Kuangazia Mgogoro Ndani ya Ccm
Baada ya Bernard Membe, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali iliyopita na kinara wa mstari wa mbele katika kinyan’ganyiro cha uraisi kupitia CCM katika uchaguzi wa 2015 kupeleka kilio chake mahakamani kwa madai ya tuhuma chafu mbalimbali anazopewa na mtu anayejinadi kuwa mwanaharakati huru Cyprian Musiba, karibuni pia tumeona makatibu wakuu wastaafu wa CCM nao wakipaza sauti zao kwa muktadha huo huo, lakini wao kwa mbinu ya kutawanya warka uliosambazwa kwa Umma ambao umewacha mjadala mkubwa.
Kilichofuatia baada ya warka huo kana kwamba kuchapua mambo zaidi, kukasambazwa mutawaliya (moja baada ya nyengine) kanda kadhaa za sauti zinazosemekana kubeba sauti za makatibu wastaafu na watu wengine nyeti ndani ya CCM zenye kudokeza kwamba mambo sio shuari ndani ya chama tawala cha CCM.
Husuma, migogoro, mizengwe na vurumai ndani ya vyama vya kidemokrasia kwa mwenye kufahamu udhati wa msingi wa vyama hivyo sio jambo geni bali ni maarufu, iwe chama tawala au upinzani, viwe vya ndani au nje. Tumeshuhudia migogoro mingi tu ndani ya vyama vya kidemokrasia, na lau kuna dhamira ya kuandika vitabu kuhusu vurumai na migogoro hiyo itakusanywa mijalada (volumes) mingi isiyo na mithali.
Sababu msingi ya migogoro, mizengwe na vurumai hizo ni kutokana na msingi mmoja tu uliojengewa siasa hizo. Nao ni ‘maslahi’. Hiki ndio kipimo cha mfumo wa kibepari na nidhamu yake ya kisiasa ya kidemokrasia. Kwa msingi huo yatosha taasisi yoyote inayotokamana na msingi huo iwe ya kisiasa au nyengineo huwa ni taasisi ya kiugomviugomvi, amma ugomvi unaotokota ndani kwa ndani kwa muda, au utaodhihirika nje muda muwafaka unapojiri. Na mgogogoro unapohusisha chama tawala huvuma zaidi na hudhihirika wazi wazi, kwa kuwa macho ya wengi yapo zaidi katika chama kinachoshikilia hatamu za utawala kuliko vyama vya upinzani. Lakini ukweli unabaki pale pale kwamba migogoro ndio tabia za vyama vyote vya kidemokrasia.
Migogoro, mizengwe na husuma katika vyama hudhihirika zaidi karibu na uchaguzi au zinazolenga malengo yake. Vurumai na husuma hizo hutokana na kuibuka kwa kambi mbalimbali za ndani zinazochuana kwa lengo la kujinyakulia madaraka (maslahi). Yameshuhudiwa hayo ndani ya CCM katika kutafuta mgombea uraisi mwaka 1995, yakajiri tena mwaka 2005 ambapo vurumai lake lilileta hali ya fadhaa, aibu na fedheha isiyo na kifani baina yao. Na vurumai la mwaka 2015, likawa kali na la kuvunja mfupa, kwa kambi moja kupingana na nyengine wazi wazi, nje hata ya vikao vyao, na hatimae kumsukuma Edward Lowassa kuacha CCM kwa ghadhabu na kuingia katika chama cha upinzani cha Chadema. Vurumai, husuma na fedheha hizo ni endelevu na hazitosita, ni kana kwamba ni zamu baina yao, kambi inayopata mara hii, hupatwa mara ijayo, inayosaliti mara hii, husalitiwa mara ijayo, hali inayoambatana na chuki, visasi, husuma na bughudha la nyoyoni kutokana na fungamano duni na dhaifu la kimaslahi ndani ya vyama vyao. Mwanachuoni mkubwa, Mujtahid, mwanafikra na mwanasiasa wa Kiislamu Sheikh Taqiudin Nabahan aliwahi kuandika haya:
‘Na miongoni mwa mafungamano fisidifu/maovu yanayodhaniwa kuwa ni mafungamano sahihi ni fungamano la kimaslahi…. Nalo ni fungamano la muda tu lisilofaa kuwafunga watu, kwa sababu hutokea mashindano ya kupata maslahi makuu, basi fungamano hili hupotea katika hali ya kupimwa maslahi makubwa zaidi. Na kwasababu hiyo, fungamano hili humalizika pindi maslahi yanapotofautika, na huwagawanya watu, kwa sababu humalizika pindi maslahi yanapotimia…’
(Nidhamu ya Uislamu – Hizb ut Tahrir)
Yanayojiri sasa ni natija ya vurumai la uchaguzi wa mwaka 2015 na bashrafu (pasha pasha) ya uchaguzi ujao mwakani. Tofauti ya safari hii na miaka ya nyuma, ni kuwa vuguvugu la kambi hizi linadhihirika mapema zaidi, na hali hii ni kutokana na sababu tatu kubwa:
Kwanza, kambi iliyokuwa na nguvu mwaka 2015 iliyokuwa karibu na uhakika zaidi wa kufanikiwa kupata nafasi ya uraisi ilikosa nafasi hiyo katika dakika za mwisho mwisho. Hivyo, bado kambi hiyo ina hisia za machungu na maumivu makubwa ya kukosa hatamu.
