Upana wa Tukio la ‘Mwaka wa Ndovu’
Mwezi wa Muharram umeingia, ndio mwanzo wa mwaka mpya wa Kiislamu, mwezi alioangamizwa Firaun lakini pia ndio mwezi uliotukia jaribio ovu la mtawala na Jemadari Abraha na jeshi lake la ndovu kutaka kuivunja Haram tukufu ya Al-Kaaba. Mwaka wa tukio hili katika tareekh huitwa ‘mwaka wa ndovu’ (570/571 AD) kwa kunasibishwa na tukio hili kubwa la aina yake la kuangamizwa jeshi la ndovu, lakini ndio mwaka huo huo aliozaliwa Mtume SAAW kuwa ishara ya mwaka wa neema na ushindi. Tukio hili la Aswahabu lfiil lilitokea karibu siku sitini au kasoro kidogo tu kabla ya kuzaliwa Mtume SAAW.
Tathmini ya kijeshi ya Abraha kwa Makureishi kwa mujibu wa kipimo cha kibinadamu ilikuwa sahihi kabisa kwamba uvamizi wake kamwe hautopata upinzani wowote wa kijeshi kutoka kwa Makureishi kutokana na namna alivyojizatiti kivita akijidhihirisha na jeshi kubwa la masilaha makubwa ya maangamizi ya ndovu ambayo hayakujuulikana katika jamii ya watu wa Makkah na waarabu kwa ujumla.
أَلَمْ تَرَى كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِأَصْحَابِ الْفِيل الفيل: 1).
“Jee hukuona jinsi Mola wako alivyowatenda watu wa ndovu?”
Tukio hili licha ya kuwa ni kielelezo cha tabia ya kimaumbile ya ushindani wa ubwana wa madola makubwa uwe wa kidini, kisiasa au kimfumo kwa zama zetu, kwa wakati ule pia lilikuwa likiashiria hitajio la mabadiliko ya kimsingi. Ni katika mazingira kama hayo Allah Taala akamleta Mtume SAAW ambae alikuja kujaza pengo la hisia/ghariza ya kuabudu na kuja kutandikia utawala thabiti wa kiuadilifu ili watu waishi katika kivuli cha raha na amani kama yalivyo maumbile ya mwanadamu kuwa na hisia ya kutaka maisha ya furaha, amani na utulivu katika ulimwengu huu.
Itakumbukwa wakati wote katika tareekh kwamba madola vinara hata kama hayakubeba mfumo (kwa wakati huo) bado yalibeba uoni kwamba ili yamakinike vyema katika ubwana wao pia yalipaswa kuwa na ubwana wa kidini.
Kwa hivyo, historia inaonesha dola vinara za wakati huo yaani Roma na Fursi daima zilikwenda mbio kuupigania na kuhifadhi hata ubwana wa kidini, amma kwa kudai tawala zao ni za kidini moja kwa moja au kutabanni dini fulani kwa kuipa heshima na hadhi, sio lazima kwa mapenzi makubwa ya dini husika lakini wakati mwengine hata kwa maslahi ya kisiasa na kiutawala.
Kwa mfano, ukiristo ulifanywa kuwa dini rasmi ya dola ya Himaya ya Roma zama za mfalme Theodosius I (379-95). Hii ni baada ya mfalme wa awali aliyetangulia Constantine I (306 – 37) kuandaa mazingira kwa kutanguliza hatua kadhaa kama vile kupitisha katika Tamko la Milan/ Edict of Milan 313, lililotoa mwito kuwa wakiristo waamiliwe kwa wema, mfalme binafsi kuwa mwenyekiti wa kikao cha Baraza la Kanisa / Council of Nicaea (325) pia kuufanya mji wa Constantinople / Istanbul kuwa mji rasmi wa kikiristo. Hatimae baada ya hatua hizo mwaka 381 ukiristo ukatangazwa rasmi kuwa dini ya dola.
