Ushirikina Kamwe Haotuunusuru Ubepari
Karibuni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dr. Rehema Nchimbi aliripotiwa na mitandao ya kijamii akiomba baraka, neema na maendeleo ya mkoa wake wa Singida kupitia mnyama kakakuona aliyeonekana katika mkoa huo.
Mkuu huyo wa mkoa ameonekana katika video fupi kupitia mitandao hiyo ya kijamii kwa unyenyekevu mkubwa akimuomba mnyama huyo ambae kuonekana kwake huwa ni jambo la nadra alete maendeleo, neema, aondoshe ukame ikiwemo kutatua tatizo la maji katika mkoa huo.
Kwa bahati mbaya baadhi ya watu katika jamii ya Tanzania huamini kuwa, kuonekana kwa mnyama huyu adimu (kakakuona ) huambatana na kupatikana kwa neema, baraka na mafanikio.
La kusikitisha zaidi imani hii duni ya kishirikiana inayobwetesha wananchi sio tu iko kwa watu wa kawaida, bali kitendo hiki cha mkuu wa mkoa kinadhihirisha pia namna imani kama hiyo ilivyoota mizizi pia hata katika vifua vya wanasiasa katika jamii.
Kwa hakika jambo hili kwa upande mmoja ni dhihirisho la kuanguka kifikra kwa Ummah wakiwemo viongozi wao, yaani wanasiasa wake. Lakini pia wanasiasa wa kidemokrasia wakati mwengine hudandia imani kama hizi za kishirikiana kama mbinu ya kijanja kupoza raia, kujifariji na kukimbia majukumu baada ya kushindwa kutatua ipasavyo changamoto na dhiki za wananchi kivitendo , na badala yake hufungamanisha ufanisi wa kutatuka kero na shida hizo na imani za kishirikiana zisizokuwa na kichwa wala miguu.
Hali hiyo ni kutokana na uovu wa mfumo batil wa kidemokrasia unaotawala dunia leo kushikamana na fikra ya mwanafikra Machieveli inayosema: “fanya vyovyote ufikie lengo lako”. Hivyo, si ajabu wanasiasa wa kidemokrasia kutenda lolote kughilibu wananchi ikiwa jambo hilo litafikisha malengo ya kisiasa, imma ya kujikuza au kuficha udhaifu wao kisiasa na kiutendaji. Kwa hivyo, katika mfumo huo si kosa kwa mganga wa jadi kufanya shughuli zake kwa msaada wa ushirikina, ikiwa mfumo huo utanufaika kwa njia moja au nyengine.
Uislamu chini ya dola yake ya Khilafah utakabiliana na vitendo vyote vya ushirikiana, awali kwa kutatua matatizo ya raia na taabu zao kiasi kwamba raia wasichanganyikiwe na kukata tamaa kwa kujitumbukiza katika vitendo kama hivyo. Aidha, dola ya Kiislamu itajenga thaqafa thabiti ya Kiislamu kwa Ummah kujiepusha na kuzuiya vitendo hivyo. Kubwa zaidi itatumia mamlaka na nguvu yake ya kidola kukabiliana matendo ya ushirikina, kama inavyodhihirika katika tareekh ya Kiislamu.
Itakumbukwa kuwa dola ya Kiislamu chini ya makhalifa katika kufungua maeneo mbalimbali (fathi) ilikutana na changamoto za fikra hatari za kishirikina zilizokuwa na madhara wazi wazi kwa jamii, ilichokifanya ni kusimama kidete kuadhibu, kuzuiya na kukataza vitendo viovu vya kishirikina, kama ilivyodhihirika wakati wa Khilafah ya Umar bin Khattab (ra) ndani ya Misri.
