25 Ramadhan

بسم الله الرحمن الرحيم

1. Siku kama hii 25 Ramadhan 658 Hijria /1260 miladi, Waislamu waliwashinda Matatar (Mongols) katika Vita vya Ain Jalut chini ya uongozi wa Saif ad-Din Qutuz katika maeneo ya Palestina.

Ushindi huu ulijiri kuwa faraja kubwa kwa Waislamu baada ya uvamizi wa kutisha wa jamii hiyo ya Mongols ndani ya mwaka 656 Hijria ambapo waliuwa na kumwaga damu ya Waislamu kwa malaki, kuleta uharibifu mkubwa katika maeneo mengi ya Waislamu na kuupindua kabisa Ukhalifa katika mji wa Baghdad.

2. Siku kama hii 25 Ramadhan 8 Hijria lilivunjwa sanamu la Al-Lat eneo la Taif kwa watu wa kabila la Bani Thaqif.
Mtume SAAW alituma kikosi maalumu chini ya uongozi wa Jemadari Khalid ibn Walid kwenda kutekeleza jukumu hilo.

Uvunjaji huo ulitokana na ujio wa ujumbe maalum wa kabila la Bani Thaqif kwa Mtume SAW na kisha kusilimu. Baada ya kusilimu watu hao wakatoa masharti kadhaa ikiwemo kuruhusiwa kuzini, kulewa, kuachwa sanamu lao la Al-Lat nk.

Masharti yao yote hayakukubaliwa, ila Mtume SAAW katika suala la kuvunja sanamu lao, kwa kuwa kabila hilo walionekana kuwa na khofu ya kulivunja kwamba watadhurika, ndio SAAW akatuma kikosi hicho maalumu kufanya kazi hiyo.

Kikosi hicho kikavunja sanamu hilo lilikuwa limejengewa juu ya msingi ambao chini yake kulikuwa na vito mbali mbali vya thamani, zikachukuliwa mali hizo na kupelekewa Mtume SAAW akazigawa kwa Waislamu.

3. Siku kama hii 25 Ramadhani mwaka 544 Hijria / 1150 AD, alizaliwa mwanachuoni mkubwa Mohammed ibn Umar, ibn Al Husayn at-Taym Fakhr al-Din al-Razi.

Al-Razi alizaliwa katika maeneo ya Amol (Tabaristan – Iran) kutokana na familia ya kiarabu ya kiqureishi waliohamia maeneo hayo.

Aliibuka kuwa mwanachuoni wa kupigiwa mfano katika fani mbali mbali ikiwemo fiqhi, tafsiri nk. Ameandika vitabu zaidi ya mia moja, maarufu zaidi katika vitabu vyake ni tafsiri yake ya Quran Tafsir al-Kabir ( Mafatih al-Ghayb )

Al-Razi alifariki dunia akiwa na miaka kama 61 katika maeneo ya Herat, Afghanistan.

4. Siku kama hii 25 Ramadhani 532 Hijria, Khalifa Haroun Ar-Rashid aliuwawa ( kauli nyengine alikufa kimaumbile)

Ar-Rashid alizaliwa baina ya miaka (148–193 Hijri, katika mji wa Ray (sehemu ya Tehran leo) alikuwa Khalifah wa tano katika Khilafah ya Abassiya

Al-Rashid alitawala katika zama za kilele katika elimu na maarifa kwa Umma wa Kiislamu. Yeye binafsi aliekeza sana katika kukuza elimu na maalumat kwa Umma wa Kiislamu kwa kuwatunza ipasavyo wanavyuoni, kuasisi vituo vikubwa vya kielimu, ikiwemo Maktaba kubwa inayoitwa Bayt al-Hikma (“Nyumba ya Hekma”), na kuufanya mji wa Baghdad, kuwa kituo kikubwa na muhimu kielimu ulimwenguni.

Katika utawala wa Al-Rashid, dola ya Ufaransa iliasisi urafiki na mahusiano mema na dola ya Kiislamu kiasi cha kuleta ujumbe maalumu kwa Khalifah Al-Rashid. Uliporudi ujumbe huo wa Ufaransa, Khalifa Al-Rashid aliwapa zawadi maalumu ikiwemo saa ili wafikishe kwa mtawala wa Ufaransa (Charlemagne). Mtawala wa Ufaransa alipopokea saa hiyo alishangaa na kustaajabu sana kutokana na teknolojia ya hali ya juu iliyotumika kutengeneza ya saa hiyo, iliyokuwa ikitoa sauti kila inapoingia saa.

Al-Rashid alifariki akiwa na miaka 43 na kuzikwa Mashhad, Iran

5. Siku kama hii 25 Ramadhani 1398 Hijria / Agosti 1978 alitoweka Sheikh Imamu Mussa Sadr, ndani ya mji wa Tripoli, Libya. Imam Mussa Sadr alikuwa ni mtu maarufu na mwanachuoni mkubwa wa madhehebu ya Jaafariya ndani ya Lebanon.

Imamu Mussa Sadr akiwa na wenzake wawili Sheikh Muhammad Yakoub na mwanahabari Abbas Badreddine walikuwa na ziara nchini Libya kwa mwaliko wa Raisi wa Libya Muammar Gaddafi. Mara ya mwisho kuonekana watatu hao ilikuwa tarehe 31 August 1978, baada ya hapo hawakuonekana tena mpaka leo.

Inaaminika kwamba waliuwawa na serikali ya Libya kwa agizo la Gaddafi, mizigo ya Imamu Mussa ilikutikana katika hotel moja mjini Tripoli na hakuna ushahidi wa watatu hao kusafiri kuondoka Libya.

Masoud Msellem

Maoni hayajaruhusiwa.