Janga la Bir-Ma’un: Dua Bega kwa Bega, Siasa na Jeshi.
Moja katika matukio ya kuhuzunisha katika tareekh ya Uislamu ni janga la mauwaji ya Waislamu katika eneo la Bir-Ma’una (Kisima cha Ma’una). Mauwaji haya yaliotokea katika zama za Mtume SAAW ndani ya mwezi kama huu wa Safar (4 Hijri).
Ikumbukwe kwamba siku chache kabla ya janga hili pia makafiri wa Banu Lihyan walitenda mauwaji kama haya (Ar-Raji)’. Makafiri walitaka kupatiliza mtihani wa Waislamu kushindwa katika Vita vya Uhud ili kuwadhoofisha na kuwamaliza kabisa.
Mauwaji ya Bir- Ma’una yalijiri baada ya Abu Bara wa kabila la Bani Amir kumtaka Mtume SAAW ampatie masahaba wake wakahubiri dini katika eneo lao la Najd. Mtume SAAW alisitasita juu ya usalama wa masahaba wake lakini Abu Bara akamuahidi kulinda usalama wao.
Kuna kauli kwamba masahaba hawa walikuwa 40 au 70, na takriban wote walikuwa wanavyuoni, mafuqaha na mahafidhul Quran wakubwa.
Kwa ufupi msafara huu ulikuwa timu nzito ya wataalamu. Kiongozi wa msafara alikuwa Al-Mundhir bin ‘Amr Ra. Ansar wa kabila la Banu Sa‘ida. Walipofika eneo la Bir-Ma’una (Kisima cha Ma’una) walimtuma mjumbe maalumu, kupeleka risala maalum ya Mtume SAAW kwa mmoja miongoni mwa viongozi wa kabila la Bani Amir.
Amir bin Tufayl, kiongozi wa kabila hilo alikataa hata kuisoma risala hiyo tukufu na akaamrisha mjumbe apigwe mkuki na kuuwawa. Hapo hapo Amir bin Tufail, kwa haraka sana akakusanya kabila lake na mengine ili kuwapiga Waislamu. Kabila la Bani Amir lilikataa kuingia katika medani ya vita kwa kuzingatia kuwa Abu Bara alikwishachukua dhamana kwa Mtume SAAW kuwalinda masahaba zake .
Bwana Amr bin Tufail, hakuvunjika moyo akachukua usaidizi wa Kabila jingine la Bani Salim na makabila mengine kuwashambulia Waislamu. Msafara wa masahaba ukawa hauna namna ila kupigana mpaka wakafa mashahid takriban wote isipokuwa mmoja Ka‘b bin Zaid bin An-Najjar Ra. ambae alidiriki kurejea Madina akiwa kajeruhiwa.
Mtume SAAW alihuzunishwa sana kwa khiyana na mauwaji haya mawili ya Bir Ma’una na yale ya awali ya Ar-Raji. Kwa kuwa mauwaji haya hayakuwa ni vita kiudhati bali ni khiyana tu ya makabila, lakini pia si tu Mtume SAAW alipoteza masahaba zake, bali alipoteza wanavyuoni wakubwa.
Bila ya kuchelewa Mtume SAAW akiwa mwanasiasa thabiti na kiongozi jasiri akachukua hatua za kisiasa, kiibadat na kijeshi kukabiliana na hali hiyo. Akapata maelezo ya kina juu ya tukio hili kutoka kwa Amr bin Umayyah ambae alikuwa karibu na eneo lilipotokea. Kiibadati aliomba dua kali kwa siku 30 kumkabili Mola, Mwenye Nguvu dhidi ya uovu, khiyana ya makabila haya.
Hatimae, miezi michache katika mwaka ule ule wa 4 Hijria baada ya kumaliza kuwapiga na kuwatimua mayahudi wa Bani Nadhir, Mtume SAAW akatuma jeshi Najd kupambana dhidi ya makabila haya na mengineyo ili kukomesha maonevu, dhulma na usaliti wao.
Safar 4 AH
Maoni hayajaruhusiwa.