Ilitokea raia wa Misri (maqbti) kutuma ujumbe maalumu kwa Gavana wa Misri, sahaba Amr ibn Ass kwa lengo la kumtaka ruhusa ya kumtoa muhanga kwa kumtumbukiza ndani ya Mto Nile binti wa kike ili kuuzuiya mto huo usikauke. Mila ya kishirikina iliyokuwa iliyokita katika jamii ya watu wa Misri kabla ya Uislamu, ambayo ikitekelezwa kila mwaka.
Ujumbe huo wa watu wa Misri ( Maqibti) ulimueleza Amr ibn Ass:
“Baada ya kupita nyusiku (nights) kumi na mbili za mwezi huu wa Juni (bowana) sisi humchukua binti mrembo kwa idhini ya wazazi wake na kumpamba kwa nguo nzuri na vito vya thamani, kisha humtumbukiza ndani ya mto, na baada ya hapo mto hufurika maji zaidi na zaidi kwa nguvu zote.”
Gavana Amr Ibn Ass (ra) alikawakatalia kutenda uovu huo kata kata, na akawaeleza kuwa Uislamu umebatilisha vitendo vyote vya mila na desturi za kishirikina zilizopita zama za ujahilia.
Ujumbe wa maqibti ukaondoka na kurejea makwao, na ikasadifu kuanzia siku chache Mto Nile ukaanza kupungua maji mpaka watu wakaanza kuhangaika na kuhama maeneo yao kwa dhiki ya maji na kuathirika shughuli za ukulima ambao ndio uti wa mgongo wa maisha yao.
Katika hali kama hiyo Amru Ibn Ass (ra) akaamua kumuandikia barua maalumu Khalifah Umar ra. kuhusu qadhia hii. Nae Khalifah Umar ra. akajibu barua ile:
“Umefanya sawa na umesema kweli kwamba Uislamu umebatilisha mila zote potofu na vitendo vya ushirikina vya zama za ujahilia. Pamoja na hayo naambatanisha barua ambayo iingize ndani ya Mto Nile’.
Barua ya Umar kwa Mto Nile ilisomeka hivi:
“Barua hii inatumwa kwa Mto Nile kutoka kwa Umar, Mtumwa wa Allah na Amiri wa Waislamu. Ewe Mto Nile! ikiwa maji yanajaa kwa matakwa yako binafsi, basi zuiya maji hatuyahitajii, lakini ikiwa maji yanajaa kwa matakwa ya Allah, basi Tunamuomba Yeye Ajaze maji katika mto”.
Baada ya barua hii kutumbukizwa mtoni, mto ulijaa maji mpaka kufikia mjao wa kima cha futi arubaini katika usiku uliotumbukizwa barua hiyo. Kuanzia hapo mila potofu ya kishirikina, ya kipagani, ya kishenzi na ya kikatili ya kumdhulumu binti asie na hatia kwa kisingizio cha kutoa muhanga ikakatika moja kwa moja.
Na katika upande wa kuwahudumia raia dola ya Kiislamu ya Khilafah daima inabeba jukumu moja tu la kuwatumikia na kuwasimamia raia kwa mambo ya ndani na nje. Katika kuliendea jukumu hilo daima dola hutafiti uhalisia wa tatizo na kulitatua kwa mujibu wa sharia. Masuala ya ushirikina hayana nafasi yoyote katika utatuzi wa matatizo hayo, wala hayazingatiwi kwa namna yoyote. Kwa kuwa tayari kuna muongozo kamili wa wahyi wa kumuongozea mwanadamu.
ثُمَّ جَعَلْنَاكَ عَلَى شَرِيعَةٍ مِنْ الأَمْرِ فَاتَّبِعْهَا وَلاَ تَتَّبِعْ أَهْوَاءَ الَّذِينَ لاَ يَعْلَمُونَ (الجاثية: 18
“Kisha tukakuweka wewe juu ya sharia ya amri, basi ifuate, wala usifuate matamanio ya wasiojuwa kitu”
(TMQ Al-Jaathiya: 18)
09 Jumada al-awwal 1440 Hijri | 15 -01- 2019 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.