14 Ramadhan 1441 H

بسم الله الرحمن الرحيم

1. Siku kama leo 14 Ramadhan 67 Hijria/ 3 April 687 alifariki dunia Tabiin mashuhuri kutoka Taif, kwa jina ni Al-Mukhtār bin Abī ʿUbayd al-Thaqafī ambaye alisimama kidete dhidi ya uasi, na kutetea Khilafah ya Imamu Hussein kwa nguvu zote ilipotokea fitna ya uasi.

Babu wa Al-Mukhtar ni Mas’ud al-Thaqafi aliyekuwa katika watu mashuhuri ndani ya Hijaz na Taif, na watu walikuwa wakimwita (Azim al-Qaryatayn/ mtukufu wa miji miwili.

Baba yake Al Mukhtar ni Abu ‘Ubayd al-Thaqafi, sahaba mashuhuri wa Mtume SAAW aliyekufa shahid katika zama za Khilafah ya Abu Bakar katika Vita vya Al-Jisr. Aidha, katika vita hivyo pia walifariki kaka watatu wa Al Mukhtar nao ni Wahb, Malik, na Jibr.

Al-Mukhtar aliuwawa katika mwaka 67 Hijria /687 miladi na kuzikwa katika mji wa Kufa, Iraq, kaburi lake lipo karibu na Msikiti mkubwa wa Kufa

 

2. Siku kama leo 14 Ramadhan 14, 1414 Hijri / 25 Februari, 1994 kulitendeka mauwaji makubwa katika mji wa Al-Khalil, Palestina. Gaidi, mlowezi wa kiyahudi mwenye asili ya kimarekani Baruch Goldstein aliuwa Waumini wa Kiislamu wasiopungua 29 wakati wakiwa msikitini katika swala ya Alfajiri ndani ya Masjid Ibrahim.

Baruch Goldstein alifanikiwa kupanda juu ya msikitini hapo ikisemekana kwa kupewa ulinzi na jeshi la Israel akitokea katika makaazi ya karibu ya Walowezi wa kiyahudi yanayoitwa Kiryat Arbaa, kisha kuanza kuwamiminia risasi Waumini ndani ya Msikiti huo.

Gaidi huyo aliyetumia bunduki inayosadikika ni ya kijeshi ya jeshi la Israel alidhamiria kuuwa Waumini wengi kadiri iwezekanavyo ili kujenga khofu Waislamu katika mji wa Alkhalil, ambao ndio mji mkubwa katika Ukanda wa Magharibi unaokaliwa na Waislamu 99. 5%

Hatimae gaidi Baruch Goldstein alidhibitiwa na manusura na kuuwawa. lau asingedhibitiwa angeuwa watu wengi zaidi

Mayahudi wengi wakiwemo viongozi wa kidini walisifu mauwaji hayo ya kikatili bila ya hatia, wakimwita gaidi Baruch Goldstein kwamba ni mtu mtakatifu na shujaa mkubwa. Aidha, wengine wamekuwa na mpaka ujasiri wa kutaka waliomuuwa gaidi huyo wakamatwe na kushtakiwa.

Mnara maalumu umejengwa kwenye kaburi la gaidi Goldstein katika eneo la Kiryat Arbaa, na mayahudi kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni huzuru kaburi hilo na kutoa heshima zao kwa muuwaji huyo.

14 Ramadhan 1441 Hijri – 07 Mei 2020 M

Masoud Msellem

Maoni hayajaruhusiwa.