Urusi ni Mbwa Mwitu Aliyejivika Ngozi ya Kondoo!
بسم الله الرحمن الرحيم
Tarehe 22 Oktoba 2018 kulifanyika Kongamano la Kwanza la Kijamii kati ya Urusi na Afrika (Russian-African Social Forum) lililoandaliwa na Muungano wa Dunia wa Masuala ya Kigeni ya Vyuo Vikuu vya Urusi na Afrika na Muungano wa Mipango ya Kibiashara ya Afrika, lilifanyika Moscow. Zaidi ya watu 500 walishiriki: watu maarufu kutoka Urusi na Afrika katika siasa na umma, wawakilishi wa kitaaluma, jamii ya wafanyibiashara na wawakilishi wa mashirika ya wanafunzi na vijana. Tukio hilo lilitoa nafasi maalum ya kubadilishana mawazo juu ya masuala ya kisasa kuhusiana na mahusiano kati ya Urusi na nchi za Afrika, hali ya sasa ya mahusiano na uwezekano wa kuzidisha maendeleo katika nyanja za kisiasa, kibiashara, kiuchumi, ubinadamu, vitengo vya kitamaduni pamoja na mengineyo. (Eurasia Review, 30/10/2018)
Mkutano huu umezidi kubainisha ‘usanii’ wa elimu ya kibepari na uhalisia wa ‘msaada/udhamini’ wa kielimu. Kwa kuwa washiriki wengi walikuwa ni wahitimu wa vyuo vya Urusi kwa miaka tofauti kutoka nchi mbalimbali, bila shaka wengi ni kutoka Afrika inaonesha namna ulivyo mfumo wa elimu duniani na natija ya ufadhili wa masomo.
Waziri wa Kigeni Sergey Lavrov alisema yafuatayo katika kauli yake ya ufunguzi wa Kongamano la Kijamii kati ya Urusi na Afrika: “Nchi yetu haikujipaka tope ya uhalifu wa ukoloni. Kinyume chake, ni kwamba ili wasaidia kwa kila hali, watu wa bara la Afrika katika kupata uhuru na ubwana wao kwa kuwapa misaada ya kuendelea na usaidizi katika kujenga mataifa yao na kumakinisha uhuru wa kiuchumi wa mataifa ya Afrika. Tunajivunia kufaulu katika ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi, kitamaduni na nyanga ningenezo.” (The Ministry of Foreign Affairs of the Russian Federation, 22/10/2018)
Nchi zilizoendelea hutumia nafasi ya ‘ufadhili’ wa kimasomo ili kuwapa thaqafa (fikra) na kuwaandaa wanafunzi hao kuwa visemeo vyao pindi warudipo makwao ili wasifie na kujivunia nchi wafadhili kwa kila chao na kushawishi ifunguliwe milango kwa ajili ya nchi wafadhili ‘kuwekeza’ na kujenga athari, kisha nao (wanafunzi) lau wakipata uongozi kuwa wakala wa wafadhili wao wa kielimu, imma kwa kudhamiria au kutodhamiria, kwa sababu akili zao ndivyo zilivyojengwa. Ndiyo ‘wasomi’ hao ambao la kwanza katika kubadilika kwao ‘kisomi’ ni kuiga tamaduni za nje na kudharau za kwao, hata kama kimsingi za kwao ndiyo bora.
Utamaduni huu unaotokana na athari za ufadhili wa kielimu unagongana na kauli au dhamira ya kuwaacha waafrika kutatua matatizo yao wenyewe. Kwani elimu hufahamika kuwa ni nyenzo muhimu kwa mwanadamu, lakini siyo elimu hii ya kuwalisha wanafunzi thaqafa/ustaarabu mgeni. Hatimaye wasomi hubakia kuwa wageni katika mazingira yao na hawaandaliwi kwa ajili ya kusaidia jamii zao kusonga mbele katika nyanja zote za maisha.
Kama alivyopata kunukuliwa Lord Macaulay, muasisi wa mikakati ya kielimu ya kimagharibi nchini India kwamba, “Ni lazima hivi sasa tufanye juhudi kubwa ili tujenge kikundi cha watu ambacho kitakuwa wafasiri wetu kati ya mamilioni tunaowatawala na sisi; kikundi cha watu ambao ni Wahindi kidamu na kirangi, lakini ni Wazungu kimtizamo, kimaoni, kimaadili na kiufahamu”
Ama kuhusu Urusi kuwa inaheshimu haki za binadamu tena za kidemokrasia halisi, hilo ni uwongo! Kihistoria katika zama za Ukomunisti, Urusi imesheheni historia ya kikatili na mauwaji ya mamilioni, kukandamiza dini, kudhulumu na kukandamiza raia kwa jumla. Na leo inaminya wapinzani wake, kuingilia masuala ya nchi jirani kama Ukraine, kuendelea na mauwaji ya kikatili ya wanawake, wazee na watoto nchini Syria bila ya kutaja dhulma na mateso wanayopata walinganiaji wa Uislamu nchini mwake wakiwemo walinganizi wa Hizb ut Tahrir waliobeba fikra angavu na kuukosoa mfumo batili wa kidemokrasia kwa njia ya fikra tu!