Halikadhalika Himaya ya dola ya kifursi (The Sassanid dynasty (224-651 AD) mapema zaidi waliitangaza dini ya Umajusi/ Zorostrian kwamba ni dini ya dola kwa kuitukuza, kuipa hadhi na dola kujitangaza kwamba wao ndio walinzi wa unaoitwa ‘moto mtakatifu’ ambao katika dini ya Majusi hudai moto huo ndio dhihirisho la Mungu wao Ahura Mazda duniani.
Kwa upande wa Makureishi japokuwa walikuwa sio wenye kutajika katika ubwana wa kisiasa katika Bara arabu, lakini bado walikuwa na haiba na hadhi ya juu kutokana na umashuhuri wa ibada ya Hija, yaani nyumba tukufu ya Al-Kaaba. Hadhi na haiba hiyo iliyafanya madola mengine hususan ya kinaswara (Roman Empire) yawe na shauku ya kutaka kuwapora ubwana huo.
Hadhi ya ibada hiyo iliwasukuma Makureishi kwanza kujipanga vyema kwa kuunda nidhamu thabiti na mwanana katika kulisimamia jukumu zima la ibada hiyo ambapo koo ya Abd Manaf / Bani Hashim (koo ya Mtume SAAW ) ikawa na dhamana ya kulisha na kunywesha mahujaji. Ilhali koo ya Abdul – Dar (Bani Shayba) ikawa na jukumu la ufunguo wa Al- Kaaba3, yaani kufunga na kufungua, jukumu wanaloendelea nalo kabila hili mpaka leo.
Pia hadhi, haiba ya Hijja iliwafanya makureishi waibebe kwa hadhari, ufakhari na uangalifu mkubwa daima wakikhofu isije ikawaponyoka, kiasi kwamba hata alipokuja Mtume SAAW kuwalingania Uislamu baadhi walikhofu kumfuata kwa kisingizio cha ufahamu wa kimakosa kwamba kukubaliana na mfumo wa Uislamu kunaweza kuibua vita baina yao na jamii nyengine, jambo linaloweza kupelekea kunyanganywa hadhi na ufakhari wao wa nyumba tukufu.
Allah Taala Anakumbusha:
وَقَالُوا إِنْ نَتَّبِعِ الْهُدَى مَعَكَ نُتَخَطَّفْ مِنْ أَرْضِنَا أَوَلَمْ نُمَكِّنْ لَهُمْ حَرَمًا آمِنًا يُجْبَى إِلَيْهِ ثَمَرَاتُ كُلِّ شَيْءٍ رِزْقًا مِنْ لَدُنَّا وَلَكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لاَ يَعْلَمُونَ (القصص: 57).
“Na wakasema : Tukiufuata uongofu huu pamoja nawe tutanyakuliwa kutoka katika nchi yetu. Je ! kwani sisi hatukuwamakinisha katika mahala patakatifu, penye amani, ambapo huletewa matunda ya kila aina kuwa rizki itokayo kwetu? Lakini wengi wao hawajui” (TMQ Al-Qas’as : 57)
Kuibuka kwa uvamizi wa Jeshi la ndovu ulikuwa ni kilele cha ushindani mkali na mkongwe wa kidini na kisiasa ulioshamiri katika baadhi ya sehemu za Bara Arabu hususan katika biladi ya Yemen. Biladi hiyo ilikuwa muhimu katika Bara Arabu kwa maendeleo na ustaarabu tangu mwaka wa 340 AD, daima ilikuwa amma medani au chimbuko la mapambano kabambe ya kisiasa na ushindani wa kidini wa kieneo.
Katika miaka 300 AD Dola ya Himaya ya Warumi iliiteka biladi ya Yemen na kuushikilia mji muhimu wa Adn (Aden). Aidha, ikawasaidia mahabeshi ndani ya mwaka 340 kuichukuwa sehemu kubwa ya ardhi hiyo, kwa kutumia udhaifu, ugomvi na husuma baina ya makabila makubwa ya Hamdan na Himyar nchini humo. Hali iliendelea hivyo mpaka katika mwaka 378 Yemen angalau ilipodiriki kupumua kidogo kwa kujiamulia mambo yake yenyewe bila ya mkono wa nje. Hata hivyo, utulivu na utangamano huo haukudumu. Hiyo ni kufuatia baadhi ya maeneo ya waarabu kuanza kuingia katika dini ya kiyahudi/Judaism.
