Kuangamizwa Firauni ni Mazingatio ya Nusra Kutoka Kwetu

Katika historia ya ulimwengu na wanadamu kuna matukio mengi yenye mazingatio ambayo Mola SWT kayafanya kuwa ibra kwa vizazi vilivyopita na vya leo. Bali Uislamu unatuhimiza kuwa na mazingatio kwa qaumu (jamii) mbali mbali zilizopita kabla yetu kutokana na nguvu, athari na uwezo waliokuwa nao.

Amesema Mola mtukufu:
أَوَلَمْ يَسِيرُوا فِي الأَرْضِ فَيَنظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ كَانُوا أَشَدَّ مِنْهُمْ قُوَّةً وَأَثَارُوا الأَرْضَ وَعَمَرُوهَا أَكْثَرَ مِمَّا عَمَرُوهَا وَجَاءَتْهُمْ رُسُلُهُمْ بِالْبَيِّنَاتِ فَمَا كَانَ اللَّهُ لِيَظْلِمَهُمْ وَلَكِنْ كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ (الروم: 9).

“Je hawatembei katika ardhi waone jinsi ulivyokuwa mwisho wa wale waliokuwa kabla yao walikuwa na nguvu zaidi kuliko wao na wakaacha athari katika ardhi (majengo, pyramid, mafuvu nk) na wakaiimarisha zaidi yenu na waliijiwa na Mitume wao kwa ubainifu, basi hakuwa Mola ni mwenye kuwadhulumu lakini wenyewe walijidhulumu nafsi zao” (TMQ 30:9 )

Ndani ya aya hii tunapata ukumbusho mkubwa hasa kwa wale wenye kufanya ufisadi katika ardhi na kwenda kinyume na mipaka ya Mola SWT hususan viongozi wanaosimamia mambo, hatamu katika maisha na kuwa na mamlaka hasa nchi kubwa zenye kumiliki kura turufu ya veto. Nchi ambazo leo viongozi wao ni vinara wa kupitisha maazimio mbalimbali, kushambulia nchi zingine hususan za Waislamu, kupora rasilimali za nchi changa hasa bara la Afrika nk. kupitia mikataba ya unyonyaji. Nchi hizo zinakumbushwa uwepo ghadhabu na adhabu za Allah SWT kama zilizowasibu waliotangulia ambao walikuwa na maumbile makubwa, nguvu, majeshi, utawala wa maeneo makubwa, kujenga majengo marefu kama kutoboa majabali na kutengeneza makazi humo kama vile qaumu Aadi nk., majengo ambayo hayajatokea tena mfano wake.

Licha ya qaumu hizo zilizotangulia kuwa na nguvu na athari katika ardhi, kamwe hazikuweza kuzuiya adhabu ya Mola, Mwenye nguvu pindi walipotakabari kwa kuwacha maamrisho yake.

Miongoni mwa tukio kubwa lenye mazingatio ni la kuangamizwa Firauni (Ramsis ii) ndani ya Bahari ya Sham (Red sea) lililotokea ndani ya mwezi huu wa Muharram. Firaun aliyekuwa mtawala wa Misri zama hizo ambaye Mola SWT alimpa nguvu na jeshi kubwa mpaka kupindukia mipaka na kuwataka watu wamwabudu yeye pekee yake na kutangaza kwa jamii yake kuwa yeye ndio Mungu mkuu zaidi. Licha ya kupewa dalili za wazi za kuwepo Mola Mmoja , Muumba, Firaun alizikanusha wazi wazi kwa uluwa na inadi

Katika zama za utawala wa Firaun kulishuhudiwa ufisadi mkubwa na mauaji ya kikatili yaliyopindukia mipaka kiasi kwamba alikuwa akiwachinja watoto wa kiume pindi tu wanapozaliwa katika hali ya uchanga na kuwaacha hai watoto wa kike.

