Ukimwi Tawi la Tatizo la Ubepari
Siku ya tarehe 1 Disemba ya kila mwaka imetangazwa kimataifa kuwa ‘Siku ya Ukimwi’. Maradhi ambayo mpaka sasa bado hayana kinga wala tiba, huku yakiwa miongoni mwa maradhi yanayogharimu maisha ya watu wengi ulimwenguni. Siku hii ya Disemba Mosi hufanywa ni siku ya kukumbuka maafa na madhara makubwa yanayoletwa na ukimwi, uhamasishaji wa kupima, kuelimishana juu ya athari yake, na zaidi kutoa msisitizo wa kuwatunza waathirika wake.
Wagonjwa wa mwanzo wa maradhi ya ukimwi waligunduliwa mnamo tarehe 5/6 /1981 ndani ya jiji la Los Angeles, Marekani. Wakiwa ni watu wanatokana na jamii ya mashoga, makahaba na watumiaji madawa ya kulevya. Wote walikuwa wakikabiliwa na maradhi ya ajabu yaliyoambatana na maumivu makali ya kifua, maradhi ya ngozi, kupungua uzito na kukonda sana. Kwa upande wa Tanzania, mgonjwa wa kwanza alithibitika Tanzania Bara katika mwaka 1983 na Zanzibar wagonjwa watatu wa mwanzo waligundulika mwaka wa 1986 katika Hospitali kuu ya Mnazi mmoja.
Siku ya tarehe 1 Disemba ilichaguliwa kuwa Siku ya ukimwi kufuatia Tamko la Mkutano wa Mawaziri wa Afya kuhusu Ukimwi uliofanyika mwaka 1988, kwa sababu siku hiyo (1 Disemba) ndiyo siku iliyogundulika kirusi cha ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Ukimwi (UNAIDS) mpaka mwaka 2018 kuna karibu waathirika wa Ukimwi milioni 37.9 miloni wenye virusi vya ukimwi. Miongoni mwao milioni 36.2 ni watu wazima na milioni 1.7 milioni ni mabarobaro (miaka kama 15). Aidha, watu milioni 1.7 walikuwa waathirika wapya ndani ya mwaka 2018. Kwa upande wa watoto wadogo waathirika wakiwa kama 160,000 (0-14)
https://www.hiv.gov/…/ove…/data-and-trends/global-statistics
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni 2019 ni “Wanajamii wana uwezo wa kuleta mabadiliko”, ikitoa mwito kwa makundi yote katika jamii kama mashoga, watumiaji mihadharati, makahaba, vijana nk. kwa kuwa ni muhimili mkubwa wenye athari , hivyo waunge mkono vilivyo na kushiriki ipasavyo katika kukabiliana na janga hili.
https://www.unaids.org/…/world-aids-day-2019-communities-ma…
Qadhia ya ‘mapambano dhidi ya ukimwi’ imekuzwa kiasi kikubwa na ‘kupigiwa debe’ sana, pamoja na ukweli kwamba siyo maradhi pekee yanayoangamiza maisha. Kuna jumuiya nyingi za ukimwi kila nchi na vitengo vyake kuanzia sehemu za kazi, mashuleni, vyuoni katika shehia, kata, wilaya, mkoa, kiwango cha taifa nk. Umoja wa Mataifa nao umeunda taasisi maalum ya kushughulikia, kusimamia na kuratibu kinachoitwa kampeni dhidi ya ukimwi (UNAIDS )
Aidha, katika nchi mbalimbali duniani kama si zote zimeundwa tume maalum katika kiwango cha Taifa kwa lengo la kujishughulisha na mapambano dhidi ya ukimwi. Maradhi haya yamefikia kiwango cha kupachikwa ‘lakabu’ ya janga la kitaifa na kimataifa, na jitihada kubwa hufanywa usiku na mchana kuhamasisha kila mtu katika jamii kujihusisha kikamilifu na mapambano dhidi ya maradhi haya.
Mfumo wa kibepari unaotawala dunia leo umefanikiwa kuidandia na kuitumia vyema ajenda ya mapambano dhidi ya ukimwi katika kufikia malengo yake kimfumo. Malengo ya kuutangaza mfumo wao, kuulinda na kupambana na mfumo mwengine.