Hamahama ya mayahudi katika maeneo ya waarabu kutokana na kipigo cha watawala mbalimbali kama mfalme Bukhtanasar na Warumi mnamo mwaka 70 AD ilipelekea kueneza dini yao sehemu za waarabu na kuanza baadhi ya makabila ya kiarabu kuikubali dini ya kiyahudi. Jambo hilo lilizidisha moto wa mashindano makubwa ya kidini hususan kutoka kwa tawala ya kirumi ambayo walitukuza Unaswara.
As’ad bin Abi Karb alikuwa mmoja kati ya walioibeba dini hiyo kutoka Yathrib na kuipeleka katika biladi ya Yemen.
Baada ya kifo chake, mwanawe Yusuf Dhu-Nawas aliibeba dini hiyo kwa misimamo mikali zaidi, kiasi cha kuwalazimisha wafuasi wa dini nyengine hususan manaswara kuifuata dini hiyo kwa nguvu kiasi cha kuwaadhibu na kuwauwa kwa mateso na ukatili wale wote waliokataa kutii mafundisho ya dini hiyo. Wakati huo ndio liliibuka tukio la la mauaji ya kikatili ndani ya mahandaki ya moto (As-hab ul uhdud).
Katika hali kama hiyo, dola ya Himaya ya Kirumi ambayo ilikuwa watawala wake ni wafuasi wa dini ya kinaswara/wakiristo ikapata tena kisingizio cha kuingilia kati tena mambo ya Yemen ili kuwakomboa manaswara wenzao waliokuwa wakikandamizwa, wakiteswa na kunyanyaswa na Dhu-Nawas kwa kulazimishwa kufuata dini ya Kiyahudi.
Dola hiyo ikamsaidia muhabeshi kwa jina la Eriat kuichukuwa na kuiteka Yemen kuwa katika himaya yao. Vuguvugu la kisiasa ndani ya utawala wa Eriat lilipelekea Eriat kupata upinzani wa ndani na hatimae kupinduliwa na Abraha. Na Abraha licha ya kuumakinisha unaswara ndani ya Yemen pia alitaka kutokana na misimamo yake mikali hata waarabu wengine wanyenyekee dini hiyo kwa gharama yoyote hata kwa mabavu, hali hiyo ilimpelekea kuja na ajenda ya kuivamia na kuivunja Al – Kaaba yenye kuhusisha ibada kubwa na mashuhuri kwa waarabu ili waarabu wanyenyekee dini ya kinaswara, lakini Allah Taala akamuangamiza Abraha na jeshi lake.
Kushindwa Abraha na jeshi la Ndovu kwa uwezo wa Allah Taala uhalisia wake ni msukumo wa kisaikolojia wa kuandaliwa jamii ya Makureishi, waarabu na wanadamu kwa jumla kumkubali Mtume SAAW. Ukiangalia kwa makini utaona eneo kubwa la Bara ya Arabu hususan maeneo ya Makureishi licha ya kaskazini mashariki na magharibi kupakana na madola makubwa ya Himaya ya Roma na Wafursi bado hayakuvamiwa moja kwa moja kana kwamba yalipewa hifadhi maalum na kubakia salama kwa muda mrefu kwa malengo maalumu. Sio hivyo, tu bali wanahistoria wanaeleza kwamba katika kipindi cha miaka 150 jamii ya makureishi walijikusanya pamoja zaidi, hali iliyopelekea kuimarika na kutoa muundo mzuri lugha na lahaja ya kiarabu chao
Silsila ya matukio hadi kufikia zama za Abraha kushindwa jeshi lake na baadae kuja Mtume SAAW kuleta ukombozi wa kweli, kunadhihirika kanuni muhimu ya mabadiliko ya kimsingi. Nako ni kutangulia migogoro, vurugu, kukosekana uthabiti wa kisiasa na kijamii na ushawishi wa madola vinara kubadilika kutoka dola moja kwenda jengine. Kwa mfano, kumedhihirika migogoro ya kuvunja mfupa baina ya makabila ya kiarabu ya Hamdan na Himyar ndani ya Yemen iliyopelekea kuchukuliwa nchi yao, kisha mgogoro wa kidini wa mateso yaliyoletwa na Dhu-Nuwas, kisha mtawala Eriat akashika hatamu ndani ya Yemen na kupinduliwa na Abraha. Na utawala wa Abraha (mahabeshi) baada ya tukio la Jeshi la Ndovu nao ukapinduliwa na Ma’dikarib Al- Himyar, kisha na utawala huu ukapinduliwa wakachukuwa hatamu za utawala mafursi ndani ya Yemen moja kwa moja mpaka gavana wao Badhan ndani ya nchi hiyo aliposilimu baada ya Mtume SAAW kusimamisha dola ya ya mwanzo ya Kiislamu.