وَإِذْ نَجَّيْنَاكُمْ مِنْ آلِ فِرْعَوْنَ يَسُومُونَكُمْ سُوءَ الْعَذَابِ يُذَبِّحُونَ أَبْنَاءَكُمْ وَيَسْتَحْيُونَ نِسَاءَكُمْ وَفِي ذَلِكُمْ بَلاَءٌ مِنْ رَبِّكُمْ عَظِيمٌ (ال
“Na kumbukeni (enyi wana wa israel) tulipokuokoeni na watu wa Firauni wakikupeni adhabu mbaya wakiwachinja watoto wenu wanamume na kuwaacha hai watoto wenu wa kike na katika hayo (kuokolewa huko) ulipatikana neema kubwa iliyotoka kwa Mola wenu” (TMQ 2:49 )

Kama ilivyokuwa desturi ya watawala waovu huwagawa watu kwa kutengeneza matabaka kwa kuwapendelea watu wa jamii yake, iwe kabila au ukoo wake. Jamii ya kiyahudi ndani ya Misri chini ya Firaun ilikuwa jamii duni, yenye kudharauliwa isiyokuwa na thamani, kiasi kwamba ilipita katika mateso ya utumwa, dhiki, khofu na wakati mgumu muda mrefu chini ya utawala wa Firauni.

Na amesema Allah Taala :
إِنَّ فِرْعَوْنَ عَلاَ فِي الأَرْضِ وَجَعَلَ أَهْلَهَا شِيَعًا يَسْتَضْعِفُ طَائِفَةً مِنْهُمْ يُذَبِّحُ أَبْنَاءَهُمْ وَيَسْتَحْيِ نِسَاءَهُمْ إِنَّهُ كَانَ مِنْ الْمُفْسِدِينَ
“Hakika ya Firauni alitakabar katika ardhi na akawagawa watu wake makundi mbalimbali akilidhoofisha kundi moja miongoni mwao akiwachinja watoto wao wanaume na kuwaacha hai watoto wao wanawake. Hakika yeye alikuwa miongoni mwa waharibifu kabisa” (TMQ 28:4)

Hiyo ndio hali na maisha waliokuwa wakiishi Bani Israil, ni maisha ya tabu na idhlali kubwa. Kutokana na ufisadi huo, Mola SWT akamtuma Mtume wake Musa As. kwa Firaun kwa hoja zilizowazi ili aache kufanya ufisadi, aache kuwaadhibu, kuwaua na kuwatesa Bani Israil na anyenyekee kwa Muumba wake.

فَأْتِيَاهُ فَقُولاَ إِنَّا رَسُولاَ رَبِّكَ فَأَرْسِلْ مَعَنَا بَنِي إِسْرَائِيلَ وَلاَ تُعَذِّبْهُمْ قَدْ جِئْنَاكَ بِآيَةٍ مِنْ رَبِّكَ وَالسَّلاَمُ عَلَى مَنْ اتَّبَعَ الْهُدَى

“Basi mwendeeni na mwambieni kwa yakini sisi ni Mitume kutoka kwa Mola wako, basi waachie wana wa Israil watoke pamoja nasi wala usiwaadhibu. Hakika tumekujia kwa ishara za wazi kutoka kwa Mola wako. Na amani iko juu ya wale wanaofuata uwongofu” (TMQ 20:47 )

Licha ya usulub / utaratibu mzuri aliotumia Nabii Musa na nduguye Harun As na hoja za wazi dhidi yake ikiwemo kubatilisha uchawi mkubwa, Firaun aliendelea kufanya ufisadi na kuwaadhibu wana wa Israil kwa kuwaua watoto wao wa kiume.Baya zaidi hata kuwasulubu wachawi aliokuwa akiwategemea kwenye utawala wake ambao walimwamini Mwenyezi Mungu baada ya kuona muujiza wa Musa As. ukiharibu na kubatilisha uchawi wao.

Ndipo Mola SWT akamwamrisha Musa As. kuondoka Misri na wana wa Israil kutokana na uadui uliokuwa umepindukia mipaka kiasi kwamba walikosa kabisa furaha na amani katika maisha yao.