Kwa upande wa kujitangaza, wanademokrasia kiurahisi sana kwa kupitia kampeni dhidi ya ukimwi wameweza kufikisha thaqafa/mila na fikra za chafu kwa Umma wa Kiislamu na wanaadamu kwa jumla. Thaqafa inayotokamana na fikra zao za ‘uhuru’ (freedoms), kwa kusambaza uchafu wa zinaa kiurahisi, elimu ya ngono wazi wazi ikiwemo pia mbinu ya kusambaza mipira ya kondomu na kuhamasisha magoma na miziki ati uhamasishaji dhidi ya ukimwi. Wamefanikiwa pia kiasi fulani kupandikiza shaka shaka kwa baadhi ya Waislamu katika aqeeda yao kwa kuwaeleza ati dawa (ARVs) zinarefusha maisha nk. Wanayaeneza haya dhidi ya Uislamu zaidi, kwa sababu mfumo wa Kiislamu ndio pekee unaogongana na fikra zao na vitendo vyao vichafu. Fikra hizi za hatari zinapenyezwa kwa watoto wa Umma wa Kiislamu maskulini, vyuoni nk. kwa kisingizio cha ‘kinga ya ukimwi’.
Upande wa pili katika kutangaza mfumo wao wakituonesha kiujanja namna walivyo makini katika kusimama kidete katika kutatua matatizo ya wanaadamu, ilhali ni usanii wa wazi.
Mbinu hii ni kujikuza na kuukweza mfumo wao wa kibepari pia ni kujificha ‘gongo wazi’ juu ya kushindwa dhahir shahir kwa mfumo wao huo wa kikafiri.
Kwa upande wa mapambano yao dhidi ya mfumo mwengine ambao kwa leo ni mfumo wa Uislamu pekee, wamefanikiwa kiasi fulani kuondoa fikra ya msingi ya Kiislamu kwa kuwafanya Waislamu kutoyaangalia matatizo ‘kimfumo’. (kwa upana). Kampeni yao hii ya kupambana na ukimwi wanaikusudia kuwafanya Waislamu na wanadamu jumla kutoangalia suluhisho la tatizo husika kwa upana wake na kwa mujibu wa Uislamu katika msingi kama mfumo kamili. Kwa hivyo, hubakia baadhi ya Waislamu na watu jumla kupambana na tatizo hili binafsi, na kwa Waislamu kuifanya dini ya Uislamu ni dini ya suluhisho la ‘kiakhlaq’ kibinafsi tu kama zilivyo dini nyengine za kiroho tu, bila ya kujihusisha na msingi unaofinyanga hizo akhlaq.
Badala ya kupambana na mfumo wa kibepari na nidhamu yake ya kidemokrasia ambao ndio unaozalisha tatizo hili la ukimwi na mengineyo, baadhi wameburuzwa kupambana na tatizo moja moja. Pia, katika mapambano haya wanademokrasia kiujanja huwaburuza baadhi ya Waislamu kuwa askari wa kukodiwa kwa kuwabebesha kauli mbiu zao na fikra zao hatari za kikafiri.
Mapambano dhidi ya ukimwi yanaendeshwa bila ya kukhalifu tembe ya fikra za kidemokrasia. Kwa maneno mengine kampeni hii inaendeshwa chini ya usimamizi thabiti wa kanuni za ‘Haki za Binaadamu’. Kwa hivyo mwenye kushirikiana nao hapana shaka yoyote atabebeshwa fikra hizo zinazoongoza mapambano hayo. Na ndio maana Sera za Ukimwi ulimwengu mzima zinaweka wazi kwamba zinashikamana na ‘Tamko la Haki za Binaadamu’ na Maazimio mengine ya kimitagaa/ matawi ya Tamko hilo. Kwa hivyo, wanaobeba bango la mapambano ya ukimwi lazima waende sanjari na fikra hizo.
Kwa masikitiko kuna baadhi ya Waislamu wanaojiingiza katika mchakato huu na wengine hata kudiriki kuunda jumuiya za kupambana na ukimwi chini ya usimamizi wa makafiri, kimsingi huwa wanapanda farasi wasiyemjua anakotoka wala anakokwenda. Msiba mkubwa! Bila ya kutaja malengo ya mfumo huu katika uchumi na ‘maslahi’ ambacho ndicho kipimo cha mfumo wao. Hayo hudhihirika kwa kuuza dawa zao za ARVs kwa wingi na kutengeneza mamilioni ya mipira ya kondom kwa ajili ya biashara. Yote hayo wanayafikia kwa kisingizio cha kupambana na ukimwi, ati ‘janga la taifa’ na ‘kimataifa’.