Kwa upande mwengine kabla ya mabadiliko makubwa ya kimsingi chini ya uongozi wa Mtume SAAW kulikuwa na migogoro ya kiuadui kwa makarne baina ya makabila ya makureishi pia makabila makubwa mawili ya Aus na khazraj ndani ya Madina.
Baada ya vurugu mechi na majanga ya kisiasa, kijamii na kiuchumi yalikuja mabadiliko makubwa ya Mtume SAAW yaliyoiweka Bara Arabu yote ikiwemo Yemen na ulimwengu jumla chini ya himaya ya dola ya mwanzo ya Kiislamu. Leo tuna wajibu wa kuilinganisha hali na matukio hayo na mazingira yetu. Licha ya kuwa bishara ya Allah Taala na Mtume wake SAAW iko upande wetu, lakini hali halisi ya matukio ya kushtadi vurugu za kisiasa na kijamii ni ishara tosha ya kuelekea katika mabadiliko ya kimsingi ya kurudi tena dola yetu ya Khilafah Rashidah.
Migogoro katika nchi za Waislamu kuanzia waarabu inadhihirisha wazi wazi kwa dhana ya uarabu iko butu na haina mashiko na kamwe haiwezi kuwanusuru waarabu. Dhana ya uafrika pia nayo inafedheheka wazi wazi kwa yanayojiri sasa ndani ya Afrika kusini ambayo hujiri kila siku katika nchi mbali mbali za Afrika kwa kupigana na kuuuwana wao kwa wao kwa misingi ya ubaguzi. Kwa upande wa kimfumo mfumo wa Kikomunisti umeanguka kifudifudi. Na mfumo wa kibepari ambao ndio unaoshikiliwa na vinara leo Marekani, Uingereza nk. nao uko hoi bin taaban.
Kunadhihirika mambo matatu ya wazi wazi kufeli kwa wazi kwa mifumo na vitawi vyake vya fikra ndogo ndogo kama za uaswabia nk, wanadamu kuhitaji suluhisho jengine. Pia kunadhihirika hali ya kukata tamaa.
حَتَّى إِذَا اسْتَيْئَسَ الرُّسُلُ وَظَنُّوا أَنَّهُمْ قَدْ كُذِبُوا جَاءَهُمْ نَصْرُنَا
“Mpaka pale Mitume ilipowafikia hali kama ya kukatisha tama, wakaona kuwa wamekadhibishwa, hapo ikawajia nusra yetu” (Yusuf : 110)
6 Septemba 2019
Marejeo
1. AChronology of Islamic History 570- 100 CE ( H.U. Rahman – Taha Publisher, London
2. https://en.wikipedia.org/wiki/Zoroastrianism
3.Kitabu cha Ar-Raheeq Al Makhtoum (The Sealed Nectar) Safi ur Rahman Al- Mubarakpuri – Maktabat- ul Iman , Luton, Uk
4. Ufafanuzi kutoka Sheikh Mussa Kileo juu ya namna Kiarabu cha Makureishi kilivyomakinika kama maandalizi ya kuja Mtume SAAW
5. Al-Muntakhab , Tafsiri ya Kiswahili ( Ali Muhsin Al-Barwan) Dubai UAE
Maoni hayajaruhusiwa.