Marekani Haistahiki Kuifundisha Afrika kuhusu Mamlaka Kamili

1

Habari:

Vyombo vya habari vya kimataifa vimeangazia juu ya ziara ya karibuni ya Waziri wa Nje wa Marekani Rex Tillerson (aliyekwishafukuzwa kazi karibuni) ndani ya Mashariki na Magharibi ya Afrika ambapo katika kisimamo chake nchini Ethiopia alilionya bara la Afrika juu ya athari kubwa na ya hatari ya kiuchumi kutoka kwa China juu ya bara la Afrika, hali inayopelekea Afrika kubakia tegemezi  na kukabiliwa na hatari ya kupotea mamlaka yake kamili.

Maoni:

Kwa mtazamo wa haraka  juu ya nchi tano zilizochaguliwa katika ziara hiyo ya Tillerson ndani ya Afrika inathibitika kwa mtazamo wa wazi kabisa kwamba kipaumbele cha kimaslahi ilicholenga Washington ndani ya Afrika ni suala la usalama, na wala Marekani haikulenga kuipatia chochote Afrika wala haikusukumwa na  hali ya kujali kupotea mamlaka kamili kwa bara la Afrika.

Bara la Afrika lilipoteza mamlaka yake kamili mara tu ulipoibuka ubepari, na tangu wakati huo halijaweza kuyarejesha, licha ya nchi zake kwa sasa kuwa na nyimbo za kitaifa,  sarafu ya kitaifa, bendera za kitaifa na siku za kitaifa, hayo yote hayatoshelezi kuwa  ndio sifa ya kuwepo mamlaka kamili kwa ukamilifu wake.

Wakati ubeberu wa Ulaya ulipoibuka ndani ya karne ya 19, ulikuja bega kwa bega na ajenda ya kukandamiza nchi na wazawa, kuhodhi kwa nguvu mamlaka ya kisiasa, unyonyaji wa kiuchumi, ubaguzi wa rangi, na hatimae kupelekea kuligawa bara la Afrika kuwa  ukanda  wa unyonyaji wao wa maliasili zake kama maadini, mazao ya kilimo, malighafi, nguvukazi na  kunyakuwa kwa kuyakalia kiuvamizi maeneo ya kistretejia (nyeti)  kwa ajili ya kudhamini na kulinda athari zao. Hali hizo pia zilijiri ndani ya mabara ya Marekani na Asia.

Madola ya kibepari yalipokita vilivyo, yalinyonya marundo ya rasilmali zake (Afrika) na walipovamia kwa ukoloni wa moja kwa moja hawakusita kuwapa majukumu kwa niaba yao watawala wa asili wa  baadhi ya maeneo, huku nyuma ya pazia watawala hao wakisimamiwa na maafisa wa kikoloni. Mfano hai ni utawala wa Usultani wa Zanzibar, Utawala wa Buganda, Utawala wa Sokoto (Nigeria) nk. Madola ya kibepari yalitenda mbinu hiyo ili kufikai malengo yao kiurahisi.

Kuibuka kwa vuguvugu la kudai uhuru na kutaka kujiamulia mambo kwa nchi mbalimbali  hususan baada ya Vita vya Pili kuliambatana na  kaulimbiu ya  kupigania kurejesha mamlaka kamili ya kitaifa. Mwito huo wa kupigania uhuru ulipigiwa tarumbeta na kupazwa sauti yake juu na wanaoitwa wapigania uhuru. Hata hivyo, kampeni hii ya kupigania uhuru kwa uhalisia wake ilikuwa ni mpango na mkakati wa Marekani na Umoja wa Kisovieti kusahilisha ajenda yao ya kuutwaa ubwana wa ulimwengu kwa kutia mkononi makoloni ya Uingereza na Ufaransa. Kwa vile Marekani kwa wakati huo ilikwishaibuka kuwa dola yenye nguvu baada ya Vita vya Pili, vita vilivyodhoofisha na kuathiri sana madola ya Uingereza na Ufaransa. Amma dola ya Umoja wa Kisovieti ikiwa dola mpya yenye mfumo, nayo pia ilikuwa na shauku inayochemka kuwa na nafasi katika uwanja wa kimataifa. Mwito wa kudai uhuru (kujiamulia mambo) ulikumbatiwa na kupokewa kwa vishindo na Umma ndani ya bara la Afrika na Asia, Umma ukiwa na tamaa ya  kupata uhuru wa kweli na mamlaka kamili kutoka kwa wakoloni, kitu ambacho kamwe hakijatokea.

Hali ya sasa ya ukoloni mamboleo imezidi kuwa mbaya zaidi tangu kusambaratika dola ya Muungano wa Kisovieti, ambapo leo Marekani ndio bwana mkubwa zaidi katika uwanja wa kimataifa, ilhali dola ya Uingereza na Ufaransa zikibakia kuwa na ushawishi mdogo. Leo Marekani hulazimisha matakwa yake kwa kila taifa, iwe upande wa kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na upande wa kijeshi, kiasi cha kuweka vituo vyake vya kijeshi kila mahala ndani ya Afrika vilivyomiminiwa zaidi ya wanajeshi 6,000 barani Afrika. Marekani inatenda hayo yote bila ya kujali wala kutia maanani kuathiri mamlaka kamili ya nchi yoyote.

Onyo la Marekani kuhusu Afrika kupoteza mamlaka yake ni tusi, lililosheheni dharau na kebehi kwa bara la Afrika, na kwa hakika Marekani haina uhalali wa kutoa kauli kama hiyo,  kwa kuwa inalifanya bara la Afrika kama bustani ya nyumbani, Marekani hunyonya itakacho, kwa muda itakao, na kwa kiwango itakacho. Bila ya kutaja katika sekta ya kisiasa ambapo huamrisha na kulazimisha matakwa yake kwa watawala wa Afrika kama watumwa wake. Ati kisha Marekani ina uhalali na ujasiri wa kuionya Afrika ilinde mamlaka yake yasipotee !

Afrika na ulimwengu wa tatu kwa jumla inahitaji mfumo wa insafu na uadilifu, nao ni Uislamu chini ya kivuli cha dola yake ya Khilafah Rashidah, dola hiyo itadhamini uhuru wa kweli na mamlaka kamili, kinyume kabisa na ubepari, mfumo muovu na wa maangamizi. Wakati umefika kuwendea Uislamu na kuachana kabisa na Ubepari.

Imeandikwa na Masoud Msellem

Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari

Hizb ut Tahrir Tanzania

Kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

1 Comment
  1. Clint-B says

    I like this web site very much, Its a very nice billet to read and get info.Blog monry

Leave A Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.