Mafunzo Kutoka Ndoa Ya Fatma Bint Rasulullah

بسم الله الرحمن الرحيم

Miezi miwili baada ya ushindi wa Waislamu katika Vita vya Badr, Imam Ali Ra. na Bi Fatma
Zahra Binti wa Mtume SAAW walifunga ndoa. Ilikuwa katika mwezi wa Dhul-Qaadah mwaka wa pili Hijria wakati Imam Ali Ra alipomchumbia Bibi Fatma Ra. kwa kumkabili Mtume SAAW na kumueleza:

‘Ewe Mtume wa Allah, umenilea mimi kama mwanao mwenyewe. Ulinijaza na zawadi zako, ukarimu wako na wema wako. Nimepewa nawe kila kitu katika maisha yangu. Sasa naomba wema mmoja zaidi kutoka kwako’.

Mtume SAAW alifahamu kwa kina lengo la Imam Ali Ra. na akawa hana budi ila kumueleza mwanawe Bi Fatma kwamba Ali alikuwa anaomba uchumba kwake, na kumtaka jibu lake. Lakini Fatma Zahra Ra. akabakia kimya bila ya jibu lolote, na Mtume SAAW akatafsiri kimya chake kwamba kakubaliana na posa hiyo. Akarudi Mtume SAAW kumjuulisha Ali Ra. kwamba ombi lake limekubaliwa. Na akamtaka aanze kufanya matayarisho ya harusi.

Maandalizi ya harusi yakafanywa, na Mtume SAAW akamkabidhi shughuli yote ya harusi kwa upande wa wanawake kusimamiwa na ‘nyanya’/bibi yake aliyekuwa akiitwa Ummu Ayman.

Mwanzoni mwa mwezi wa Dhul-Hijjah katika mwaka wa 2AH Mtume aliwaalika Muhajirina na Answar kuhudhuria katika shughuli ya harusi. Mtume SAAW mwenyewe akatoa khutba ya ndoa, akawaozesha na akawatangaza rasmi Ali Ra. na Bibi Fatma Ra. kwamba tayari wameshakuwa mke na mume.

Wageni waalikwa waliandaliwa na Mtume SAAW karamu ya nyama ya kondoo, mikate na maji ya tende na maziwa (juice). Waislamu wakala, wakanywa, wakafurahi na wakampongeza Mtume SAAW na maharusi katika tukio hili tukufu lililojaa baraka tele. Kadhalika Mtume SAAW akaomba baraka za Allah ziwe juu yao wote.

Siku chache baadae, ndani ya mwezi huu huu wa Dhul-hijjah, Bibi Fatma akaiga nyumba yao aliyokuwa akiishi na kupelekwa nyumbani kwa mumewe. Bibi Fatma akasaidiwa na Baba yake kupanda juu ya ngamia maalum kuelekea nyumbani kwake.
Katika siku hiyo, mji wote wa Madina ulijaaa furaha, nderemo, vifijo, hoihoi na kuririma kwa ‘takbeer’. Salman al Farsi alishikilia hatamu za ngamia wa Bibi Harusi (ambae alikuwa ngamia jike wa Mtume SAAW) akaongoza msafara huku akisoma aya tukufu za Quran, Mtume SAAW nae alitembea upande mmoja wa msafara, na upande wa pili alikuwepo Ami yake Hamza Ra. (Bwana wa Mashahid).

Masahaba jumla na vijana wapanda farasi wa Bani Hashim walipanda farasi kama wasindikizaji wa bibi harusi. Huku panga zao zikimeremeta na kunyanyuliwa juu kwa furaha isiyo na kifani. Nyuma yao wanawake wa Muhajirina na Answar wakiimba qasida nzuri nzuri katika maandamano yaliyozunguuka Msikiti wa Mtume (Masjid Nabawi) na yakafikia kilele chake chini ya nyumba ya maharusi.

