Wanawake wa Kiislamu Bado Ujira Wenu Mkubwa

Mazingatio ya Ramadhani – 5

Suala la malipo kwa mwanadamu ni suala ambalo halina shaka kwa mwenye imani thabiti mbele ya Mola wake. Lakini kuna suala la kujiuliza hasa kwa akinamama na madada zetu kwa kuwa wao muda mwingi huwa na majukumu ya ndani ya nyumba zao tofauti na waume zao. Aidha, inadhihirika kuwa wanaume hupata muda mwingi zaidi wa kufanya ibada ziada jambo linaloweza kuleta hisia kuwa watapata darja kubwa mbele ya Allah Subhanahu Wataala. Ilhali wanawake wakaona, wao ni wenye nafasi ndogo tofauti na darja kama za waume zao au makaka zao.

Asma bint Yazid al-Answari (r.a) anatuelezea juu ya suala hilo. Siku moja alikwenda kwa Rasulullah Sallallahu Alaihi Wasallam na akamwabia:

“Ewe, Rasullullah! Wewe ni kipenzi kwangu mimi kuliko wazazi wangu. Wanawake wa Kiislamu wamenituma kama mwakilishi wao ili nije nizungumze nawe kwa niaba yao. Bila shaka wewe ni Rasulullah kwa wanawake na wanaume pia. Sisi hupitisha wakati wetu zaidi baina ya kuta nne za majumba yetu. Tumefungika katika wajibu wetu wa kutosheleza shahawa za waume zetu, kuwazalia watoto na kuwatunzia majumba yao. Licha ya haya yote, wanaume wanatushinda katika kupata thawabu kwa mambo ambayo sisi hatuwezi kuyafanya. Wao huenda msikitini wakaswali swala zao kwa jamaa kila siku, na pia swala ya Ijumaa kila wiki, wao huwazuru wagonjwa, huwenda mazikoni, wanakwenda hajj baada ya hajj, na juu ya hayo yote wao hupigana katika njia ya Allah (s.w).Wanapokwenda Hajj au katika Jihad, sisi huwatunzia mali zao tukawalea watoto wao na tukawashonea nguo zao. Je nasi hatupati sehemu katika thawabu zao?”

Mtume SAAW aliwaelekea Maswahaba waliokuwa pamoja naye, akasema: Jee mumewahi kumsikia mwanamke akiuliza swali bora kuliko hili ?”

Maswahaba ra. walimjibu:
“Ewe, Rasulullahi! Hatukufikiria kamwe kuwa anaweza kuuliza swali kama hili.”
Mtume SAAW akamwambia Asma :

“Sikiza kwa makini halafu nenda ukawaambie kwa wenzako wanawake waliokutuma, mwanamke akitafuta radhi za mumewe, na akazitekeleza kazi za nyumbani kwake mpaka mumewe akaridhika, anapata malipo sawa sawa na mume kwa ibada zote anazozifanya huyo mume.”

Nasaha hizi za Mtume SAAW ziondoshe hisia za unyonge wa akinamama juu ya uhafifu wa amali zao hususan ndani ya mwezi huu wa Ramadhani. Aidha, nasaha hizi zisiwe kisingizio cha wanaume kuwatwisha makazi mengi wake zao kiasi cha kuwakosesha fursa kujihusisha na ibada kwa kadiri inavyowezekana. Ni muhimu kuzipokea nasaha hizi kwa uzani na sio kuufanya mwezi huu ni wa kupikapika muda wote.

Tunamuomba Allah SW Katika mwezi huu mtukufu Atuokoe na moto na ahli zetu na Atuingize katika Pepo kwa Rehma zake , tuwe pamoja na wema waliotangulia na Mashahidi – Amiin

07 Ramadhani 1440 Hijri / 12 Mei 2019
Masoud Msellem
#RamadhanNaMuongozoWaQuran

Maoni hayajaruhusiwa.