Kizaazaa Cha Wimbi La Utekaji Nchini Tanzania
Habari:
Vyombo vya habari vya Tanzania na kimataifa vimearifu juu ya kutekwa Mohammed Dewji (43), bilionea kijana zaidi Afrika , nje ya hoteli ya kifakhari akiwa katika ratiba zake za kawaida za kufanya mazoezi asubuhi.
Maoni :
Kutekwa Mohammed Dewji kumetokea katika eneo lenye hadhi na ulinzi mkali, karibu na makazi ya viongozi waandamizi wa nchi. Eneo lenye walinzi na kuangaziwa kwa uwepo wa kamera zaidi ya 30 za kufuatilia matukio. Tukio hili linaacha maswali mengi kuliko majibu kuhusu hali ya ulinzi na usalama katika Tanzania.
Katika miaka ya hivi karibuni kumezuka wimbi kubwa la utekaji na mauaji ya raia wa kawaida, wanasiasa, watu mashuhuri , wafanyabiashara, waandishi wa habari nk. huku tukio hili la mfanyabiashara huyu mashuhuri likiangaziwa kwa upana na kusikika zaidi kuliko yaliyotangulia.
Mbali na kutekwa Dewji, baadhi ya matukio ya utekaji yaliyotokea miaka ya karibuni ni pamoja na kutekwa Ben Saanane, miongoni mwa viongozi waandamizi wa upinzani, Azory Gwanda, mwandishi wa habari katika Mkoa wa Pwani, mkoa ambao mamia ya watu wamenyakuliwa, kutoweka na hawajulikani walipo kwa mujibu wa Mbunge wa upinzani Zitto Kabwe.
Pia kumetokea utekwaji wa wafanyabishara kama Samson Josiah na Peter Zakaria, wanachama watatu wa Hizb ut Tahrir waliotekwa mwaka jana kisha kutelekezwa, achilia mbali kutoweka raia na kuokotwa miili ya watu katika fukwe za bahari ya Hindi katika mkoa ya Pwani na Dar es Salaam, na matukio mengine ambayo hatukuyataja hapa. Yote haya yanaonesha mapungufu na kushindwa kwa vyombo vya usalama kulinda maisha, mali na utu wa raia.
Watekaji wowote watakaokuwa, na kwa malengo yeyote waliyonayo, hapana shaka kwamba mfumo wa ubepari unajifedhehi na kudhihirisha kushindwa kuwatumikia na kuulinda ubinadamu ipasavyo, kiasi hata cha kuruhusu uwepo wa magenge ya kiharamia ndani na nje ya vyombo vya usalama. Amma uwepo wa magenge hayo ndani ya vyombo vya dola, hilo limewahi kutamkwa na Mbunge Hussein Bashe mbele ya bunge kuwa “ kuna watekaji ndani ya vyombo vya dola ”(Zanzibar24, 10/04/2017).
Kwa upande mwengine, katika suala hili la kutekwa Dewji, licha ya vyombo vya ulinzi na usalama kutoa matamko yasiyokinaisha, pia vimeonesha hisia za kiubaguzi kwa kujali zaidi matajiri. Lau Dewji asingekuwa bilionea, juhudi zingekuwa hafifu au zisingekuwepo kamwe kuhusu mahala alipo. Mfano mzuri ni kuwa mpaka sasa hakuna maelezo ya kutosha kwa Ummah kuhusu kutoweka kwa wengi, na kuokotwa miili ya watu katika Mto Ruvu na fukwe ya “Coco” katika Bahari ya Hindi.
Wakati tukitoa pole za dhati kutoka nyoyoni mwetu kwa familia, ndugu, na marafiki wa Dewji na jamii kiujumla kwa tukio hili. Pia tunatoa mwito kwa jamii kuwa na tafakuri na kuibua mjadala kuhusu mfumo mbadala kando na ubepari. Mfumo utakaoleta amani, usalama na kudhamini kinga kwa raia wote bila ya kuzingatia asili, utajiri au dini zao. Bila ya shaka ni Uislamu pekee chini ya dola ya Khilafah ndiyo wenye sifa ya kuyatenda hayo.
Imeandikwa na Said Bitomwa.
Mjumbe wa Afisi ya Habari, Hizb ut Tahrir Tanzania.
Kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir.
Maoni hayajaruhusiwa.