15 Ramadhan 144 H

بسم الله الرحمن الرحيم

1. Siku kama hii mwezi 15 Ramadhan mwaka 3 AH alizaliwa Hassan bin Ali bin Abi Talib (ra)

Huyu ni mjukuu wa Mtume SAAW, mwana wa mwanzo wa binti ya Mtume Muhammad (SAAW) bibi Fatima na mume wake Khalifah wa nne, Sayyidna Ali Bin Abi Talib (ra).

Jina ‘Hassan’ alilitoa mwenyewe Mtume SAAW, na bwana huyu alishabihiana sana na Mtume SAAW kwa maumbile na tabia. Mtume SAAW kamtaja Hassan kuwa ni katika mabarobaro wa peponi. Alikuwa bwana mchamungu asio na mfano, mpole, mnyenyekevu na mwenye elimu ya hali ya juu.

Wakati wa tukio la ‘Fathi Makka’ Hassan alikuwa na miaka saba, hata hivyo, licha ya umri wake mdogo aliweza kujifunza na kunukuu mengi kutoka kwa babu yake SAAW.

Hassan alipata malezi na makuzi mema kutoka kwa babu yake, baba yake na mama yake ambao walikuwa watu muhimu na wakupigiwa mfano kwa murua na uchamungu.

Baada ya kuuwawa baba yake Khalifa wanne Sayyidna Ali Bin Abi Talib (ra), Waislamu walimchagua Hassan ashike kiti cha Ukhalifah, na alishika nafasi hiyo kwa muda wa miezi saba kisha kuachia ngazi, baada ya makubaliano ya sulhu baina yake na Muawiyah ambaye aliasi na kuzozana na Khilafah ya baba yake awali.

Baadhi ya Maulamaa wa Kiislamu wanamuhesabu Hassan kuwa ni miongoni mwa Khulafaa rashiduun (makhalifa waongofu)

Baada ya mkataba wa makubaliano na Bani Umayya , Hassan aliondoka Kufa (Iraq) na kurudi kuishi zake Madina, alibakia na kuishi Madina ila kwa safari za hapa na pale, mpaka mwisho wa maisha yake mwaka 50 Hijria.
Hassan alizikwa Madina katika makaburi ya Al-Baqi’, kando na kaburi la bibi yake mzaa baba Fatima bint al-Asad.

 

2. Siku kama hii mwaka 37au 38 Hijria Muhammad bin Abu Bakar aliteuliwa kuwa gavana wa Misri katika Khilafah ya nne ya Imamu Ali bin Abi Talib.

Muhammad bin Abi Bakr ambaye ni mtoto wa Saydna Abu Bakar ra. Khalifah wa pili katika Uislamu alizaliwa mwaka 10 AH (Februari 632) wakati Mtume SAAW akielekea Makka katika Hijja ya kuaga.

Wakati alipokufa baba yake Sayidna Abu Bakar, Muhammad alikuwa mdogo wa chini ya miaka mitatu.
Mama yake Muhammad bin Abu Bakar ni Asma bint ‘Umays, katika wanawake mashuhuri waliokubali Uislamu mapema.
Awali bi Asma alikuwa mke wa Ja’far bin Abi Talib, na alipouwawa Ja’far aliolewa na Abu Bakar ra. Na baada ya kufariki Abu Bakar aliolewa na Imamu Ally bin Abi Talib ambaye alimlea Muhammad bin Abu bakar kwa mapenzi makubwa na kuwa mshirika wake mkuu.

Uteuzi wa Muhammad Abu Bakar kuwa Gavana wa Misri ulikabiliwa na changamoto nyingi za uasi ndani ya Misri dhidi ya Khilafah ya nne.

Muhammad bin Abu Bakar inaaminika aliuwawa ndani ya Misri na kuzikwa nchini humo katika mji wa Fustat

Masoud Msellem

15 Ramadhan 1441 H – 08 Mei 2020 M

Maoni hayajaruhusiwa.