Wakati wakitoka Misri, Firauni na jeshi lake waliwafuata kwa kiburi na uadui mkubwa ili wawaangamize kabisa na kukifuta kabisa kizazi cha Wana wa Israil. Kizazi ambacho hakikuwa na silaha yoyote ya kupambana na mtawala huyo. Tahamaki Firauni yupo nyuma yao, ilhali mbele yao kukiwa ni bahari isiyokuwa na mashua wala marikebu.

Mbele ya bahari ya Sham, Mola SWT akamwamrisha Musa As. kupiga bahari kwa fimbo yake na kutengeneza njia kimiujiza ambayo Bani Israil walipita katikati ya bahari bila ya kizuizi.
Quran Tukufu inasema:

وَجَاوَزْنَا بِبَنِي إِسْرَائِيلَ الْبَحْرَ فَأَتْبَعَهُمْ فِرْعَوْنُ وَجُنُودُهُ بَغْيًا وَعَدْوًا حَتَّى إِذَا أَدْرَكَهُ الْغَرَقُ قَالَ آمَنْتُ أَنَّهُ لاَ إِلَهَ إِلاَّ الَّذِي آمَنَتْ بِهِ بَنُو إِسْرَائِيلَ وَأَنَا مِنْ الْمُسْلِمِينَ (يونس: 90

“Na tukawapitisha Wana wa Israil katika bahari, basi Firauni na wanajeshi wake waakawafuata kwa dhulma na kibri, na hata mpaka alipofikiwa Firauni na kuzama alisema naamini ya kwamba hakuna aabudiwaye kwa haki ila Yule wanayemwabudu Wana wa Israil na mimi ni miongoni mwa wanaosalimu amri’ (TMQ 10:90)

أَالآنَ وَقَدْ عَصَيْتَ قَبْلُ وَكُنْتَ مِنْ الْمُفْسِدِينَ (يونس: 91

“Leo hii (ndio unamkumbuka Mola) hali ya kuwa uliasi kabla na ulikuwa miongoni mwa waharibifu” (TMQ 9:91 )

فَالْيَوْمَ نُنَجِّيكَ بِبَدَنِكَ لِتَكُونَ لِمَنْ خَلْفَكَ آيَةً وَإِنَّ كَثِيرًا مِنْ النَّاسِ عَنْ آيَاتِنَا لَغَافِلُونَ (يونس: 92).

“Basi leo tutakuokoa kwa kukuweka mwili wako ili uwe dalili kwa ajili ya watakaokuja baada yako, na watu wengi wameghafilika na ishara zetu (TMQ 10:92)

Ishara hii kubwa ya kuokolewa mwili wa Firaun na kuwepo mpaka leo katika makumbusho nchini Misri ni alama kubwa ya kuwepo Mola, Mwenye nguvu, na kamwe waovu na madhalimu hawana uwezo wa kumkimbia akitaka kuwaangamiza.

Huu ndio ukawa mwisho wa Firauni kwa kuangamizwa kwa idhlali kubwa hali ya kuwa Wana wa Israil wakishuhudia tukio hili lililoacha athari mpaka leo ili iwe mazingatio kwa waovu na watawala wenye tabia kama ya Firaun, tabia ya kufanya ufisadi katika ardhi ikiwemo kujitwisha jukumu la Muumba la kuwatungia watu sheria hali ya kuwa milki ya kutunga na kuweka sheria ni ya Mola pekee.
Aidha, tukio hili ni ishara tosha kwa kila mwenye shaka juu ya nusra ya Allah Taala kutambua kuwa nusra, ushindi dhidi ya vitimbi vya watu waovu huishia pabaya na si chochote mbele ya Mola, Mwenye nguvu.

Umma wa Kiislamu leo licha ya kupita katika hali ngumu ya dhulma na mateso kila mahala kuanzia China, Afghanistan, Iraq, Kashmiri, Somalia , Yemen tuna wajibu wa kuendelea kulingania huku tukiwa na yakini kwamba Allah SWT anaona vitimbwi vya makafiri na vibaraka wao, na utakapofika muda wake ataleta nusra yake na hakuna wa kumzuiya.

Ust. Issa Nasibu

Risala ya Wiki No. 57
24 Muharram 1441 hijri 23/09/2019 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.