Baada ya kushuka Bi harusi juu ya ngamia wake, Mtume SAAW akaushika mkono wa Bi Fatma Ra. na kuuweka juu ya mkono wa mumewe, akasimama juu ya kizingiti cha nyumba yao na kuwaombea dua:
‘Ewe Allah ninawaweka Ali na Fatma, waja wako wanyenyekevu, kwenye ulinzi Wako. Uwe Wewe ndio Mlinzi wao. Wabariki hawa, Kuwa radhi nao, na uwape neema Zako zisizo na mipaka, huruma, na fadhila Zako bora juu yao. Uifanye ndoa yao kuwa yenye matunda, na uwafanye wote imara katika upendo Wako, na ibada zako.’

Pamoja na mafunzo mengi yaliyomo katika tukio hili kubwa, funzo moja kubwa na muhimu linadhihirika wazi wazi. Namna Mtume SAAW alivyoondosha fikra chafu ya uaswabia na ubaguzi kwa vitendo kwa kuwashirikisha kikamilifu na mstari wa mbele masahaba wasiokuwa waarabu wala Bani Hashim katika tukio hili. Hilo hudhihirika katika hali mbili:

Kwanza, Mtume SAAW alimpa jukumu nyanya (bibi) yake Ummu Ayman Ra. kusimamia shughuli ya harusi hii. Bibi huyu mtukufu ni mwanamke mwenye asili ya kihabeshi (Ethiopia), awali alikuwa mtumwa wa baba yake Mtume SAAW, na baadae Mtume SAAW akampa uhuru wake.

Itakumbukwa kwamba bi Ummu Ayman kwa mujibu wa kauli ya Mtume SAAW atakuwa miongoni mwa watu wa peponi. Lakini pia ndie mwanamke aliyekuja kuolewa na sahaba mkubwa Zaid bin Harith Ra. na kumzaa shujaa katika mashujaa wakubwa wa Kiislamu (Usamah bin Zaid). Kijana ambaye nae pia Mtume SAAW alimpa jukumu la ujemadari wa jeshi la Kiislamu bila ya kuzingatia kabila wala nasabu yake, na kuwaacha Waislamu wenye makabila makubwa ya kiqureish.

Pili, Mtume SAAW namna alivyomchagua Salman Al Farsi kuongoza msafara wa Bi harusi bila ya kumzingatia kwamba yeye si muarabu. Bali alimpa hadhi hiyo kwa moyo mkunjufu bila ya kuonyesha hisia yoyote ya kibaguzi.

Salman RA. awali kabla ya kusilimu aliwahi kuwa mtumwa katika viunga vya Madina akakombolewa baada ya kusilimu kwake. Uislamu ukampandisha daraja ya juu hadi siku moja ‘Muhajirina’ na ‘Answar’ walipozozana juu ya haiba yake, wengine wakisema Salman ni ‘Answar’ na baadhi wakisema ni katika ‘Muhajirina’. Mtume akaondosha mzozo wao huo kwa kusema:
‘Salman ni katika Ahul-bayt yangu’.

Leo Umma wa Kiislamu umesibiwa kwa kiasi kikubwa na uchafu na uovu mbaya wa uaswabia na ubaguzi, kuanzia wa kimaeneo, kikabila, rangi, nchi nk. Uchafu ambao Mtume SAAW alisema wazi kwamba ni ‘uvundo’ na tujiepushe nao. Na kipimo pekee cha kumzingatia mtu kwa ni kwa mujibu wa ucha Mungu.

Tukumbuke kauli yake Mtume SAAW aliposema:

Kwa hakika watu wote tangu zama za Adam mpaka leo wako sawa kama meno ya kitana, na hakuna ubora juu ya Muarabu kwa asiyekuwa Muarabu, wala hakuna ubora wa Mwekundu kwa Mweusi, ila kwa ucha Mungu.’
(Mustadarak- ul-Wasa’il)

#UislamuNdioMfumoSahihi

Masoud Msellem

Maoni hayajaruhusiwa.