Ama kuhusu maendeleo ya Afrika, tatizo kubwa leo hii ni tatizo la kiaidiolojia/ kimfumo ambao hujenga na kuathiri mtazamo na mwendo wa mtu na taifa juu ya maisha. Urusi kwa sasa wamebaki kuwa wajamaa kinadharia tu, lakini ni mabepari katika mipango, mikakati na kimatendo. Matatizo yanayoikabili Afrika ndiyo hayo hayo kwa nchi zote duniani, ambayo ni kutokana na kutawaliwa na mfumo wa Ubepari.
Itawezekana vipi utatuzi huo wakati Urusi na madola mengine ya kibepari ya kikoloni wanapora usiku na mchana rasilimali za Afrika kama madini, kisha kuwaachia waafrika mashimo tu?! Aidha, itawezekana waafrika watatue matatizo yao ya Afrika ilhali wasomi wao ambao ndio tegemeo msingi na nyenzo muhimu katika juhudi hizo, wameshaharibiwa akili kwa kuandaliwa kinadharia zaidi, tena kwa manufaa ya wafadhili (Urusi)?!
Itawezekanaje kutatuka matatizo ya Afrika ilhali matatizo hayo na ya nchi nyengine changa ni mtaji na fursa kwa ustawi wa Urusi na nchi za kibepari jumla?! Kattu mataifa ya kimfumo wa kibepari hayapo na hayatakuwa tayari kuona ‘makoloni’ yao yakiimarika. Wameondoka kimwili lakini kimikakati bado wanakoloni. Viongozi wa nchi za Afrika ni vibaraka wao, wasomi ni visemeo vyao na wabeba agenda zao za maangamizi.
Ama kuhusu matamshi ya Waziri wa Kigeni wa Urusi kwamba Nchi yetu haikujipaka tope ya uhalifu wa ukoloni, ni dalili ya kibri na kuonesha wazi kwamba mkutano wao una lengo na ajenda ya kikoloni ili kuendeleza kupora rasilimali watu na vitu kwa ustawi wa nchi yao. Hawana lengo la utu, msaada, huruma wala mashirikiano ya dhati, zaidi ya muendelezo wa ukoloni mambo leo kwa sura ya kijanja. Sio ujamaa ulioanguka wala ubepari unaotawala leo hii ina uwezo wakutatua matatizo ya wanaadamu katika nchi yoyote. Mifumo hii ni tatizo mama na kamwe sio suluhisho, na yanayotangazwa kuwa ni matatizo ni matokeo na viashiria vya tatizo hilo.
Kwa leo, mfumo unaotawala wa kibepari kiasili unapuuza nafasi ya Mwenyezi Mungu Muumba, na badala yake unatukuza (kiumbe) akili ya binadamu kufikia kuiona kuwa inaweza kupangilia maisha yao kikamilifu na kwa usahihi kabisa. Pamoja na maendeleo yote ya kisayansi hayajawaongoza kuona na kukiri udhaifu wa mwanadamu kama kiumbe na kwamba hastahiki kujipangia namna ya kuishi bali anahitaji mjuzi zaidi ampangie na kumsimamia. Naye ni Mwenyezi Mungu.
Kupinga nafasi ya Mungu ndiko kunakoondoa utu katika nyoyo na mabongo ya binadamu na hatimaye kuzua vurugu na machafuko. Yakapatikana matabaka ya mabwana na watwana. Mabwana wakawa na maisha yao ya kuthamini zaidi mbwa wao, na kuacha binadamu wenzao (watwana). Watu wakauana ili kujiongezea mali (maslahi) kwani hilo ndiyo ‘heshima’ katika mfumo wa kibepari.
Suala kwa upana wake sio waafrika kwa Afrika yao, bali iwe walimwengu kwa Ulimwengu wao. Na utatuzi wa kweli na wa ufanisi haupatikani ila kwa kuondoa mfumo wa kibepari na kuweka mfumo mbadala, sahihi na kamili wa kuongoza maisha ya binadamu. Nao ni Uislamu pekee. Kama ulivyoshindwa ujamaa, na ubepari nao uko mahututi na unaendelea kuzalisha matatizo kila uchao.
Ni wakati sasa kuipa nafasi aidiolojia/ mfumo wa Kiislamu ili ustawishe jamii ya wanadamu bila ya kujali maeneo wala rangi zao. Na hili ni marudio tu, kwani historia inaushuhudia Uislamu kuwa ndio mfumo pekee bora uliowatawala wanadamu kwa muda mrefu na kwa mafanikio makubwa katika nyanja zote za maisha.
Hamza Sheshe
Mwanachama wa Hizb ut Tahrir Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.