanuzi na kueleweka vyema kwa hadhira yake.
Baada ya Sheikh kurudi masomoni Saudia (1978-1983 ) kutoka chuo cha Ummu ul Quraa kilichopo Makkah, nami katika mwaka 1985 nikiwa mwanafunzi ninayejifunza Uislamu, kwa kutaka kujiendeleza zaidi katika upande wa lugha ya kiarabu, basi niliamua kwenda kwa Almarhum Sheikh Kilemile kuwa mwanafunzi wake katika fani ya swarfa na Alhamdullilah ! nilifaidika vya kutosha kwa elimu yake ambayo ni swadaka yake endelevu, Allah Taala aendelee kumlipa malipo makubwa – Amiin
Usuhuba wangu na Sheikh Kilemile uliimarika zaidi mwishoni mwa miaka ya 80’s (1987- 1989) pale Sheikh alipokuwa akiendesha darsa na khutba za kimwamko katika Msikiti wa Chihota, Tandika, nami nikiwa mmoja wa wanafunzi wake katika darsa hizo na kuzidi kuchota katika kisima cha elimu yake.
Kwa kupitia darsa hizo kutokana na kipaji na elimu aliyokuwanayo Sheikh Kilimile aliweza kutuamsha makundi mengi ya vijana na wazee kwa kutuzindua juu ya dhulma zinazotukabili Waislamu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Waislamu kukosa maamuzi.
Nakumbuka vyema namna Sheikh alivyoweza kufafanua kwa ufasaha mkubwa kwamba Uislamu ndio kheri na ndio chaguo pekee la Allah SW kwa wanaadamu. Aidha, kufafanua namna Uislamu unavyohimiza kusoma elimu nyengine, akibainisha hayo kwa dalili mbali mbali za Qur’an na Sunna
Sheikh Kilemile katika darsa zile daima alitaka Waislamu tuwe tayari kuishi kwa mujibu wa Uislamu, kuutumikia na kujiandaa kumtumikia Allah SW vilivyo na kuachana kabisa na kila kilicho kinyume na Uislamu.
Baaada ya Sheikh Kilemile kutupika tukapikika katika darsa zake za kimuamko pale Chihota, nakumbuka baadhi ya vijana tukamfuata nyumbani kwake na kumueleza Sheikh utayari wetu katika hali yoyote iwayo katika kuutumikia Uislamu, na kilichobaki tulimtaka Sheikh atueleze na atufundishe nini kinafuata. Tulikuwa tunamueleza Sheikh, kwamba vijana tuko tayari kwa hali na mali kumtumikia Allah SW na kufuata radhi zake na kuachana na mifumo ya kibinadamu, nakumbuka tukawa tunamuuliza je Sheikh tufanye nini ? Al-Marhum Sheikh Kilemile alikuwa daima akitutuliza kwa kutwambia tuendelee kuwa na subra huku tuendelee na jitihada za kujenga shule ili vijana zaidi wa Kiislamu wazidi kupata elimu.
Kabla ya safari yangu ya kwanza ya kimasomo (Oktoba 1989) nchini Sudan sikuwacha mara kwa mara kumtembelea Sheikh nyumbani kwake tukijadili mambo mbali mbali hususan ya kuuhuisha Umma wa Kiislamu. Aidha, niliporudi safari yangu ya pili ya kimasomo Madina Islamic University (1992-1996) bado niliendelea kuwa karibu na Sheikh Kilemile katika kadhia mbali mbali za kuunusuru Uislamu.
Kufuatia kubeba kwangu fikra za harakati ya Hizb ut Tahrir nakumbuka kumpatia Sheikh Kilemile kijitabu cha kiarabu cha ‘Demokrasia Ni Nidhamu ya Kikafiri’ kilichoandikwa na Hizb ut Tahrir, na pia nakumbuka kumweleza Sheikh, sasa nimepata jibu la swala lile la wakati ule “tufanye nini ?” Hizb ut Tahrir inalo jibu kwa wanaharakati wote wa Kiislamu, kwa kufafanua njia/manhaj ya Mtume SAAW ya kuleta mageuzi ya kweli kupitia ulinganizi wa kifikra na kisiasa bila ya kutumia nguvu wala silaha yoyote ile. Njia inayolenga kuurujesha tena utawala wa Kiislamu (Khilafah) itakayoanzia katika nchi kubwa za Waislamu.
Baada ya hapo Sheikh Kilimile daima amekuwa yupo karibu na Hizb ut Tahrir, akiunga mkono kazi ya da’wah ya kurejesha tena maisha ya Kiislamu kwa mfumo anaouridhia Mwenyezi Mungu.
Hapana shaka, Sheikh wetu alitamani sana kuona siku Uislamu utakapotawala tena dunia na kuwakomboa wanaadamu toka katika viza vya ushirikina na utwaghuti kwa kuurejesha tena nuru na uadilifu wake, lakini qadhaa ya Mwenyezi Mungu imemfikia.
Kwa kukhitimisha, nikiri bayana kwamba Sheikh ameacha pengo kubwa kwa Umma wa Kiislamu lakini pia amewacha alama na hazina adhimu katika upande wa kielimu na kuutumikia Uislamu. Msimamo wake huo ni jambo kuigwa na Umma amma, lakini na sisi masheikh khaswa, tuunusuruni Uislamu kwa kurejesha tena maisha ya Kiislamu kwa kuirejesha tena Khilafah Rashida ya Pili kama alivyobashiri Mtume (s.a.w), huku tukijiweka kando na mfumo fisidifu wa ubepari na siasa zake batil.
Innaa lillah wainnaa ilayhi Raaji’uun
Alkhamis 14 Ramadhani 1441 Hijri / 07 Mei 2020
Sheikh Mussa Kileo
Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano Hizb ut Tahrir Tanzania.
Maoni hayajaruhusiwa.