Pili, baada ya kambi hiyo (yenye nguvu) kukosa iliekeza kwa hali na mali kuhakikisha ushindi katika kambi yenye hatamu sasa, ikitarajia kambi (iliyokuwa na nguvu) walau kutokana na jitihada yake itavuna makubwa katika utawala huu, ili ipate muda wa kujiandaa na kujipanga kwa uchaguzi mwengine. Kwa bahati mambo yamekwenda kinyume na matarajio ya kambi hiyo, si tu yamewaendea kinyume, bali wanahisi wamekuwa wakielekezewa tuhuma mbalimbali chafu zilizoratibiwa, kitu ambacho ndio msingi wa kilio chao.
Tatu, baadhi ya wachambuzi wanaona kwamba tuhuma zinazoelekezewa kambi hii (iliyokuwa na nguvu) ni sehemu ya uwepo wa khofu ya utawala wa sasa kwa kambi hii, hususan kutokana na nguvu yake na kwa kutilia maanani uzoefu wa yaliyojiri katika kinyan’ganyiro cha mwaka 2015.
Kwa upande wa dola ya Marekani ambayo ndio mlezi na bwana wa chama tawala cha CCM na serikali yake, inaonekana kuwa na utulivu kwa kuwa mgogoro huu ni wa kindani unaodhibitika. Inawezekana dola hiyo inauangazia kwa makini utafikia wapi. Aidha, inawezekana kuutumia mgogoro huu kutishia na kuweka aina fulani ya shinikizo kwa serikali ya sasa katika baadhi ya mambo ambayo inahisi haijanyenyekea vya kutosha.
Haitarajiwi mgogoro huu kuendelea kihivyoo, licha ya kuwa utaacha madonge na mafundo makubwa nyoyoni mwa wanakambi, na lau kama mgogoro huu utaendelea, matarajio kwa haraka Marekani kuleta sulhu baina ya kambi hizo, kuepusha kuja kutekwa nyara na Jumuiya ya Ulaya kupitia chama chao Chadema ili kudhoofisha athari, ushawishi na ubwana wake katika nchi yenye maslahi yake makubwa. Sulhu itakuwa amma, kuutaka utawala wa sasa kumega sehemu ya ngawira kwa kambi iliyo nje ya utawala, au kuiwacha mkono kambi iliyo nje ya utawala, ikiwa kambi inayotawala sasa itadhamini na kunyenyekea vilivyo juu ya matakwa na maslahi ya Marekani.
Huo ndio uhalisia wa siasa za kidemokrasia, siasa chafu ambazo watu wanapaswa kujiepusha nazo, siasa zilizogubikwa unafiki, kutafunana, sura mbili, matusi, ugeugeu, kudhalilishana, kuvuana uraia, kufedheheshana, mauaji, mateso, utekaji, ubaguzi wa kimaeneo, kimadhehebu na kidini ili tu kufikia au kuhifadhi maslahi fulani. Siasa hizi za kibepari zimekosa sifa ya kumsimamia mwanadamu, kwa kuwa hazijali thamani ya utu wala dini, bali dini yake ni ‘maslahi’.
Kwa bahati mbaya wafuasi na viongozi wa siasa hizi hujinasibu kwamba wako imara na wamefungamana pamoja juu ya vyama wanavyodai kwamba ni thabiti, ilhali ukweli kila mmoja katawaliwa na ajenda ya ‘umaslahi’ unaochochea chuki zisizokwisha, bughdha, husuma na uadui vifuani mwao.
تَحْسَبُهُمْ جَمِيعًا وَقُلُوبُهُمْ شَتَّى ذَلِكَ بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لاَ يَعْقِلُونَ (الحشر:
“…..Utawadhania kama wako pamoja, kumbe nyoyo zao ziko mbalimbali. Hayo ni kwa sababu wao ni watu wasio na akili” (59: 14)
Maoni hayajaruhusiwa.