Hapana shaka kwamba ukimwi ni tatizo, lakini ni tatizo tawi lililozaliwa kutokana na tatizo msingi, nao ni mfumo muovu wa kidemokrasia. Ukiondoshwa mfumo huu tatizo hili litadhibitiwa. Hivyo, ni wazi wagonjwa waliopo wanastahiki matibabu na matunzo, na wasiojimudu kwa kufariki kwa mawalii wao wapewe msaada unaostahitahiki. Hata hivyo, mfumo wa kidemokrasia kimaumbile hauna uwezo wa kuyafanya hayo kikamilifu kwa sababu zifuatazo:
Kwanza, ni mfumo wa ‘kimaslahi’ usiokuwa na fungamano la vitendo na maisha yajayo (akhera).
Pili, hauna fikra ya thamani ya kumuongoza na kumtuliza mwanaadamu aliyesibiwa na majanga. Hii ni kwa sababu suala la kumtuliza mwanaadamu aliyesibiwa na majanga lina mahusiano na fungamano baina ya mwanaadamu na Mola wake. Kwa kuwa miongoni mwa sifa za Allah Ta’ala, ni Mwenye kuleta alitakalo na kumsibu amtakae (qadhaa).
Tatu, fikra za ‘uhuru’(freedoms) ambazo ndizo nguzo za mfumo wa kidemokrasia na muongozo katika mapambano dhidi ya ukimwi ndicho kiwanda kikubwa cha kuzalishia vichochezi vinavyopelekea kuongezeka na kukuwa kwa janga hili. Chini ya fikra ya uhuru binafsi (personal freedom) kunahamasishwa kila aina ya uovu na uchafu kama ushoga, zinaa, usagajii, nk. mambo yanayochangia kwa kiasi kikubwa kwa janga hili.
Maovu yote hayo ni katika haki za msingi kwa demokrasia na si ‘dhambi’. Ndio maana hata aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo, Vijana na Jinsia wa Tanzania Dr. Incy Nkya aliwahi kukutana rasmi na mashoga mwaka 2009 kupanga mikakati ya kupambana na ukimwi, na alisema:
‘Hatuwezi kiudhati kukabiliana na Ukimwi bila ya kuwa na maongezi na makahaba na mabaradhuli,tutashinda vita hii tu ikiwa tutaungana na si zaidi ya hivyo’
(The Weekend African 29-30 Sept. 2009)
Aidha, katika mapambano haya kuna mkakati unaoitwa ‘ABC’ wakimaanisha ‘jizuilie’ (Abstinence), ‘kuwa muaminifu’ (Be faithful) au ‘tumia kondom’. (Use condom). Vipi mtu atajizuilia wakati katika mfumo wa kidemokrasia ilhali kwao ngono ni miongoni mwa haki za msingi kwa mwanaadamu, na mwanadamu yuko huru kufanya tendo hilo na anayemtaka? Na vipi mtu awe muaminifu wakati ‘uaminifu’ unafungamana na malipo na maisha yajayo (akhera), kitu ambacho mfumo wa kidemokrasia umeyabeza? Ukweli pekee wanawataka watu watumie kondom.
Fikra za mfumo wa kidemokrasia na dhana yake ya ‘mapambano ya ukimwi’ ni vitu vinavyogongana wazi wazi, na kuyafanya mapambano haya ni mapambano ya ‘kisanii’, kwa kila mwenye macho. Mapambano ya kweli dhidi ya janga hili na mengineyo yatawezekana na mfumo wa Kiislamu chini ya dola yake ya Khilafah Rashidah. Huu ni mfumo wa maadili katika kuepusha maovu na kuadhibu, si mfumo wa kisanii kama wa kidemokrasia wenye majigambo na kuwadanganya wenye fikra duni. Amesema kweli Ta’ala alipowafedhehi makafiri :
وَالَّذِينَ كَفَرُوا أَعْمَالُهُمْ كَسَرَابٍ بِقِيعَةٍ يَحْسَبُهُ الظَّمْآنُ مَاءً حَتَّى إِذَا جَاءَهُ لَمْ يَجِدْهُ شَيْئًا
‘Na waliokufuru matendo yao ni kama sarabi (mazigazi / mirage) uwandani. Mwenye kiu huyadhania kuwa ni maji. Hata akiyaendea hapati chochote’….. (TMQ 24: 39)
01 Disemba 2019
Masoud Msellem
Maoni hayajaruhusiwa.